KLABU ya Lyon imejiondoa katika mipango ya kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa timu ya Arsenal, Manchester City na Tottenham, Emmanuel Adebayor (32).
Adebayor ambaye ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na klabu ya Crystal Palace, alikuwa mbioni kujiunga na timu ya Lyon.
Nyota huyo wa Togo, Ijumaa iliyopita alikuwa jijini Lyon, Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo na kocha wa Lyon, Bruno Genesio.
Lakini klabu hiyo haikukubaliana na nyota huyo kutokana na umri wake kuwa mkubwa, huku ikidai kwamba atashindwa kuwa na msaada katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo timu hiyo inashiriki msimu huu.
Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), pia ilidai haitafurahishwa na hatua za kumkosa mchezaji huyo kwa miezi miwili ya msimu huu wakati akiwa na timu yake ya taifa katika Kombe la Mataifa barani Afrika.
Katika hatua nyingine, Lyon ilisema ina furaha kumsajili mshambuliaji mwengine, Jean Phillipe Mateta, baada ya Adebayor kusema kuwa angependa kuliwakilisha taifa lake katika kombe la bara Afrika mapema 2017, hatua ambayo ingemfanya kutochezea timu hiyo kati ya mwezi mmoja hadi miwili.