24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Maabara Mkemia Mkuu ilivyoleta mabadiliko Kanda ya Ziwa

Ma AVELINE KITOMARY

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imekuwa na nafasi kubwa katika vipimo vya utambuzi na udhibiti wa kemikali.

Wakati wa kuanzishwa kwake lengo kuu lilikuwa ni kufanya utafiti wa magonjwa ya ukanda wa joto (tropical disease) mwaka 1895 na magonjwa yaliyolengwa kwa wakati huo yalikuwa ni malaria na kifua kikuu.

Baada ya uhuru, maabara hiyo ilikuwa ni idara ndani ya Wizara ya Afya lakini kwa sasa ni mamlaka inayojitegemea kutokana kuundwa rasmi kisheria kupitia Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na.8 ya mwaka 2016.

Maabara hiyo ina jukumu la kufanya uchunguzi wa kitaalamu au kisayansi wa sampuli mbalimbali zinazotokana na makosa ya jinai, usalama na ubora wa bidhaa, masuala ya kijamii na usalama wa afya kazini.

Licha ya majukumu hayo, inasimamia utekelezaji wa sheria za udhibiti
wa kemikali viwandani na majumbani na kudhibiti matumizi ya vinasaba vya binadamu na kutoa ushahidi wa kitaalamu mahakamani kwenye mashauri yote yanayohusisha uchunguzi wa kimaabara.

Majukumu mengine ni kutoa ushauri wa kitaalamu na mchango katika tiba kwa kushirikiana na hospitali mbalimbali ndani ya nchi ikiwamo huduma za upandikizaji wa figo na utambuzi wa jinsia tawala kwa watoto waliozaliwa na jinsia mbili.

Uimarishaji wa sekta ya afya unaofanywa na serikali ya awamu ya tano umeweza kufanya huduma za uchunguzi wa sampuli, uchunguzi wa ubora wa bidhaa na uchunguzi wa uchafuzi wa mazingira.

Mafanikio ya maabara hiyo yanaendelea kuonekana hasa katika Kanda ya Ziwa ambapo maabara sasa imekuwa na uwezo mkubwa wa kupima sampuli za aina mbalimbali ikiwamo ile ya mazingira.

Kanda ya Ziwa inajumuisha mikoa Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera na Kigoma.

Akizungumza wakati wa Kampeni ya ‘Tumeboresha sekta ya Afya’ inay- oendeshwa na Maofisa habari wa Wizara ya Afya na Taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo, Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa, Boniventure Masambu, anasema maabara hiyo ilizinduliwa Januari mwaka 2005 ili kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma.

“Huduma tunazotoa ni uchunguzi wa sampuli za makosa ya jinai kama ubakaji, sumu, mauaji na dawa za kulevya. Nyingine ni uchunguzi wa ubora wa bidhaa, uchunguzi wa uchafuzi wa mazingira unaolenga kulinda afya na mazingira na kutoa ushahidi wa kitaalamu mahakamani.

“Huduma zingine ni usimamizi na udhibiti wa kemikali, hapa tunafanya uk- aguzi wa maeneo yenye kemikali, usajili wa maeneo yenye kemikali, usimamizi na udhibiti wa kemikali katika mipaka iliyoko kanda ya ziwa, kutoa vibali vya kusafirisha, kuingiza na kuuza nje ya nchi kemikali,” anaeleza.

Mamlaka upande wa Kanda ya Ziwa pia inafanya tafiti mbalimbali ili kuweza kuendana na teknolojia ya sasa.

Uwekezaji wa miundombinu wezeshi ya uchunguzi wa sampuli umefanya uchunguzi wa maabara kuongezeka kutoka sampuli 1,085 mwaka 2015 hadi kufikia sampuli 7,193 mwaka 2019.

Masambu anasema ununuzi wa miambo umechangia kuboreshwa kwa huduma zinazotolewa hivyo kupunguza muda wa kuchungaza sampuli kwa kusaidia sampuli nyingi kuchunguzwa hapo badala ya kupelekwa makao makuu.

“Muda wa kufanya uchunguzi wa sampuli zinazoletwa maabara umepungua kutoka siku 30 mwaka 2015 hadi siku 10 mwaka 2019 kwa sampuli ambazo hazihitaji kupelekwa kwenye maabara zingine kwa uchunguzi.

“Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi sasa sampuli
zote huchunguzwa sumu katika maabara hii. Vifaa vya kisasa vya GC vimewezesha sampuli hii kufanyika hapa na kupunguza muda wa kuchunguza na kutoa majibu,” anabainisha.

Anasema uchunguzi wa dawa za aina zote za kulevya unafanyika katika kanda hiyo hatua ambayo imerahisisha kuharakisha kesi mahakamani.

“Ofisi ya kanda imekuwa ikishiriki katika vikao vya kusukuma mashauri mahakamani na maabara ya kanda imesaidia kuharakisha mashauri yalioyopo mahakamani, vikao hivi vimekuwa vikifanyika kila baada ya miezi mitatu.

“Kanda imeshiriki katika vikao vyote vya mahakama kuu, Mahakama ya Mkoa wa Mwanza na wilaya zake, pamoja na kushiriki vikao vya kuharakisha kesi huku wataalamu wa kanda wakiwa wamehudhuria jumla ya mashauri 436 kwaajili ya kutoa ushahidi ambao ni wasatani wa mashauri 188 kwa mwaka,” anafafanua Masambu.

SAMPULI ZA UCHAFUZI MAZINGIRA

Masambu anasema katika kipindi cha miaka minne serikali ilinunua mitambo ya AAS na DR 5000 iliyowezesha uchunguzi wa sampuli za uchafuzi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Masambu, matokeo ya tafiti za mazingira zinazofanywa yanatumiwa na serikali katika kuchukua hutua za kisheria.

“Jumla ya plant nane, elusion plant nne za uchenjuaji wa dhahabu na maeneo ya kilimo ya Serengeti yaliyosababisha uchafuzi wa mazingra katika Kanda ya Ziwa, sampuli zake zilifanyiwa uchunguzi na maabara hii.

“Sampuli za uchafuzi wa mazingira za migodi midogo na mikubwa iliyoko Kanda ya Ziwa zilifanyika katika maabara hii, itakumbukwa katika kipindi hicho kulikuwa na mgogoro mkubwa wa uchafuzi wa mazingira wa Kampuni ya Mgodi ya Acacia North Mara.

“Maabara hii ilihusika katika hatua zote za uchunguzi wa jumla ya sampuli 210 ambazo zilichukuliwa katika vipindi tofauti na majibu yake ndio yalitumiaka katika uamuzi wa serikali,” anasema.

SAMPULI ZA KEMIKALI

Sheria ya udhibiti na usimamizi wa kemikali za viwanda na majumbani namba 3 ya mwaka 2003 inaitaka mamlaka kusimamia uzalishaji, utunzaji, usafirishaji, utumiaji na utupaji wa kemikali ili kulinda afya

ya wananchi na mazingira. Kutokana na matakwa ya kisheria, kanda hiyo imekuwa ikifanya ukaguzi, uelimishaji na utoaji vibali ikiwa ni njia ya kudhibiti na kusimamia matumizi ya kemikali nchini.

Masambu anasema kanda hiyo ina wakaguzi katika mipaka mitano ya Kanda ya Ziwa ili kuhakikisha ukaguzi wakati wa uingizwaji wa kemikali.

“Ukaguzi wa ndani wa maeneo yenye kemikali umeongezeka kutoka maeneo 151 mwaka 2015 hadi kufikia 213 mwaka 2019.

“Kanda imeendelea kutoa vibali vya kuingiza na kutoa kemikali nchini kupitia mipaka ya Kanda ya Ziwa, vibali vilivyotolewa vimeongezeka kutoka 1,350 hadi 2,246; kutokana na ongezeko hilo, wadau wengi waliokuwa wanapitisha kemikali bila vibali sasa wanafuata sheria na kuzuia kemikali hatarishi.

Anasema usajili wa maeneo yenye kemikali umesaidia kutambua maeneo yanayotunza kemikali na kujua matumizi yake katika maeneo hayo.

“Hii husaidia kuzuia matumizi yasiyofaa ya kemikali hasa yanayoendana na uharibifu, katika zoezi hilo maeneo yaliyosajiliwa yameongezeka kutoka 72 mwaka 2015 hadi maeneo 213 mwaka 2019,” anaeleza Masambu.

Anasema mafanikio mengine yaliyopatikana ni utoaji elimu juu ya faida ya matumizi salama ya kemikali na kusababisha ongezeko la wachenjuaji na wauzaji.

“Watumiaji wa kemikali katika uchenjuaji wameongezeka kutoka 183 mwaka 2015 hadi 592 mwaka 2019 ongezeko hilo limeongeza wauzaji wa kemikali kutoka 15 mwaka 2015 hadi kufikia 92 mwaka 2019. “Kuongezeka kwa wauzaji kumeongeza wasafirishaji kutoka 0 hadi 14 mwaka 2019,” anabainisha.

Anasema hatua zote zimekuwa na mafanikio makubwa katika kanda kutokana na kazi iliyofanywa na serikali.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles