30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola, Zungu wasaka ‘mateja’ mitaani

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya operesheni ya kuwasaka na kuwakamata mateja mbalimbali ambao wanatumia dawa za kulenya na kufanya uhalifu katika bonde la Jangwani, Ilala, Dar es Salaam.

Lugola aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu, juzi kwa lengo la kuwasaka mateja hao ambao wanatumia aina mbalimbali ya dawa za kulenya.

Hata hivyo, mateja hao baada ya kuona viongozi hao wanawasaka, walikimbia maeneo ya vijiwe vyao.

Lugola wakati akiwa katika operesheni hiyo aliyoifanya kwa saa moja na nusu, akitembelea mitaa mbalimbali ya bonde hilo, alimpigia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala-RPC, ACP Zuberi Chembera, kufika na askari eneo hilo kuiendeleza.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Jangwani, Lugola alisema wahalifu hawa wanapaswa kusakwa kwa nguvu zote na kukamatwa, kwa sababu walishampora mtu katika mitaa hiyo na kumua.

“RPC kuanzia muda huu, nakuagiza askari wako waingie mitaani kuwakamata wahalifu hawa, na nitakuja kuona wahalifu wote katika bonde hili wamejaa katika kituo cha Msimbazi, na muwakamate wahalifu na sio kuwaonea watu wasiokuwa na makossa,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa Serikali haiwezi kukaa kimya kufumbia macho matukio ya kiuhalifu ambayo yamekithiri eneo hilo na kuwafanya wananchi kutopata usingizi kuhofia kuvamiwa muda wowote – usiku au mchana.

Kwa upande wake, Mbunge Zungu, ambaye ndiye aliyemwalika Lugola kutembelea eneo hilo kuona kero kubwa wanazopata wananchi wake, alisema wahalifu hao hawatoki katika jimbo lake pekee, bali wengi wao wanatoka maeneo mbalimbali Dar es Salaam.

“Wenyeji wa eneo hili ni wachache, wengi wanatoka mitaa mbalimbali ya hapa Dar es Salaam, ikiwemo Temeke na kwingineko, hivyo Mheshimiwa Waziri tunajua utendaji wako, tunakuomba hii kero inatuumiza sana, wananchi wanakosa amani kutokana na uwepo mkubwa wa wahalifu hawa,” alisema Zungu.    

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles