20.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 28, 2022

LUKUVI AZIAGIZA KAMPUNI ZA UPIMAJI ARDHI KUWATAFUTIA HATI WANANCHI

NA JOHANES RESPICHIUS – DAR ES SALAAM


KAMPUNI zinazohusika na shughuli za upangaji na upimaji ardhi zimetakiwa kuhakikisha zinawapatia hati wananchi ambao maeneo yao yamerasimishwa na si kuweka nondo na bikoni tu.

Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipokutana na kampuni za kupanga na kupima ardhi, watendaji wa kata, mitaa na maofisa wa wizara hiyo.

Lukuvi alisema kampuni hizo zimekuwa zikipima viwanja na kuweka bikoni kisha zinaondoka jambo ambalo limekuwa likiwagharimu fedha nyingi wananchi kutokana na mlolongo wa kupata hati.

“Nyinyi kampuni mnaofanya kazi hizi mshirikiane pamoja na wilaya kukokotoa gharama ili mwananchi apate haki na isiishie tu kupanga kwa kuweka nondo na bikoni, ninachokitaka huduma yenu ya mwisho iwe kukabidhi hati.

“Muweke gharama zote hata hiyo tozo ya primiamu na hatimaye mwananchi aitwe tu kusaini na hatimaye kuchukuwa hati yake, leo (jana) kuna kampuni zimepanga na kupima lakini wananchi hawajapata hati kwa zaidi ya miezi sita kisa anajua wapi hati zinapatikana.

“Kwa hiyo jukumu la kukabidhi hati kwa wananchi ni kampuni iliyohusika na upimaji ihakikishe inapanga, inapima na kukabidhi hati kwa mwananchi aliyerasimishwa na si unakabidhi nondo wala bikoni,” alisema Lukuvi.

Alisema atalazimika kuifuta kampuni yoyote itakayoendelea na shughuli za upangaji na upimaji ardhi bila kuhakikisha wananchi waliorasimishwa wanapata hati zao.

Pia alisema kuanzia Julai mosi, mwaka huu, Serikali ilipunguza gharama za malipo ya awali ya thamani ya ardhi iliyopimwa (premium) kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia moja ikiwa ni jitihada za kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi nchini.

“Kutokana na punguzo hili wananchi wote ambao wapo mijini ni lazima makazi yao yarasimishwe kwa sababu kikwazo ambacho kilikuwa kikilalamikiwa (premium) kimepunguzwa,” alisema Lukuvi.

Pia alisema kutokana na utafiti alioufanya kuhusu gharama za upangaji na upimaji wa ardhi amegundua kuwa kampuni hizo zimekuwa zikitoza fedha nyingi kuliko kazi wanayoifanya na kuanzia sasa kima cha juu cha gharama za urasimishaji hakipaswi kuzidi Sh 250,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,102FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles