29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi hagombei Uspika-Rais Samia

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi hatogombea nafasi ya uspika na badala yake atampa kazi maalum.

Pia,ametangaza kumpa kazi aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa.Palamagamba Kabudi ya kusimamia mikataba ambayo Serikali itaingia na wabia. 

William Lukuvi.

Itakumbukwa Januari 8, mwaka huu Rais Samia alifanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa kutowateua Lukuvi na Prof. Kabudi hatua ambayo ilizua minongono kwa baadhi ya watu.

Akizungumza leo Januari 10,2021, mara baada ya kuwaapisha Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu Ikulu Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia amesema akiwatizama Lukuvi na Kabudi ni kama Kaka zake hivyo kutokana na uzoefu wao katika kazi hatowaweka pembeni.

“Nina kaka zangu wawili Lukuvi (William) na Kabudi (Palamagamba) nikiwatizama hawa umri wao kama yangu na ukitizama niliowateua hamfanani kabisa, kwahiyo kaka zangu wawili hawa nimewavuta waje kwangu waje wanisimamie,” amesema Rais Samia.

Amesema Prof. Kabudi amefanya kazi nzuri katika kusimamia mazungumzo ya serikali katika mikataba hivyo amemkabidhi rasmi kazi hiyo licha ya kwamba haipo katika mfumo.

Profesa Palamagamba Kabudi.

Amesema Mashirika yote kazi zake ambazo zitaingia ubia na serikali Prof. Kabudi ataongoza yote huku akimuita Baba wa  mikataba.

“Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya serikali na mashirika na ndiyo kazi ambayo sasa nataka kumkabidhi kindaki ndaki aendelee na kazi hiyo ila kazi yake kwa sababu haipo katika muundo haitangazwi wala nini na yeye ndio atasimamia kazi hiyo,” amesema Rais Samia.

Kuhusu Lukuvi amesema atakuwa na kazi nae hivi karibuni na huku akiwataka watu kupuuza maneno maneno yanayoendelea ya  kwamba atagombea uspika.

“Kaka yangu Lukuvi yeye  atakuwa na kazi na mimi mtaisikia baadae, lakini namvuta Ikulu kazi yake ni kutusisimamia kwa sababu nikiwatizama hapo wote wanakaribia kustaafu miaka 2 wengine bado mna safari ndefu, sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na makatibu wakuu kwahiyo nimeona meseji afadhali Lukuvi katoka hajatoka yupo.

“Wengine wameanza kumletea meseji za ajabu ajabu wakijua atagombea uspika, hatagombania anakazi na mimi, kwahiyo hatakuwa Spika wala hatagombania kwahiyo msianze kumchafua ametumikia Taifa hili kwa uadilifu kwa muda mrefu mwache aende na mimi amalize kazi,”amesema.

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimuahidi Rais Samia yeye na walioapishwa leo kwamba watafanya kazi kwa matokeo chanya kama anavyotaka kuhakikisha wanawafikia na kuwahudumia wananchi mpaka katika maeneo ya vijijini.

Pia, amemuahidi kwamba watafanya kazi kwa uadilifu na uaminifu kuhakikisha watanzania wanapata maendeleo na wao waliopewa dhamana wanafanya kazi kwa weledi.

“Mheshimiwa Rais mara kadhaa umekuwa ukisisitiza  kufanya kazi kwa matokeo chanya naomba nirudie kukuhakikishia  kwamba kwenye mipango yetu na majukumu yetu tutahakikisha tunafanya kazi kwa matokeo chanya kuwatumikia wananchi na tunajua jukumu letu la kwenda kuwakuta wananchi mpaka kijijini, kwenda kuwasikiliza wananchi kule walipo na changamoto na kuwahudumia jukumu hilo tutalitekeleza,”amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amesema Rais Samia sio tu kiongozi wa serikali lakini ni Mkuu wa Nchi, kwa hiyo uongozi wake hauko sawa sawa na kiongozi yeyote wa Muhimili wowote uliopo hapa nchini.

Amesema wao kama Bunge wapo  tayari  kutoa  ushirikiano kwake

“Natoa ushauri kwenu kuwa Mheshimiwa Rais Samia amewaamini kumsaidia, hizo kazi ni kazi zake hivyo ninyi mnapoenda kuzifanya kazi hizo fanyeni kama wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si vinginevyo.

“Kila mmoja ambaye ameteuliwa katika nafasi yoyote aliyoipata, Mhe. Rais Samia alishafanya kazi katika maeneo hayo kwa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali, ninawapongeza kwa sababu mnayo sehemu ya kuanzia katika kuelezea mazuri ya Serikali hii,”amesema Dk. Tulia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles