Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakuu wa Wilaya za Ilala na Kisarawe wamemaliza utata wa muda mrefu wa mgogoro wa mpaka katika Mtaa wa Ngobedi B ambao sasa utatambuliwa kuwa upo Wilaya ya Kisarawe.
Hatua hiyo inafuatia baada ya kikao cha pamoja baina ya kamati za ulinzi na usalama za wilaya hizo pamoja na maaofisa ardhi wa wilaya hizo.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Ngobedi B, Wakuu wa Wilaya hizo, Ng’wilabuzu Ludigija (Ilala) na Nickson John (Kisarawe) wamewataka wananchi kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaokwenda kuweka alama za mipaka.
“Tulichofanya ni kutafsiri sheria na ili kurahisisha wataalam watakuja kuweka mipaka na alama zitaonekana,” amesema John maarufu kama Nikk wa Pili.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amesema kwa muda mrefu wananchi walikuwa wanahangaika kutaka kujua wako wilaya ipi.
“Sisi wote bado ni Watanzania mipaka ya Kisarawe na Ilala haiondoi Utanzania wetu, na hii inatusaidia zaidi kwa sababu kumekuwa na shida wananchi wamekuwa wanakuja wanataka wapate ukweli wako wapi,” amesema Ludigija.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wamesema hawajaridhika na uamuzi huo kwa kile walichodai kuwa Ngobedi B iko Ilala.
“Mpaka sasa tumebaki njia panda kwa sababu kama Ngobedi ni ya Kisarawe kwanini Ngobedi A iko Ilala?” amehoji mmoja wa wakazi hao Flora Kamata.
Wakuu hao wa wilaya pia wameahidi kuendelea kushirikiana ili kutatua changamoto zinazokabili eneo hilo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaokwenda kuweka mipaka.