LWANDAMINA ATUA, KUANZA MAHESABU YA MSIMU MPYA

0
643
KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, George Lwandamina,
KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, George Lwandamina,

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, George Lwandamina, amewasili jana nchini tayari kuanza maandalizi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lwandamina ambaye alikuwa Zambia kwa mapumziko marefu mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, aliifanikisha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 68 katika msimamo, ikiwa sawa na Simba zikitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mbali na ligi timu hiyo ina kibarua kizito cha mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi Simba, unaotarajiwa kupigwa Agosti 19, mwaka huu  katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Hadi sasa wachezaji waliowekwa wazi kusajiliwa na Yanga ni beki Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’ kutoka Jang’ombe Boys ya Zanzibar, kiungo Pius Busitwa kutoka Mbao FC, huku ikiwaongezea mikataba wachezaji wao wa zamani, Donald Ngoma na Amiss Tambwe.

Pia Wanajangwani hao ambao wamepanga kufanya usajili wao kimya kimya, wamepania kuona wanafanya vema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu ili waweze kufika mbali zaidi tofauti na misimu ya nyuma.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Lwandamina alisema atapanga ratiba ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.

“Nilikuwa mapumzikoni nyumbani, lakini natarajia kuanza ratiba ya mazoezi muda wowote kuanzia sasa baada ya kumalizi likizo yangu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here