23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola: Mauaji watoto Njombe yanahusika na imani za kishirikina

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema vyombo vya usalama vimeshawabaini watu wanaodaiwa kutekeleza mauaji ya kikatili ya watoto 10 katika Wilaya ya Njombe na kwamba taarifa za awali zinaonesha matukio hayo ni ya kishirikina.

Lugola alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mufindi Kusini, Menrad Kigola  (CCM), aliyetaka kupata kauli rasmi ya Serikali kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa baada ya kuibuka taharuki kutokana na mauaji hayo yanayoendelea.

Akijibu swali hilo, Lugola alisema tayari wameishabaini waliohusika na mauaji hayo.

“Tayari tumeshawabaini watu wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji hayo kutokana na imani za kishirikina na naibu waziri wangu (Hamad Yusufu Masauni) yuko huko akiendelea kuchukua hatua,” alisema.

Lugola alisema mambo yatakuwa sawa na hawatacheza na watu wanaoichokoza Serikali ya Rais Dk. John Magufuli ambao amewatumia salamu.

Alisema tangu juzi naibu wake Masauni yupo mkoani Njombe ambako anafanya vikao vya ndani na kamati za ulinzi ili kutafuta chanzo.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantumu Dau Haji (CCM) alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwapatia askari polisi stahili zao kutokana na baadhi yao kupandishwa vyeo lakini hawapati stahili zao kama inavyotakiwa.

Akijibu, Lugola alisema Jeshi la Polisi kama ilivyo wizara na idara nyingine za Serikali lilihusika na uhakiki wa watumishi, ambao ulisitisha marekebisho yoyote kwenye daftari la mishahara, ajira mpya na upandishwaji vyeo kwa watumishi.

“Baada ya zoezi hilo kukamilika, tayari maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali zaidi ya 8,440 waliokuwa na madai mbalimbali yakiwemo stahili za kupandishwa vyeo wamerekebishiwa mishahara na stahili zao.

“Pia maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wapatao 2,143 kati ya 3,089 waliopandishwa vyeo mwezi Juni, Septemba na Desemba 2018 wamerekebishiwa mishahara yao, hata hivyo taratibu za kukamilisha kuwarekebishia askari waliobakia zinaendelea,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles