24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi aweka rekodi akiifumua ardhi

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

UAMUZI unaofanywa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi katika wizara anayoingoza, ni wazi umekuwa ukimjengea sura mpya kila kukicha.

Lukuvi, ambaye ni miongoni mwa mawaziri waliokaa kwa muda mrefu katika wizara hiyo pasipo kukumbwa na mabadiliko aliyoyafanya Rais John Magufuli mara kadhaa, anatofautishwa na wengine kutokana na uamuzi wake, ikiwamo kufuatilia, kuwahamisha na hata kuwasimamisha kazi watumishi wanaodaiwa kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.

Waliokumbana na makali yake ni wale wanaotajwa kutokuwa waaminifu, walarushwa, kwa maana ya waliozoea fedha za ‘dili’ za viwanja.

Hatua aliyoichukua sasa na uamuzi wake kutangazwa wiki hii, ya kuwasimamisha watumishi 183 wa ardhi kwa tuhuma za kuiibia Serikali kupitia mfumo wa malipo ya kodi za pango la ardhi, ni mwendelezo wa hatua nyingine nyingi kama hizo alizochukua huko nyuma.  

Pengine kutokana na mwenendo wa utendaji wake huo, huenda ndiyo sababu ya kusalia katika nafasi hiyo tangu Rais Magufuli aunde Baraza la Mawaziri Desemba 2015, licha ya kufanya mabadiliko kadhaa ya kuwaondoa na kuwahamisha baadhi ya mawaziri.

Katika hilo, Lukuvi anaingia katika orodha ya mawaziri sita ambao hawajawahi kuhamishwa katika wizara zao.

Wengine ni Dk. Hussein Mwinyi (Ulinzi), Ummy Mwalimu (Afya), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk. Philip Mpango (Fedha) na Jenista Mhagama (Sera, Uratibu na Bunge).

Tofauti na mawaziri wote hao, Lukuvi ndiye waziri pekee ambaye amekuwa akipongezwa si tu na wananchi, bali hata wanasiasa wa upinzani ambao kwao ni nadra kufanya hivyo.

Wakati fulani Kambi ya Upinzani Bungeni ilitoa hotuba iliyosifia utendaji wa Lukuvi.

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), aliwahi kumpongeza Lukuvi, akisema anastahili kuigwa kwa kuwa ameimudu vyema wizara anayoiongoza.

Msigwa alitoa pongezi hizo Aprili, mwaka juzi, wakati Lukuvi akizindua ramani mpya ya mipango miji ya Manispaa ya Iringa katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali.

“Kwa mnaonifahamu vizuri, mimi sio mbunge wa kusifiasifia, mimi ni mbunge mwenye msimamo, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipotoa pongezi kwa Waziri Lukuvi kutokana na uchapakazi wake unaokonga nyoyo za wadau wa shughuli zinazofanywa na wizara yake,” alisema Msigwa.

Mara kadhaa Lukuvi ameonekana maeneo mbalimbali nchini, akitoa elimu ya jinsi ya kumiliki ardhi, Serikali ilivyorahisisha upatikanaji wa hati za umiliki wa viwanja, akitatua kero za ardhi kwa kurudisha nyumba na hata viwanja vilivyopokwa kiunjanja na masuala mengine muhimu kuhusu rasilimali hiyo nyeti.

WAZIRI KIVULI ANENA

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wilfred Lwakatare, alisema Lukuvi amejipambanua kuwa mfuatiliaji na kuchukua hatua, tofauti na mawaziri wengine.

Lwakatare, ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini kupitia Chadema, alieleza wasiwasi wake kuwa tatizo la mfumo linaweza kumkwamisha Lukuvi.

“Hata katika hotuba zetu, tulieleza bayana kwamba Lukuvi ni miongoni mwa mawaziri waliojipambanua kutokana na kufuatilia kila jambo na kuchukua hatua katika masuala yote ya ardhi.

“Sisi upinzani tuna wasiwasi kwa sababu hakuna mfumo ulio imara, sasa mtu peke yake hawezi kutatua matatizo kwa vile mfumo mzima ndio una matatizo, hivyo unapaswa kutengenezewa sheria kila mahali.

“Nasema hivyo kwa sababu Tanzania ni pana, sasa Lukuvi hawezi kwenda kila mahali. Ni vyema sasa tuangalie upya sheria na kanuni zetu za usimamizi,” alisema Lwakatare.    

VIONGOZI WA DINI WAMPA TUZO

Juni, mwaka juzi, viongozi wa dini walitangaza kumpa tuzo Lukuvi kutokana na utendaji wake uliojaa ubunifu na uwajibikaji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga, alipata kueleza kuwa Lukuvi amekuwa imara katika kufuatilia masuala yanayohusu ardhi, ikiwamo utatuzi wa migogoro iliyodumu muda mrefu.

“Lukuvi ameing’arisha Serikali ya awamu ya tano kwa kuendana na kasi ya Rais Magufuli. Hakika amevaa viatu vya Magufuli, hivyo tumeamua kumpa tuzo maalumu kwa ajili ya utendaji wake,” alisema Askofu Mwamalanga.

Tangu alipokabidhiwa wizara hiyo Desemba mwaka 2015, Lukuvi ambaye pia ni mbunge wa Isimani, amekuwa akifanya ziara nchi nzima na kutembelea maeneo yenye migogoro ya ardhi.

Katika ziara zake hizo, amekuwa akichukua hatua mbalimbali dhidi ya watumishi wanaobainika katika tuhuma tofauti.

ASIMAMISHA WATUMISHI 183

Uamuzi wake wa kuwasimamisha kazi watumishi 183 wa wizara hiyo kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili, unamwingiza katika rekodi ya waziri pekee kuchukua hatua kama hiyo.

Pengine katika kile kinachowiana na alichokisema Lwakatare, Lukuvi mwenyewe juzi wakati akizungumzia jinsi walivyobaini watumishi hao 183, alisema huko nyuma watendaji walikuwa wakisimamiwa na Tamisemi, lakini sasa hivi wamepata nguvu ya kuwasimamia wao.

“Tumeamua tujisafishe, kipindi kirefu kumekuwa na mchezo huu,” alisema.

Watumishi hao, ambao waziri huyo alikabidhi majina yao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi, wanadaiwa kuiibia Serikali fedha nyingi.

Taarifa ya wizara hiyo ilitaja majina ya watumishi waliopo katika mikoa 25, Arusha ikiongoza kwa kuwa na watumishi 15 waliosimamishwa.

Dodoma inafuatia kwa kuwa na watumishi 10, huku Kilimanjaro ikiwa na watumishi tisa, sawa na Mbeya.

Mikoa mingine ni Shinyanga na Pwani yenye watumishi nane kila mmoja, huku mikoa ya Mwanza, Morogoro na Manyara ikiwa na watumishi sita kila mmoja.

Mikoa mingine ni Dar es Salaam, Mara, Lindi, Songwe, Ruvuma na Kagera yenye watumishi watano kila mmoja, Iringa, Mtwara, Simiyu na Tabora ikiwa na watumishi watatu kila mkoa. 

Mkoa wa Kigoma una watumishi wanne waliosimamishwa kazi na mikoa ya Rukwa na Singida ina watumishi mmoja mmoja.

Lukuvi alichukua uamuzi huo mgumu ikiwa ni miezi miwili imepita tangu alipoyataja mashirika, taasisi na kampuni 270 zilizokuwa zinadaiwa jumla ya Sh bilioni 200 za kodi ya ardhi.

Yeye mwenyewe aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa hadi sasa jumla ya Sh bilioni 21 zimekwishalipwa na baadhi ya mashirika na taasisi hizo 270.

MAOFISA ARDHI WATATU

Novemba mwaka jana, Lukuvi aliwasimamisha kazi watumishi watatu wa sekta ya ardhi Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa tuhuma ya kushirikiana na matapeli wa viwanja.

Katika hilo, aliwaagiza maofisa hao kutokanyaga eneo la ofisi za jiji hilo hadi uchunguzi utakapofanyika na uamuzi dhidi ya tuhuma zao utakapotolewa.

Lukuvi alichukua uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza ofisi za Jiji la Arusha kutokana na kuwapo tuhuma nyingi za matapeli wa viwanja kushirikiana na baadhi ya maofisa wa ardhi wasiokuwa waaminifu kufanya utapeli kwa wamiliki halali.

Maofisa ardhi waliosimamishwa kwa tuhuma hizo ni Elizabeth Mollel, Lassen Mjema na Zawadi Mtafikikolo.

Mbali ya kusimamishwa kazi watumishi, Lukuvi aliagiza maofisa ardhi wa Jiji la Arusha kuhakikisha matapeli wote wa viwanja wanaoshirikiana na watumishi hao kutopatiwa huduma katika masuala yoyote ya ardhi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, watumishi hao wa sekta ya ardhi walikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na matapeli wa viwanja, jambo lililotia shaka utendaji kazi wao.

Hivyo, aliagiza hati zote za wito wa mahakama nchini kusainiwa na ofisa ardhi mteule au msajili wa hati ama Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda na Mwanasheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi lazima afahamishwe uwapo wa kesi husika.

ALIVYOKABIDHI POLISI MAJINA 30 YA MATAPELI WA ARDHI

Novemba 19, 2016, Lukuvi alikabidhi majina 30 ya matapeli wa ardhi kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ili wachukuliwe hatua.

Lukuvi alichukua hatua hiyo kutokana na migogoro mingi ya ardhi mijini kusababishwa na watu wanaoshukiwa kuwa ni matapeli, ambao ama hushiriki kuwauzia wananchi viwanja ambavyo tayari vina umiliki, vilivyo kwenye maeneo ya miradi ya maendeleo au kuongeza gharama za upatikanaji wa hati za ardhi.

AONDOA WOTE ARDHI MOROGORO

Mei 19, mwaka huu, aliagiza kuhamishwa watumishi wote wa sekta ya ardhi wa mkoa mzima wa Morogoro, sambamba na kuanzishwa ofisi ya Ardhi Kanda ya Mashariki.

Lukuvi alisema baada ya kutembelea Wilaya ya Kilosa, alibaini watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo wamejisahau na njia pekee ni kuwaondoa na kupata watendaji wapya.

“Majaribio mengi yamefanyika katika Mkoa wa Morogoro kama vile kupanga na kupima kila kipande cha ardhi, utoaji hati za kimila, pamoja na uamuzi wa Rais Magufuli kufuta mashamba makubwa yasiyoendelezwa. Lakini, bado mambo katika sekta ya ardhi kwenye mkoa huo hayaendi,” alisema Lukuvi.

Vile vile, Lukuvi alipiga marufuku wamiliki wa mashamba yaliyofutwa na Rais kurejeshewa kinyemela kwa kisingizio cha kuyaendeleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles