23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Maafa ya tetemeko Kagera isiwe mtaji kwa walafi

pg-41

Na Tobias Nsungwe,

WAATHIRIKA wa tetemeko lililotokea mkoani Kagera hivi karibuni, wanahitaji huduma za haraka ili warudi katika hali yao ya awali.

Porojo, matamko na ziara za wanasiasa wanaopitapita mkoani Kagera ‘kutathmini’ athari  zake havina tija kama waliobomokewa na nyumba zao wanazidi kulala nje, bila chakula, mavazi na maji.

Haitakuwa busara kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) au vyama vya upinzani kuitumia Kagera kama uwanja wa kupigana vijembe vya kisiasa au kutoa misaada kwa kufuata itikadi.

Maafa yanapotokea hayabagui mtu. Walioshikwa na janga la tetemeko Bukoba na mkoani Kagera ni watu wanaofuata dini tofauti tofauti. Itakuwa si uungwana kwa watoa misaada kutoa misaada hiyo kwa misingi ya dini.

Ikiwa taasisi au mtu ni Muislamu, ajue ana wajibu wa kutoa misaada kwa waathirika wote. Wakatoliki na Wakristo wengine nao hawapaswi kubagua wanapotoa misaada yao.

Viongozi wa vitongoji na vijiji, madiwani na viongozi wengine walio karibu na kaya zilizopata matatizo hayo, wanao wajibu kwa Mwenyezi Mungu na taifa kufanya hesabu na kutoa taarifa za uhakika juu ya mahitaji halisi ili Serikali na watoa misaada wengine wawe na uhakika kwamba misaada inawafikia walengwa.

Njama zozote za kupotosha taarifa kwa nia ya kujinufaisha na maafa hayo, lazima zilaaniwe.

Uaminifu wa mabalozi wa nyumba kumi kumi, viongozi wa vijiji, vitongozi na kata na hata madiwani utapimwa sana kutokana na jinsi wanavyoratibu utoaji misaada kwa walengwa halisi wa tetemeko lile.

Tumezoea kuona vibaka wakiwaibia abiria pindi zitokeapo ajali. Hatutarajii kuona viongozi wa Serikali za mitaa wakijigeuza vibaka na kuiba fedha na vifaa vinavyopelekwa Kagera kwa lengo la kuwasaidia waliopatwa na mikasa ya tetemeko.

Viongozi wasithubutu hata kufikiria tu kunufaika na misaada ya tetemeko. Haipendezi pia kulitumia sakata hilo kutaka kujiimarisha kisiasa.

Hatutegemei kuona baadhi ya viongozi wakijenga mahekalu kwa fedha za misaada. Sakata la Kagera halikuja ili baadhi ya watu walitumie kupata sifa na au kuuza sura kwenye runinga na magazeti.

Kinachotakiwa ni kwa nchi kutumia tetemeko hilo kuungana ili kama taifa kutafuta njia mwafaka ya kuwa tayari wakati wowote yanapotokea majanga. Zaidi ya kaya 126,000 zimeathiriwa na tetemeko lile, huku nyumba16,667 zikiwa zimeharibika na 9,471 zikipata nyufa. Ingawa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu, amekuwa akiendelea kupokea misaada kutoka sehemu na taasisi mbalimbali, hali bado inaelezwa kuwa mbaya.

Kokosekana takwimu sahihi na za kutosha kuhusu waathirika halisi bado ni kikwazo. Hili linaweza kutumiwa na matapeli kupeleka misaada hiyo kwa wasiostahili. Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu mkoani Kagera, Robi Wambura, amesema mpaka sasa wamesaidia kaya 2,000, huku wakikabiliwa na changamoto ya kupata takwimu sahihi ambazo zingewawezesha kufikia waathirika wengi zaidi.

Tetemeko la Kagera likiamshe kitengo cha maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa siku zote kiwe tayari kutoa misaada sehemu na wakati wowote wanachi wanapopatwa na majanga. Jukumu la kwanza la Serikali ni kulinda uhai wa wanachi wake.

Yanapotokea majanga kama la Kagera, watu na taasisi mbalimbali hujitokeza kutoa misaada. Hata hivyo, ukweli unabaki kwamba jukumu la kusaidia wananchi wanapopatwa na shida linabaki kuwa la Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles