25.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Lukuvi amng’oa ofisa ardhi Rufiji

Na NORA DAMIAN-RUFIJI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amemsimamisha kazi Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Rufiji, John Hangi kutokana na utovu wa nidhamu.

Hatua hiyo inafuatia baada ya Lukuvi kufanya ziara jana katika baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo lakini ofisa huyo hakuwepo huku waziri huyo akidai amekuwa akimkwepa mara kwa mara.

Akizungumza kwa nyakati tofauti jana katika Wilaya za Rufiji na Kibiti, aliwataka watendaji wa ardhi kufanya kazi kwa weledi ku- tatua kero za wananchi.

“Hangi asikanyage ofisi ya Rufiji, hii ni mara ya tatu ananikwepa, nitashangaa sana kanali (Mkuu wa Wilaya ya Rufiji) kama huyu mtu asiyekuwa na adabu anakaa ofisini.

“Na kama kuna mtu mwingine ambaye anampenda sana ampeleke huko anakotaka,” alisema Lukuvi.

Mkuu wa Wilaya hiyo Luteni Kanali Patrick Sawala, alimu- hakikishia Waziri Lukuvi kuwa atatekeleza maagizo hayo.

“Hangi kuanzia sasa hivi asikanyage ofisini, kama kuna mtu wake amfikishie salamu, nikimkuta huko lake langu, hayo ni maelekezo,” alisema Luteni Kanali Sawala.

MGOGORO WA NGULAKULA, MIWAGA

Akiwa katika Kijiji cha Ngulakula, Lukuvi aliagiza ekari 23,000 ambazo mwekezaji hajaziendeleza zirudishwe kwa wananchi.

Kumbukumbu zinaonyesha mwekezaji alimilikishwa na kijiji hicho ekari 29,168 na kati ya hizo zilizoendelezwa ni 6,000 tu.

Waziri huyo pia aliagiza kufanyika kwa uchunguzi na iwapo wananchi hao hawakulipwa fidia kwa wakati waongezewe malipo kwa asilimia saba.

“Watu wote waliochukua ardhi halafu hawaiendelezi irudi mikononi mwa wananchi. Shughulikeni na ekari alizolipia fidia na zile ambazo hazijafidiwa kuanzia sasa ziko chini ya serikali ya kijiji.

“Unawekezaje ekari zote hata kodi ulipi, kwani ulizaliwa nayo, si umeikututa tulikutunzia sasa lazima ulipe kodi ya ardhi, usifikiri kulipa fidia peke yake ndiyo unahalalisha kukaa na ardhi…sitaki kumpa maumivu mara mbili lakini leo ningeweza hata kunyang’anya hizo 6,000,” alisema Lukuvi.

Awali mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho, Abdallah Kirungi, alisema kabla ya kumpatia mwekezaji ardhi hiyo walimweleza changamoto lakini kilichotekelezwa ni ujenzi wa nyumba ya mwal- imu na ununuzi wa trekta.

“Visima vimechimbwa hakuna maji na msikiti haujajengwa,” alisema Kirungi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, alisema hadi kufikia mwaka 2017 mwekezaji alikuwa amelipa fidia ya Sh milioni 515.8 na kati ya hizo Sh milioni 354 ni kwa Kijiji cha Ngulakula na Sh milioni 161 Kijiji cha Miwaga huku wakiendelea kudai Sh bilioni 1.9.

Naye Mwekezaji Shiraz Jaffary wa Kampuni ya Carbon Planning, alijitetea kuwa changamoto za miundombinu ya barabara na maji ndizo zimechangia kushindwa kuendeleza eneo lote.

MGOGORO WA MCHUKWI B, MKUPUKA

Akiwa katika Vijiji vya Mkupuka na Mchukwi B vyenye changamoto ya mipaka, alisema ataunda timu maalumu kutoka wizarani kuhakiki mipaka na kuchunguza fidia zilizolipwa kwa wananchi.

Pia alimuagiza mwekezaji kusimamisha shughuli zake hadi uchunguzi huo utakapokamilika.

“Kuna changamoto ya mpaka kati ya Mchukwi B na Mkupuka kwa sababu maeneo yanayotakiwa kuendelezwa Mchukwi B wananchi wa Mkupuka wanaamini ni yao,” alisema Lukuvi.

Mwakilishi wa Mwekezaji Daud Brothers & Family, Ibrahim Manzool, alisema waliomba ekari zaidi ya 1,531 katika Kijiji cha Mkupuka na hadi sasa wameshalipa fidia ya Sh milioni 143.

Hata hivyo alisema walipoanza kusafisha ekari 500 waliambiwa baadhi ya maeneo ni ya Mchukwi B hatua iliyosababisha kuwapo kwa mgogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,649FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles