22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

LUGHA ZA KUUDHI ZINAWEZA KUKUTENGA NA MARAFIKI

Na CHRISTIAN BWAYA


AISHA anapenda kuongea na watu. Kila anapokuwa na watu, Aisha hupenda kujielezea maisha yake binafsi na kuonesha namna alivyopiga hatua kubwa za kimaendeleo. Lakini anapozungumzia watu wengine, Aisha hutumia lugha ya kejeli yenye kuwalaumu na kuwakosoa watu kwa yale wanayoyafanya au kumfanyia. Hata inapotokea anapozungumzia matukio ya kawaida, Aisha huona mabaya tu yanayofanya aishie kulalamika, kukosoa, kubeza, na kuonesha namna ambavyo mambo hayaendi.

Tabia hii, hata hivyo, wakati mwingine imemwingiza matatani. Imemfanya akosane na watu wake wa karibu ambao angetamani waendelee kuwa rafiki zake. Juzi alipokuwa akizungumza na Monica, rafiki yake anayefanya kazi isiyo na mshahara mkubwa kama wa kwake, Aisha alijikuta akisema maneno ya kuudhi:

“Nashangaa kuna watu wanafanya kazi miaka mitano lakini bado hawawezi kumaliza mwezi bila kukopa,” alimwambia Monica, aliyekuwa amekwenda kumkopa fedha kidogo zimsaidie kumaliza tatizo alilokuwa nalo.

Kusikia hivyo Monica alinyong’onyea. Lugha hiyo ilimfanya ajione kadhalilika. Uso wake ulipoteza furaha. Aliamua kunyanyuka na kuondoka. Aisha, kwa kugundua alikuwa amemkosea rafiki yake, alimwomba msamaha  kwa maneno hayo aliyoyaita ni utani. ‘Sikukusudia shoga yangu. Hutaniwi? Ule ulikuwa utani mwaya!’ alimwambia huku akicheka.

Monica, hata hivyo, aliamini Aisha alimaanisha kile alichokisema. Kwa kurejea tabia yake ya kuwabeza watu mara kwa mara, ilikuwa ni vigumu kwake kufikiri Aisha hakulenga kumdhalilisha kihisia. Uhusiano wake na Aisha ulianza kuingia doa.

Kuna wakati unaweza kujikuta unakuwa mtu mwepesi kukosoa, kubeza, kuwakejeli wengine. Unafanya hivyo bila kughamua kile unachokifanya. Wakati mwingine inakuwa kama unafurahia hicho unachokifanya. Ukiwa kwenye mitandao ya kijamii, kwenye mazungumzo na watu, unasema maneno magumu yanayowafanya watu wajisikie vibaya.

Aidha, unaposikia jambo fulani limefanywa, akili yako inaona makosa kwa haraka. Unajigeuza kuwa mchambuzi asiyerasmi kuonyesha mapungufu ya kile kilichofanywa. Wanaokusikiliza wanaweza kukubaliana na wewe kwa sababu hicho unachokisema kinaweza kuwa na ukweli ndani yake.

Hata hivyo, pale unapoongea mambo yanayokuhusu wewe mwenyewe, hali inakuwa tofauti. Ufahamu wako unafunga mlango wa kuona upungufu, kisha mlango wa kuona mema unafunguka. Unafanya hivyo bila kufikiria. Unaweza kutumia muda mwingi kuelezea namna ulivyo mtu wa pekee, namna unavyojitahidi kuwasaidia watu, hata kama wakati mwingine si kweli. Umewahi kujiuliza kwa nini inakuwa hivi?

Ukweli ni kwamba tabia hii ni kiashiria cha ugonjwa wa nafsi. Mtu mwenye tatizo la nafsi hana tofauti na Aisha ambaye ndani yake kuna njaa ya kuwazidi wengine. Kukuza mabaya ya watu ambayo wakati mwingine hawanayo kunamwaminisha kwamba yeye ni mtu bora. Anapowafanya wengine wakate tamaa, wajisikie vibaya kama alivyofanya kwa Monica, Aisha anajisikia kusahau maumivu aliyonayo ndani yake.

Pamoja na faida ya muda mfupi anayojisikia, Aisha anajikuta akiwachosha watu wanaomzunguka. Fikiria kukaa na mtu ambaye muda wote anajizungumzia yeye na mafanikio yake. Hatoi nafasi kwa mtu mwingine kusema isipokuwa yeye. Fikiria mtu ambaye kila anapoongelea watu ni mtu wa kukosoa na kukejeli. Haoni jema lolote isipokuwa mapungufu. Ni dhahiri huwezi kumvumilia isipokuwa kama na wewe una tabia hiyo. Wahenga walisema, ndege wafananao huruka pamoja.

Unaposikika ukilalamika muda mwingi, unawachosha watu wanaofikiri mambo makubwa. Huwezi kuwa na urafiki wa muda mrefu na watu wanaotafuta majibu ya matatizo kama wewe una tabia ya kulalamika. Huwezi kuendeleza urafiki wa kudumu na watu wenye tabia ya kuwainua wengine, kama umezoea kuwavunja moyo watu wengine. Unawavuta wanaofanana na wewe.

Pamoja na hayo, bado unaweza kubadilika. Badiliko linaanza kwa kushughulika na nafsi yako. Ili abadilike, Aisha anahitaji kujifunza kuingiza maneno chanya moyoni wake. Badala ya kusikia habari zinazovunja moyo, Aisha aanze kuwasikiliza watu wenye kuwainua wengine.

Sambamba na hilo, Aisha anahitaji kuanza kujenga tabia ya kujisemea maneno chanya anapokuwa mwenyewe. Akifanya hivi kwa muda mrefu, chemichemi ya maneno chanya inataanza kububujika ndani yake. Aisha hatakuwa na sababu ya kubeza, kukosea au kujisifia mbele za watu na ataanza kuwavutia watu chanya kwenye maisha yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles