30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ma-DED marufuku kusimamia uchaguzi

PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imebatilisha kifungu cha sheria cha namba 7(1) na 7(3) kinachowaruhusu wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi nchini.

Kesi hiyo namba 8/2018, awali ilikuwa inasikilizwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na aliyekua Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambari, ambaye kwa sasa amehamishiwa Mahakama ya Rufaa, Jaji Rehema Sameji, ambaye pia yupo Mahakama ya Rufaa na Jaji Temba amestaafu.

Kesi hiyo ambayo mjibu maombi alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ilifunguliwa na Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, aliyekuwa akiwakilishwa na Wakili Fatma Karume (ambao ndio waleta maombi) na walikuwa wanapinga kifungu cha sheria ya vyama vya siasa kinachotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwateua wakurugenzi hao kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo jana, Jaji Atuganile Ngwala, alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, kifungu namba 7(1) na 7(3) ni batili kwa sababu kinatoa nafasi kwa wateule wa Rais ambao pia si waajiriwa wa NEC kusimamia uchaguzi.

Alisema kifungu cha 7(1), kinasema kuwa kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.

Alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na Katiba mama ambayo inasimamia nchi.

Alisema lakini pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.

Alisema lakini Katiba inasema kuwa mtu yeyote aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Alisema kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa waleta maombi, vimeonyesha pasi na shaka kuwa wasimamizi wa uchaguzi wana masilahi na wateule wao.

Alisema kutokana na hali hiyo, mahakama imeona kuwa vifungu hivyo ni batili na kwamba havifai kutumika wakati wa kusimamia uchaguzi.

“Mahakama imebatilisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi namba 7(1) na 7(3) kutokana na NEC kuteua wakurugenzi wa Jiji, halmashauri na manispaa kuwa wasimamizi wa uchaguzi wakati ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC,” alisema Jaji Ngwala.

NJE YA MAHAKAMA

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili Fatma, alisema hukumu hiyo ni ya kihistoria baada ya mahakama kubaini vifungu namba 7(1) na 7(3) kuwa ni batili kutumika katika sheria ya uchaguzi.

Alisema kutokana na sababu hiyo, inaonyesha wazi kuwa miaka yote wananchi walikuwa wanasimamiwa uchaguzi na viongozi wasio sahihi.

“Miaka mingi tulikua tunapiga kelele kuhusiana na udhaifu wa baadhi ya vifungu katika sheria ya uchaguzi kuwa ni batili na kwamba vinaegemea kuwalinda viongozi wa CCM, sasa mahakama imeona hiyo na kuwa vifungu hivyo havifai, pia vifutwe au Serikali ipeleke muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi bungeni ili vibadilishwe,” alisema Fatma.

Alisema katika kesi hiyo, walipeleka vielelezo vya kuonyesha wakurugenzi 74 ambao ni wanachama wa CCM, wamevalia sare cha chama hicho na wao ndio wasimamizi wa uchaguzi, wakusanyaji wa makaratasi ya uchaguzi, wapanga matokeo na watangazaji wa matokeo, jambo linaloonyesha wazi kuwa hawawezi kutangaza matokeo sahihi bila ya kulinda masilahi ya chama chao.

Alisema kitendo hicho kinawanyima haki vyama vingine kupata mshindi kwa sababu anayesimamia uchaguzi tayari ana mgongano wa masilahi na chama chake.

Alisema kutokana na hali hiyo, kila mwananchi ana haki ya kwenda mahakamani kudai haki pale anapoona kuna ukiukwaji wa sheria katika maeneo tofauti.

Naye Wangwe aliishukuru mahakama kusimamia haki katika kesi hiyo na kutoa hukumu inayoonyesha wazi kuwa imetenda haki.

“Katika hili lazima tuishukuru mahakama kwa kusimamia na kutoa hukumu ya haki, kwa sababu ma-DED siku zote wamekuwa wakilinda masilahi ya waajiri wao kwa kutangaza matokeo yasiyo sahihi katika chaguzi mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles