NA JESSCA NANGAWE
KIKOSI cha Kagera Sugar kinatarajia kushuka dimbani Agosti 12, kuumana na Yanga, katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi cha Kagera Sugar kwa sasa kimepiga kambi jijini Dar es Salaam, kikijifua kwaajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utaanza Agosti 26.
Akizungumza na MTANZANIA, Kocha wa Kagera, Mecky Mexime, alisema mchezo huo ni maalumu kwaajili ya kuchangia damu.
“Mchezo huu ni maalumu kwa ajili ya kuchangia damu salama, lakini pia ni sehemu ya maandalizi yetu ya msimu ujao.
“Keshokutwa timu itarudi Kagera, ambako kambi yetu ya kudumu ipo na kuendelea na mazoezi pamoja na ratiba ya mechi za kirafiki,” alisema Mexime na kuongeza:
“Hata hivyo, kabla ya kukutana na Yanga, Agosti 9 tutacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Stand United.”
Alisema anaamini mchezo wao na Yanga na Singida United utakuwa kipimo sahihi kwao kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu kuanza.
Kagera ilimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa nafasi ya tatu, nyuma ya Simba, iliyokamata nafasi ya pili na Yanga iliyotwaa ubingwa.