23.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

Maafisa Ustawi watakiwa kubuni mbinu za kuzuia ukatili kwa Watoto

Na Mwandishi Wetu, Songwe 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu amewataka Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini kuhakikisha wanakuwa wabunifu ili Jamii itambue umuhimu wa majukumu yao.

Akizungumza na Maafisa wa Mkoa wa Songwe katika kikao kazi chenye lengo la kujadili changamoto wanazokutana nazo, Dkt. Jingu amesema Maafisa hao wana jukumu kubwa la kutatua  migogoro ya familia pamoja na kubadili fikra na mila potofu zinazochangia ukatili hususani kwa watoto

Jingu amesisitiza kuwa, Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wahakikishe wanatumia ujuzi, weledi na utaalamu wao hasa katika kulinda na kutetea maslahi ya watoto.

“Chanzo kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto ni migogoro katika familia, lazima sisi kama wataalamu katika jamii, tuone namna gani tunaweza tukaboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya familia ili watoto wetu wakue vizuri na waweze kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote,” amesema Jingu. 

Ameongeza pia Maafisa Maendeleo ya Jamii ni wataalamu wa kushughulikia na kubadilisha Jamii kwenye fikra, mila na desturi zinazoendeleza ukatili huku Maafisa Ustawi katika eneo hilo wana jukumu la kutatua migogoro na kuhakikisha haki inatendeka, ndiyo sababu wanatakiwa kuwepo wakati wa kusikiliza kesi za watoto.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Dk. Seif Shekalaghe akimkaribisha Dkt. Jingu kuzungumza na Maafisa hao amemshukuru kwa uamuzi huo kwani utawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Baadhi ya Maafisa wakimueleza Katibu Mkuu jinsi wanavyohakikisha wanapunguza tatizo la ukatili wamesema wanashirikiana na wadau mbalimbali kama vile viongozi wa Dini ambapo hivi sasa matukio ya ukatili yamepungua.

“Elimu zimeendelea kutolewa kuanzia ngazi ya chini hususani Viongozi wa Dini na Viongozi wa mila ili wakawaelimishe wananchi katika maeneo yao,” amesema Mariam Daniel, Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.

Aidha, Ritha Kamenya na Daud Mdaki wamesema kikao na Katibu Mkuu kimekuwa na manufaa kwao kwani kimewapa nguvu ya kuendelea kufanya kazi kwa juhudi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,244FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles