Na VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
SERIKALI imewapa miezi mitatu watu wanaomiliki maeneo zaidi ya 600 nchini ambayo hawajayaendeleza kwa namna yoyote na kuwataka wayaendeleze kabla hawajanyang’anywa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao cha wataalamu wa upimaji na upangaji ardhi wa sekta binafsi.
“Najua wapo watu wanamiliki hati 1,000 wengine 10,000 wamefungua masijala majumbani mwao wakati Serikali peke yake ndiyo inayopaswa kuwa na masijala ya masuala ya ardhi.
“Wapo wanaotumia ujanja kwa kuandika majina tofauti tofauti na tunawajua,” alisema Lukuvi na kuongeza.
“Siku moja alikuja mtu mmoja hapa wizarani akachukua hati 700 kwa jina lake, jambo hili halikubaliki hata kidogo.
“Kuna watu wanamiliki maeneo mengi makubwa ambayo hawayaendelezi na wakati huo huo wapo wengine wanayahitaji.
“Kitendo cha baadhi ya watu kumiliki maeneo makubwa na kuyaacha bila kuyaendeleza kimesababisha viwanja navyo kupanda bei, yaani hata miji imeharibika kama kule Kisarawe na Mkuranga ambako hakuna mwenye hati hata mmoja.
“Wasomi mpo na mvi zenu, lakini maeneo hayajapimwa, mnafanya nini, kwanini msiende kule kusaidia wananchi?
“Kwa hiyo, huo muda wa miezi mitatu tuliotoa kwa wanaomiliki maeneo makubwa ukiisha, tutayachukua, tutayapima na kuwagawia wananchi wenye shida kwa sababu Serikali imekusudia kuongeza idadi ya wananchi waliorasimishwa ardhi kutoka 170,000 hadi 400,000 ndani ya mwaka huu,” alisema.
Pamoja na hayo, Waziri Lukuvi alisema kazi hiyo ni ngumu kwa kuwa Serikali haina wataalamu wa kutosha ndiyo maana imeamua kuzishirikisha sekta binafsi.
“Tunawaamini kwa sababu baadhi ya kazi mmezifanya, tumeona mmefanya vema kuliko hata yale maeneo ambayo yalipimwa na maofisa wetu,” alisema Lukuvi.
Katika utekelezaji wa kasi hiyo, Waziri Lukuvi alisema tayari ameshazungumza na wakuu wa mikoa ili watangaze tenda kwa maeneo yaliyo tayari kwa ajili hiyo.
Alisema wizara yake tayari imeandaa mwongozo wa namna kazi hiyo itakavyofanyika bila kuwaumiza wananchi hasa wale wa hali ya chini.
“Kama nilivyosema awali, watu walikuwa wanafanya biashara hii kama ujambazi, wanapima maeneo na kuyauza kwa bei ghali na ndiyo maana wengine hawajafanikiwa kuyauza,” alisema.
Alisema mwongozo huo umeandaliwa ili biashara hiyo ifanyike kwa kuzingatia ubinadamu.
Katika mkutano huo, Waziri Lukuvi aliwakabidhi pia fomu wananchi 446 waliowahi kunyang’anywa maeneo jijini Dar es Salaam na maofisa ardhi wasiokuwa waaminifu.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, wananchi hao watagawiwa viwanja katika eneo la Kibada lililoko Kigamboni japokuwa watalazimika kulipia nusu ya gharama.
“Nataka kabla sijahamia Dodoma, niwaache wakazi wa mji huu wakiwa na kicheko kwa sababu utaratibu huu ni endelevu na kila mwenye vithibitisho vya kuporwa eneo, aje navyo wizarani na wale wa mikoani, waende kwenye ofisi za halmashauri watasikilizwa,” alisema.