Na MWANDISHI WETU-MTWARA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amemuweka ndani Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kati mjini Mtwara (OCS), Ibrahim Mhando, kwa kushindwa kuwaweka mahabusu watuhumiwa wanne.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Y&P Architects, Benjamin Kasiga ambaye alitoa taarifa za uongo kwa Waziri huyo kuhusu ujenzi wa Makao Makuu ya Uhamiaji mkoani humo.
Lugola alichukua uamuzi huo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo hicho, wakati anakwenda Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kurudi Dar es Salaam.
Waziri alikwenda katika kituo hicho kuthibitisha kama maelekezo yake ya mtuhumiwa akamatwe na kuwekwa mahabusu yalifuatwa, lakini alimkuta mtuhumiwa huyo akiwa chumba cha upelelezi badala ya kuwekwa mahabusu ya polisi.
Kwa sababu hiyo, Lugola alimhoji Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Lucas Mkondya ni kwa nini agizo lake lilikuwa halijatekelezwa.
“Hivi ndivyo polisi mnafanya, haya ndiyo madudu mnayoyafanya? Tabia hii siku zote tunaipinga inachafua Jeshi la Polisi na hii ndiyo tabia yenu….najua ndiyo maana nimekuja ghafla.
“Mnafahamu maadili ya Jeshi? RPC hawa polisi wako wanafanya nini, OCS njoo hapa… kwa nini umeweka hawa watuhumiwa chumba cha upepelezi badala ya mahabusu?
“Sasa na wewe unaingia ndani kwa kushindwa kuwaweka ndani hawa watuhumiwa, RPC muweke ndani sasa hivi huyu,”aliamuru Lugola.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo (RPC), Mkondya alimweleza Waziri Lugola kuwa polisi wake walifanya makosa kwa kutowaweka mahabusu watuhumiwa hao.
OCS Mhando kabla ya kuwekwa mahabusu, alisema sababu ya kutowaweka mahabusu watuhumiwa hao ilitokana na mahabusu kujaa.
Hata hivyo, Lugola alipinga kauli ya Mhando kuhusu mahabusu hiyo kujaa wakati nafasi ya kukaa watuhumiwa hao ilikuwapo ndani ya mahabusu hiyo.
“Mbona nafasi ipo pale mahabusu, ile pale nafasi naiona. Siwezi kukubaliana na uzembe huu na hii ni tabia yenu huwa mnakamata watuhumiwa lakini baadhi hamuwaweki mahabusu, unanidanganya kuwa mahabusu imejaa, hii haikubaliki,”alisema Lugola.
Lugola ambaye alikuwa katika ziara ya dharura katika mikoa wa Mtwara na Lindi, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kugundua majengo ya uhamiaji mikoa hiyo pamoja na Gereza la Ruangwa kuwa yamejengwa chini ya kiwango.
Akiwa wilayani Ruangwa, Lugola aliwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya wizara yake kuwaondoa mara moja wananchi wote waliovamia maeneo ya majeshi nchini.
Aliyasema hayo baada ya kulikagua gereza jipya la Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambalo lina ekari 100 huku ekari 20 zikiwa zimevamiwa kwa kujengwa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, ufuta na korosho katika eneo la Jeshi la Magereza.
Akizungumza baada ya kulikagua gereza hilo, alisema kuanzia sasa viongozi wa vyombo vyake wahakikishe hawaruhusu mwananchi yeyote kuingia katika maeneo ya jeshi na atakuwa mkali kulifuatilia suala hilo.
Lugola ambaye pia alikataa kuipokea taarifa ya ujenzi wa gereza hilo ambayo ilikuwa inasomwa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Lindi, Rajabu Nyange, alisema taarifa hiyo ina upungufu mkubwa na asingeweza kuipokea licha ya kuelezwa kuhusu ardhi ya jeshi hilo kuvamiwa.
“Mimi huwa nashangaa inakuwaje wananchi wanavamia ardhi ya jeshi tena bila woga halafu jeshi linakaa kimya linabaki kunung’unika.
“Hii haijakaa sawa kabisa na kamwe sikubaliani nalo,”alisema Lugola.