30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Maabara binafsi za afya zatakiwa kufuata sheria, kutoa majibu sahihi

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAMILIKI wa maabara binafsi za afya wametakiwa kufuata sheria na taratibu zinazosimamia uendeshwaji wake ili kutoa majibu sahihi yatakayosaidia upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maabara binafsi za afya katika wilaya zote za Dar es Salaam, Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi  za Afya nchini, Dominic Fwiling’afu alisema lengo la ukaguzi huo ni kuangalia hali ya utoaji wa huduma za maabara mkoani Dar es Salaam.

Alisema wameamua kukagua ikiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za maabara ambazo zitawasaidia matabibu kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

“Katika ukaguzi wetu tumepita katika wilaya zote za Jiji la Dar es Salaam, tumefanya ukaguzi, tumetoa elimu , ushauri na maelekezo mengine ili kuboresha huduma,” alisema Fwiling’afu.

Alisema pia kuna baadhi ya maabara zimelazimika kufungwa kutokana na kuendeshwa kinyume na sheria Na. 10 ya mwaka 1997 jambo ambalo ni kuhatarisha maisha ya Watanzania wanaofika kupata huduma katika vituo hivyo.

Alisema zipo maabara ambazo zimepongezwa kwa kutoa huduma bora kwa kufuata sheria na miongozo na hivyo kupelekea wananchi kupata huduma bora za Maabara. 

Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Maabara Wilaya ya Ilala, Petrobas Hassan aliishukuru Wizara ya Afya kwa kufanya ukaguzi huo katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa kuna maabara nyingi na zinahitaji kujengewa uwezo ili zitoe huduma bora kwa wananchi.

“Naishukuru sana Wizara ya Afya kupitia Bodi ya Maabara Binafsi za Afya,  kwa kuja kufanya ukaguzi huu, mimi kama maratibu nimefarijika sana maana ninaowasimamia wamepata elimu, ushauri pamoja na maelekezo mengine yanayolenga kuboresha huduma, hivyo nashauri ukaguzi huu ufanyike mara kwa mara ili kuendelea kuboresha huduma,” alisema Hassan.

Mtaalamu wa maabara kutoka kituo cha Ibrahim Haji cha Dar es Salaam, Deogratious aliishukuru Wizara ya Afya  kwa kufanya ukaguzi na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa maabara jambo ambalo limewaongezea ujuzi na maarifa katika kufanya kazi zao za kila siku na kuhakikisha wananchi wanapata majibu sahihi kwa wakati ili kupata tiba bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles