LUKUVI AITWA KUSULUHISHA MGOGORO WA ARDHI KIGOMA

0
698

Na EDITHA KARLO


WAKAZI wa Mtaa Mgeo, Kata ya Buhanda, Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuingilia mgogoro wao wa ardhi na Taasisi ya Kiislamu ya Baraza Kuu (BAKUU) ambayo wameilalamikia kuwapora ardhi yao.

Kwa mujibu wa wananchi hao, wameshangazwa na eneo hilo ambalo wamekuwa wakilitumia muda mrefu kwa shughuli mbalimbali, kutolewa kwa taasisi hiyo na watendaji wa Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Tatu Ibrahim, mkazi wa eneo hilo, alisema maeneo hayo wamekuwa wakiyatumia kwa muda mrefu, lakini wameshangazwa kuona watu wamepima maeneo hayo na kuambiwa yamegawiwa kwa taasisi hiyo ya dini na wananchi hao kutotakiwa kuingia kufanya shughuli yoyote katika eneo hilo.

Alisema hata walipofungua kesi katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigoma na baadaye kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, shauri hilo limekuwa likitolewa hukumu pande moja bila walalamikaji kufika wakati wa usikilizaji wa shauri hilo.

Azizi Keketwa, Mwenyekiti wa Mtaa Mgeo, naye ameshangazwa na watendaji wa Idara ya Ardhi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kugawa eneo hilo kwa watu wengine wakati tayari Serikali ya Mtaa ilishayapima maeneo hayo na wananchi wa eneo hilo kugawiwa kwa shughuli mbalimbali.

Alisema anakusudia kuongoza kamati ndogo ya wananchi hao kumwona Waziri Lukuvi kwa sababu wamejaribu kufuatilia Idara ya Ardhi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji bila msaada wowote.

  Mjumbe wa kamati ya usimamizi ya eneo hilo aliyepo taasisi hiyo, Lumu Mwitu, alisema wao walianza kumiliki eneo hilo tangu mwaka 1998 wakiwa na nia ya kujenga shule ya sekondari ya Kiislamu na kushangazwa na wanaolilalamikia.

Alisema baada ya kuuziwa eneo hilo na mwaka 2000 kupatiwa hati ya umiliki ya miaka 33, walianza kutengeneza ramani ya mradi wa shule baada ya kupata wafadhili.

Mwitu alisema wakati mchakato wa matayarisho ya ujenzi ukiendelea, ndipo walipotokea wananchi wakidai taasisi imevamia eneo lao na kwenda mahakamani, ambako taasisi hiyo imeshinda na kupewa haki ya kumiliki eneo hilo.

  Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Judathadeus Mboya, alisema taarifa alizopewa na wasaidizi wake zinabainisha kwamba eneo hilo linamilikiwa kwa halali na taasisi hiyo ya Kiislamu na kukiri kuwapo taarifa ya mgogoro kwa wananchi kulalamika kuporwa eneo lao.

  Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava, alisema     tume iliyoundwa ya madiwani kushughulikia migogoro ya ardhi ya manispaa hiyo, pia ilipata malalamiko ya mgogoro katika eneo hilo, lakini bado hajapokea ripoti ya tume iliyoundwa kuhusu mgogoro wa eneo hilo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here