25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

LUGHA CHAFU YA WAUGUZI YAKERA WANANCHI

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA


BAADHI ya watumishi wa vituo vya afya vinavyosimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya wametajwa kutumia lugha za maudhi na kejeli kwa wagonjwa wakati wa kutoa huduma.

Mbali na kauli hizo, pia vituo hivyo vinadaiwa kushindwa kutoa huduma kwa wakati, hali inayosababisha wagonjwa wanaofika kukaa zaidi ya saa nane hadi 10, wakisubiri huduma.

Vituo kama Igawilo kilichopo eneo la Uyole, Kiwanja Mpaka kilichopo eneo la Sokomatola na Mwanjelwa vyote viko ndani ya Jiji la Mbeya.

Gazeti hili lilifanikiwa kutembelea vituo hivyo na  kujionea hali halisi, huku baadhi ya wagonjwa wakitoa ya moyoni kwa sharti la kutotajwa majina yao.

Wakizungumza kwa uchungu na majonzi, wakazi hao waliutupia lawama uongozi wa halmashauri kwa kushindwa kuvisimamia vituo hivyo, ambavyo baadhi ya watendaji wamekuwa wakifanya kazi wanavyojisikia wao na kusahau wajibu wao kwa wagonjwa.

“Tangu saa mbili asubuhi hadi saa tisa alasiri sijapata huduma, msongamano wa wagonjwa ni mkubwa, wamekuwa wakiendelea na shughuli zao za kupiga stori, kuzungumza na simu na kukaa nje wakiota jua na kusahau wajibu wao kwa wagonjwa,” kilisema chanzo kimoja cha habari hii.

“Wahudumu wa afya wamekuwa wakitumia lugha za maudhi na zinazokera kwa wagonjwa pale wanapofuatwa na kuelezwa shida zao.

“Mgonjwa anamfuta nesi na kumweleza hali halisi ya tatizo lake lilivyo kubwa na kuomba kuonana na daktari, cha kushangaza utamsikia akijibu subiri niongee na simu, au utamsikia akisema kwa hiyo mimi Mungu… hivi wewe ni kipofu huoni kwamba daktari anahudumia wagonjwa wengine, kwa kweli haya maneno yanaudhi na kukera,” kilisema chanzo kingine cha habari hii.

Akizungumzia tatizo hilo, Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, Jonas Lulandala, alikiri ofisi  kupokea malalamiko hayo na kwamba yameanza kufanyiwa kazi.

“Malalamiko hayo ni kweli tupu, mimi mwenyewe nimeyafanyia kazi  na kujiridhisha na kuwabaini baadhi yao, sipingani na wananchi, nawaomba waendelee kutoa ushirikiano wao kwa kutoa taarifa za watumishi hao ambao si waadilifu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles