25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ma-RC, DC wakati wowote

Kassim Majaliwa*Elimu, uzoefu na ukada kutumika kwenye mchujo mpya

*Wazee, wagonjwa na walioshindwa uchaguzi mkuu kutupwa

Na Elias Msuya

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wakati wowote kuanzia sasa uteuzi mpya wa wakuu wa mikoa na wilaya utafanyika.

Amesema watakaoteuliwa baada ya kuapishwa watasainishwa tamko la ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.

Akizungumza jana Ikulu ya Magogoni katika hafla ya kuapishwa kwa makatibu na manaibu katibu wakuu, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kudhibiti utendaji wa viongozi wa umma kwa kila mmoja akiteuliwa kusaini tamko la ahadi ya uadilifu.

“Kama ambavyo leo hii makatibu wakuu wameanza, utaratibu huu utaendelea pia kwa wakuu wa mikoa watakaoteuliwa wakati wowote kuanzia sasa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya watakaoteuliwa.

“Kila mmoja atakuwa anakuja kuapa mbele ya kamishna wa maadili ili kulithibitishia taifa kuwa atawatumikia na kuwahudumia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema utendaji wa viongozi wa umma lazima uwe wa uwazi, uadilifu na uaminifu utakaoleta matokeo yanayotarajiwa na wananchi ambao ndiyo walengwa wa kupewa huduma.

“Shughuli zetu pia zinakwenda na mpango wa fedha na maendeleo ya kitaifa ambayo lazima itekelezwe. Mipango mingi inatengewa fedha zitakazopelekwa kwenye maeneo hayo. Nyie makatibu wakuu ndiyo mtakuwa mnaanza na mambo hayo na kuelekeza Serikali za mitaa kwa utekelezaji,” alisema Waziri Mkuu.

Akizungumza kuhusu wakuu wa wilaya alisema wanapaswa kusimamia na kufuatilia matumizi ya rasilimali fedha zote zitakazokwenda kuwahudumia wananchi.

“Wakuu wa wilaya kama wasimamizi wa Serikali ndiyo watakaowakilisha wilaya zao zitakazokuwa na halmashauri moja hadi mbili, kwamba fedha iliyoletwa kwenye wilaya yake na halmashauri lazima itumike kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema.

Aidha, aliwataka Watanzania kuendelea kujenga imani kwa Serikali kwa kuwa itaendelea kusimamia maendeleo na hasa ambayo Rais na Makamu wa Rais waliyaahidi wakati wa kampeni.

Alisisitiza kuwa upo uwezekano wa uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya kuegemea zaidi kwenye kiwango cha elimu, uzoefu, kujitoa kwa makada wa CCM katika harakati za uchaguzi, umri na hali ya afya.

Kauli hii ya Waziri Mkuu imekuja huku kukiwa na tetesi kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ambao baadhi ya majimbo wanayoyasimamia yaliangukia kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu wa 2015 huenda wakapoteza nafasi zao.

Mikoa ambayo imekuwa ikitajwa sana ni pamoja na Dar es Salaam, ambapo CCM imeambulia majimbo manne kati ya 10 yaliyochukuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).

Mkoa mwingine ni Kilimanjaro ambao CCM imeambulia majimbo ya Mwanga na Same Magharibi, huku majimbo mengine manane yakienda Chadema na NCCR Mageuzi pamoja na mikoa ya Arusha, Manyara, Mbeya, Lindi na Mtwara ambako CCM ilifanya vibaya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Mbali na kampeni za uchaguzi, tetesi hizo zimekuwa zikidai kuwa katika uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya, inaelezwa kuwa huenda kigezo cha umri na hali ya afya kikatumika kuwaondoa baadhi ambao ni wazee na wanaosumbuliwa na maradhi.

Kwamba kigezo cha elimu na uzoefu pia kinaweza kutumika ili kuleta ufanisi katika kuendana na kasi ya utendaji kazi ya Serikali ya awamu ya tano.

Baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa kigezo cha kuzingatia elimu katika uteuzi wa nafasi hizo linaonekana wazi katika uteuzi uliokwishafanywa wa mawaziri na makatibu wakuu wa wizara ambao wengi wao kiwango cha elimu ni uprofesa, shahada ya uzamivu na uhandisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles