26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

MA-DC WAKALIWA KOONI BUNGENI

Na ELIZABETH HOMBO

-DODOMA

WABUNGE wamewashukia wakuu wa wilaya wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kupoka uenyeviti wa mitaa na vijiji.

Hali hiyo ilijitokeza juzi jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha vifungu vya bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambayo ni Sh bilioni 821.3.

Wakati wa kupitia vifungu vya bajeti hiyo, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF), aliitaka Serikali kutoa kauli kuhusu wakuu wa wilaya wanaotumia madaraka yao vibaya.

“Hivi sasa wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia ovyo madaraka yao kwa kuwapoka wenyeviti wa mitaa na vijiji madaraka yao,” alisema.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisema sheria ya Serikali ya Mitaa imempa mamlaka mkuu wa wilaya kuwepo katika mkutano ulioitishwa na kijiji ama mtaa.

“Sheria inamtaja kwamba mkuu wa wilaya atasimamia upigaji kura wa kuamua kuhusu wenyeviti ndiyo maana wanakuwepo pale na si kwa namna nyingine,” alisema Simbachawene.

Pamoja na hilo, Ngombale ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), aliitaka Serikali kutoa kauli kuhusu jambo hilo na kushikilia shilingi katika mshahara wa waziri ili wabunge wajadili jambo hilo.

Naye Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalllah Salim (CUF), aliunga mkono hoja ya Ngombale na kutoa mfano wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mdeme, akisema anatumia vibaya madaraka yake.

“Mfano halisi ni wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma anatumia vibaya madaraka yake, alikwenda Mtaa wa Mlimwa Kusini na akamwachisha uenyekiti mwenyekiti wa mtaa,” alisema.

Naye Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alisema wakuu wa wilaya wanakwenda katika mitaa na kuwaondoa madarakani wenyeviti bila kufuata utaratibu wa kisheria.

“Wakuu wa wilaya wanakwenda katika mitaa hata hawawaulizi wananchi, wala watuhumiwa hawapewi muda wa kujitetea katika tuhuma zao,” alisema.

Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, alisema hakuna haja ya kubishana kuhusu hoja hiyo kwa sababu wakuu wa wilaya wamekuwa wakiwaonea wananchi kwa kuwaondoa wenyeviti.

“Mfano katika Kijiji cha Msangani Kibaha yule DC Assumpta Mshama alimweka ndani mwenyekiti kwa sababu tu alikataa kumkabidhi fedha za wanakijiji bila ridhaa ya waliochanga,” alisema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso, alisema wakuu wa wilaya wamekuwa wakiendesha mikutano inayohusu kutoa uamuzi wa uongozi wa kijiji hata bila kujali akidi.

“Wamekuwa wakifanya mikutano ya uamuzi bila hata kujali akidi ya nusu ya wana mtaa ama kijiji imehudhuria,” alisema.

Pareso alisema wakuu wa wilaya wamekuwa wakifanya mambo yasiyo katika majukumu yao.

“Mfano DC wa Arumeru, Mnyeti (Alexander), anataka wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ndio wapitishe bajeti, haipo hiyo. Hawa ma DC waliopo wakati huu ni zaidi ya wale waliokuwepo wakati wa ukoloni,” alisema.

Hata hivyo, hoja ya kutaka Serikali kutoa kauli ilipingwa na mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, baada ya kusema hakuna haja ya kutoa tamko kwa sababu tayari kuna sheria.

Mawaziri waliopinga ni pamoja na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama na Simbachawene.

Masaju alisema mamlaka ya wakuu wa wilaya yamewekwa katika sheria na hayawezi kutolewa tamko.

“Kauli unatoa mahali hakuna sheria. Kwanini hamkwenda mahakamani kama mnaona kuna ukiukwaji wa sharia,” alihoji.

Kwa upande wake, Mwigulu, alisema wakuu wa wilaya ni wakuu wa kamati za ulinzi na usalama, ni wajibu wao kuhakikisha kuwa maeneo yao yanakuwa na amani.

Baada ya mabishano hayo, Ngombale, alikubali kurudisha shilingi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles