25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola aonya maofisa uhamiaji wanaopiga wageni PI

Na Safina Sarwatt -Moshi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewapiga marufuku makamishna uhamiaji na maofisa wa idara hiyo, kucha tabia ya kutoa tangazo la kuondolewa mtu asiye raia nchini (P. I notes) lenye utata kwa masilahi binafsi bila kuzingatia athari ambazo nchi itapata.

Aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa maofisa uhamiaji waandamizi kutoka Tanzania bara na visiwani uliofanyika Chuo cha Uhamiaji mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Yapo malalamiko kwamba kuna wageni wanaingia nchini na kuwekeza kwa ubia na Watanzania, biashara inapokuwa inaendelea Watanzania huwazunguka wageni na kuwatengenezea mazingira ya kuwafukuza ili wapate fursa ya kumiliki hizo biashara na hapo ndipo Idara ya Uhamiaji hutumika, acheni hayo mambo kwa kuwa yanatuchafua kama taifa,” alisema Lugola.

Alisema Rais Dk. John Magufuli anatafuta wawekezaji kwa nguvu na kuwahakikishia usalama wao na biashara zao, lakini baadhi ya watumishi wa umma badala ya kusaidia jitihada hizi, wao wanatumika kuwafukuza kwa dhuluma.

Lugola alisema wageni hao wakishafukuzwa, wanaacha uwekezaji wao nchini ambao wanadhulumiwa na huko waliko wanaisema nchi vibaya na kwa uzoefu huo, wageni wengine hawawezi kuja nchini.

“Badala maofisa hao kusimamia na kuimarisha hali nzuri ya wawekezaji kutoka nje, lakini wamegeuka kuwa kikwazo na kuwafukuza wageni bila kufuata taratibu. Narudia tena, mjitathmini, fanyeni kazi, simamieni haki, zingatieni sheria za nchi na taratibu.

“Amani na usalama wa nchi vinategemea sana Jeshi la Uhamiaji, hivyo hakikisheni mnalinda amani bila kutanguliza masilahi binafsi kwa kuwahudumia wageni na wananchi kwa ukarimu, kwa lugha inayostahili.

“Msiruhusu masilahi binafsi yakazidi masilahi ya taifa letu, daima simamieni jambo hili na kwa wasaidizi wenu wa ngazi za chini kwani mkishindwa ipo gharama yake na uhamihaji ni uso wa taifa hili,” alisema Lugola.

Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inavutia uwekezaji na utalii ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda, hivyo wahakikishe kwamba wanaboresha mazingira ya usalama wa wageni.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, aliwataka maofisa wa uhamiaji kufanya kazi kwa uadilifu na uweledi kwa masilahi ya nchi kutokana na uwepo wa baadhi yao wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na wengine kusaidia wageni ambao wanaishi nchini kinyume na taratibu.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, alisema katika kikao hicho zitatolewa mada mbalimbali zitakazowasilishwa kuhusu rushwa na kanuni za uendeshaji za uhamiaji za mwaka 2018ambazondio mwongozo wa utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji.

 “Kwa kuwa Idara yetu ya Uhamiaji inatoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo pasipoti, vibali vya ukazi, pasi pamoja na viza, hivyo kupitia kikao hiki tutazingatia kikamilifu mada hizo kwa kuwa zitatusaidia katika kutoa huduma bora kwa masilahi ya idara yetu, Wizara na taifa kwa ujumla,” alisema Dk. Makakala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles