23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi awaweka mtegoni maofisa ardhi

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewasimamisha kazi maofisa ardhi wa wilaya wenye tuhuma mbalimbali, huku akitangaza kiama kwa matapeli wa ardhi.

Alisema hayo jana jijini hapa wakati wa mkutano wa wataalamu sekta ya ardhi, uliokutanisha makatibu tawala wa mikoa na maofisa ardhi wa wilaya.

Lukuvi alitangaza kuanzisha kanzi data ya matapeli wa ardhi na kuwataka wananchi kumtumia majina yao na eneo walipo ili yachapishwe katika tovuti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 “Siwatishi, lazima niwaambie ukweli. Mmeingia kwenye 18 zangu, sitomvumilia mtu, nataka mbadilike, haiwezekani kiwanja kimoja kigawiwe kwa watu watatu alafu unajiita mtaalamu uliyesoma. Acheni hayo mambo mtaungua,” alisema Lukuvi.

Alisema licha ya baadhi ya maofisa ardhi kuiingizia hasara Serikali na kuwadhulumu wananchi, amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Doroth Mwanyika, kuwachukulia hatua ikiwemo kuwasimamisha kazi.

LINDI

Alisema kuna ofisa ardhi amehamishiwa Sengerema akitokea Lindi anbako ametoa ardhi ya eneo la pwani ya bahari zaidi ya hekari 600 bila kufuata taratibu.

Alisema ofisa huyo alijichukulia uamuzi huo ikiwemo kutoa hati ya umiliki ardhi hiyo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria.

ARUSHA

Kadhalika, alisema tukio jingine limetokea mkoani Arusha ambako ofisa ardhi mwingine amesababisha Serikali kudaiwa fedha nyingi za fidia baada ya kumilikisha mtu ardhi ambayo hati yake ilifutwa na rais.

“Ardhi ambayo umiliki wake ulifutwa na rais, tena kwa wino mwekundu, ofisa ardhi huyo aliimilikisha kwa mtu mwingine, huyu naye asimamishwe kazi na achunguzwe, sasa amehamishiwa Nkasi,” alisema Lukuvi.

RUFIJI

Pia alisema alipokuwa akifanya ziara mikoani, akiwa Rufiji, ofisa ardhi wa wilaya hiyo ambaye amehamishiwa Tabora, alikuwa akimkimbia.

 “Mimi simwogopi. Hata mkuu wa wilaya na mkurugenzi hawaogopi? Na amekuwa akilalamikiwa kila mahali, huyu naye asimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike,” alisema.

KINONDONI

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, alisema kuna ofisa ujenzi ambaye amesababisha matatizo kwa kutoa kibali cha ujenzi kinyume na kile kilichotolewa na kamati ya ujenzi.

Alibainisha kuwa kamati iliruhusu kujengwa jengo la ghorofa nne, lakini ofisa ujenzi aliandika kibali cha ujenzi wa ghorofa tano.

Lukuvi alieleza pia Idara ya Ardhi katika manispaa hiyo, kuna vitendo vya rushwa kwa watumishi kuwaomba fedha watu wanaotaka kupatiwa huduma.

“Kuna binti ambaye ofisa wa Ikulu alikwenda kupatiwa huduma katika ofisi ya ardhi, lakini binti huyo baadaye alimtumia ujumbe mfupi ofisa wa Ikulu kuwa amtumie Sh 300,000 ili ampatie huduma.

“Nimeshawaeleza hili na nimearifiwa kuwa binti huyo alikuwa akifanya kazi kwa kujitolea na wameshamwondoa,” alisema.

JIJI LA DODOMA

Lukuvi alisema Kaimu Ofisa Ardhi wa Jiji la Dodoma (hakumtaja jina) amekuwa akijihusisha na vitendo vya kuomba hongo ili kutoa huduma.

“Ukifika ofisini kwake anakuelekeza uende kwa vijana ambao wapo kwenye chumba kingine, huku watakutaka muelewane kuanzia Sh milioni moja hadi Sh 50,000 wanachukua.

“Nilikupigia simu jana (juzi) uache, najua mambo mengi. Pale pia kuna vijana ambao kazi yao ni kugonga mihuri ambapo wanawatoza Sh 10,000 wananchi wanaohitaji huduma, wale hapana, haiwezekani tena, hela zinaenda katika mifuko yao,” alisema.

Lukuvi alisema kuanzia jana watu hao wasahau kuendelea kuwa katika nafasi hizo za utumishi walizokuwa nazo.

KILWA

Pia alisema wilayani Kilwa yupo ofisa ardhi aliyemtaja kwa jina moja la Sultani, ambaye amemdhulumu Sh milioni 33 Joseph Kahama, mtoto wa Sir Geogre Kahama.

“Nina ujumbe wako ambao ulimtumia asishtaki kwangu, sasa taarifa ninazo. Pia nafahamu unataka kumtapeli Mmarekani Sh milioni 13. Na huyu naye asimamishwe kazi na uchunguzi dhidi yake ufanyike,” alibainisha.

KANZI DATA YA MATAPELI

Katika hatua nyingine, Lukuvi ametangaza kuanzisha kanzi data ya matapeli wa ardhi, hivyo kuwataka wananchi kumtumia majina yao pamoja na eneo walilotapeliwa, ambayo yatachapishwa katika tovuti ya wizara.

Lukuvi pia alipiga marufuku kwa watendaji wa ardhi nchini kujihusisha na udalali au mtandao wa madalali wa ardhi.

“Vitendo hivi vipo Dodoma na Arusha. Wapo watu kila siku utawaona kwenye ofisi za ardhi, unajiuliza hivi shida zao haziishi? Sasa hawa wanafahamiana na watumishi, sitowavumilia,” alisema.

WATUMISHI WALARUSHWA KUONDOLEWA

Aidha, alisema watumishi wenye kujihusisha na vitendo vya rushwa, hawatopewa nafasi za utumishi wa umma, huku akitaka wale watakaopewa nafasi hizo, majina yao yahakikiwe kisha kupelekewa.

Lukuvi alipiga marufuku watumishi wa Idara ya Ardhi kufanya kazi binafsi za upimaji ardhi wakati wakiwa watumishi wa Serikali na kusababisha mgongano wa masilahi.

“Kama unataka kufanya kazi zako binafsi, mweleze katibu mkuu kwamba kazi imekushinda. Sisi tutawasiliana na utumishi watupe mwingine tuzibe pengo,” alibainisha.

Pia alipiga marufuku watumishi hao kuwatoza wananchi fedha wanazodai kuwa za huduma, akisisitiza malipo ya kodi, tozo na ada yalipwe kwa utaratibu uliowekwa serikalini.

HATI SASA MIKOANI

Kadhalika, Lukuvi ambaye pia ni mbunge wa Isimani, alitangaza mabadiliko ya utendaji kazi yenye lengo la kurahisisha huduma kwa wananchi pamoja na kuondoa urasimu.

Aliyataja mabadiliko hayo ni kuanzia Agosti mosi kila mkoa utakuwa na ofisi ya ardhi badala ya zile za kanda.

Pia hatimiliki za ardhi zitatolewa na kusajiliwa ofisi za mikoa badala ya wananchi kupata huduma hiyo katika ofisi za kanda.

Aidha, hati na nyaraka zote za wanaotaka kukopa, zitapelekwa mkoa ambao muhusika anakopea badala ya ofisi za kanda.

Vilevile, ramani, michoro ya mipango miji, vijiji iliyokuwa ikipelekwa ofisi za kanda, zitapelekwa ofisi za mikoa pamoja na mabadiliko yote ya mipango miji.

Alisema taarifa za uthamini ardhi zilizokuwa zikitolewa na Mthamini Mkuu, zitatolewa kila mkoa badala ya Dodoma.

Pia alisema kila mkoa utakuwa na vifaa vya kisasa vya kupimia ramani bila kukodishwa na vifaa vya upimaji vilivyopo katika kanda visambazwe mikoa husika.

Alisema sasa ni wakati kwa watendaji hao kubadilika kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

HATI ZA KIELEKTRONIKI

Aidha, Lukuvi alisema mwakani Serikali itaanza kutoa hati za kilektroniki ambazo kwa sasa wanafanya hivyo maeneo ya Ubungo na Temeke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles