Na EVANS MAGEGE
-DAR ES SALAAM
MAABARA ya teknolojia ya hali ya juu ya uchambuzi na uongezaji thamani madini ya vito iko mbioni kufunguliwa nchini.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe, maabara hiyo itarahisisha shughuli za utafiti, uchambuzi na uthaminishaji wa madini mbalimbali yanayochimbwa Afrika.
Profesa Mdoe alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 37 wa mwaka wa Kituo cha Madini Afrika.
Alisema ujenzi wa maabara hiyo unatokana na maazimio ya mkutano wa mwaka jana ambayo yalinuia kukiwezesha kituo hicho kujiendesha chenyewe.
“Malengo tuliyojiwekea mwaka jana ni kuongeza thamani ya madini, kufanya utafiti na kujiwezesha. Pia kusaidia nchi hizi katika kufanya uchambuzi wa madini mbalimbali na kuweka kazidata za sayansi ambazo awali zilikuwa za kanda lakini kwa sasa ni za Afrika.
“Kwa mfano ukitaka kujua kuna madini gani Tanzania unapata na hata ukitaka kujua ukanda fulani una madini ya aina gani na ni kiasi gani utapata.
“Kwa hiyo malengo ya mwaka jana ni kukiwezesha chuo kijisimamie na kiweze kujiendesha kwa njia ya kuwa na miradi yake, kwa mfano wa kujenga maabara ya teknolojia ya hali ya juu. Na sasa inabidi tuone ujenzi umefikia wapi ili tuifungue,” alisema Profesa Mdoe.
Awali Profes Mdoe alisema kuwapo Kituo cha Madini Afrika nchini kumenufaisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosomea jiolojia na uchakataji wa madini ambao wamekuwa wakikitumia kituo hicho kwa mazoezi ya masomo yao.
Awali alisema nchi wanachama wanalipa ada ya dola 62,000 kwa mwaka hivyo kwa nchi mwanachama inayohitaji huduma za kituo hicho inapunguziwa asilimia 40 ya gharama za kazi husika.
Mkurugenzi wa Jiolojia kutoka Wizara ya Nishati na Madini ya Kenya, Shadrack Kimomo alisema kituo hicho kimewasaidia kupika wataalamu wengi wa madini nchini mwake.
Alisema kituo hicho kimesaidia Serikali ya Kenya kujenga kituo chake cha kuchambua madini ya vito.
“Wataalamu wengi nchini kwetu wanategemea kituo hiki kwa kupata ujuzi zaidi …napenda kuweka wazi bila kituo hiki na sisi huko Kenya tusingeweza kujenga chetu,” alisema Kimomo.