24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola amng’oa RTO Arusha kwa ukaidi

Mwandishi Wetu -Malinyi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amemwondoa madarakani Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO), Charles Bukombe kwa kosa la kupuuza maagizo yake na kuyaita ya kisiasa.

Licha ya kumwondoa katika nafasi hiyo, Lugola amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara yake, kumchukulia hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa maofisa wengine wa trafiki mikoa mingine.

Alisema ameshuhudia video ambayo ilikuwa inasambaa mitandaoni, Bukombe akipinga maagizo yake na kuyaita ya kisiasa na pia kugoma kuyatekeleza akiwa katika mkutano jijini Arusha.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa mji wa Malinyi mkoani Morogoro jana, Lugola alisema yeye hatoi maagizo ya kisiasa, bali yatakayomsaidia rais kazi zake kwa wananchi wanyonge wanaopambana na umasikini na ajira.

“Namwagiza katibu mkuu achukue hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kumwondoa u-RTO afanye shughuli zingine za kipolisi na wengine ambao mkono wangu haujafika kwenu, nimeanza kuwaona hamsimamii vizuri maagizo yangu.

“Wapo  ambao wanaendelea na uonevu, wapo baadhi ya askari wanaendelea kuchukua rushwa barabarani,” alisema Lugola.

Pia Lugola alitoa onyo kali kwa wakuu wa trafiki wa mikoa ya Morogoro na Mara na kuwataka wachukue fursa ya kujitathmini katika utendaji wao kabla hajawachukulia hatua.

“Wapo baadhi ya askari waonevu, wanaendelea kuchukua rushwa, wajitathmini katika utendaji wao kabla sijawachukulia hatua kali za kinidhamu,” alisema.

Lugola ambaye alihutubia mikutano mingi kwa nyakati tofauti jana, alisema Serikali ni sikivu na haitaki kumnyanyasa mwananchi yeyote kupitia makosa ya trafiki wasiokuwa waaminifu.

Kutokana na hali hiyo, alitoa maagizo kwa Jeshi la Polisi nchini, kwamba bodaboda zinazotakiwa kuwapo kituo cha polisi ni zile zilizopo katika makundi matatu; zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika katika ajali.

“Bodaboda hizo ndizo zinapaswa kuwapo vituoni, lakini kuziweka ambazo hazipo katika makundi hayo, napiga marufuku, nataka polisi nchi nzima mnielewe,” alisema Lugola.

Aliwataka waendesha bodaboda mjini Malinyi na Tanzania kwa ujumla, wafuate sheria za usalama barabarani ikiwamo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.

Pia alipiga marufuku tabia ya baadhi ya askari kukamata pikipiki wakiwa hawana sare za jeshi, akisema kufanya hivyo kunaleta kero kwa madereva na pia anayekamatwa anaweza akadhaniwa kuwa ni jambazi.

Lugola anaendelea na ziara yake mkoani Morogoro na anatarajia kumaliza ziara hiyo Wilaya ya Ulanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles