28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Sina mpango wa kushindwa

lowassaNA WAANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akisema hana mpango wa kushindwa.
Lowassa aliwasili katika Makao Makuu ya CCM mjini hapa jana saa 10:20 jioni akiambatana na mkewe, Regina huku akisindikizwa na wabunge mbalimbali pamoja na wanachama wa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wanachama waliokuwapo katika Ukumbi wa Makao Makuu ya CCM mara baada ya kuchukua fomu, Lowassa alisema hawezi kuzungumzia upande wa kushindwa katika safari yake.
“Swali rahisi sana, sina mpango wa kushindwa,” alisema Lowassa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kama atashindwa katika kinyang’anyoro hicho.
Alipoulizwa kuhusu hali ya nchi kuwa na watu wanaoshambuliwa, Lowassa alisema atajenga Serikali itakayojali utu na uhuru wa vyombo vya habari.
“Kwanza nimpe pole yule mwandishi wa MTANZANIA aliyeteswa. Sikubaliani na mambo ya kuingilia uhuru wa watu kuteswa. Serikali yangu itaheshimu uhuru wa vyombo vya habari,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wanachama wa CCM waliokuwa wamefurika ndani na nje ya ukumbi huo.
Alipoulizwa kwanini anahusishwa na vitendo vya ufisadi, Lowassa aliyekuwa akijibu maswali kwa ufupi, alisema kama kuna mtu ana ushahidi na tuhuma hizo amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme, na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi ila tutawapima kwa matendo yao,” alisema.
Kada huyo wa CCM alivitaka vyombo vya habari kutoshabikia tuhuma zisizo na ushahidi, huku akisisitiza kuwa kila mtu apimwe kwa rekodi yake.
Kuhusu uteuzi wa mawaziri, Lowassa hakutaka kulizungumzia akisema bado hajavuka daraja.
“Nitavuka daraja nitakapolifikia,” alisema.
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa, alisema ni sera ya CCM iliyotekelezwa baada ya kutokea mgogoro kati ya vyama vya CCM na CUF.
“Angalieni kule Marekani, vyama vya Democrat na Republican, vinashindana kwa kura chache sana. Hata sisi tunapishana kwa kura chache, mimi nadhani kama hatupishani sana hivyo hilo ndilo suluhisho,” alisema.
Awali Lowassa aliwashukuru wana CCM waliofurika katika ukumbi huo akisema anajua kero za chama hicho na atakapokuwa rais atazishughulikia.
“Nawashukuru kwa kunileta nyumbani, nimeitumikia CCM kwa muda mrefu. Nilieleza Dodoma na Arusha nia yangu. Naelewa matatizo wanayopata watumishi wa CCM, nayaelewa. Mishahara midogo, hawakopesheki, hawana fedha za likizo na hawana uchumi mzuri. Wakati wengine wanajengewa nyumba na mikopo wenyewe hawapati,” alisema Lowassa.
Hata hivyo, alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa kuimarisha uchumi ndani ya chama hicho, lakini akasema akiwa rais atafanya zaidi.
“Tunaweza kufanya zaidi, tusiwe ombaomba. Nilipokuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini tumejenga jengo la ghorofa 22 Dar es Salaam. Tuna viwanja na maeneo mengi. Nikichaguliwa kuwa rais na mwenyekiti nitaangalia hilo…Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba,” alisema.
Baada ya mkutano huo, Lowassa alikwenda kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Dodoma kupata udhamini wa chama hicho ambapo Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi alikuwa miongoni mwa wanachama waliomdhamini, akiwamo mlemavu wa miguu, Idd Omari.
Baadhi ya vigogo waliokuwa ukumbini ni pamoja na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah.
Akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Dodoma Mjini baada ya kuchukua fomu, Lowassa alisema vigelele na makofi anavyopigiwa sasa haviwezi kumpeleka Ikulu isipokuwa wananchi wanapaswa kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili iwe njia rahisi ya yeye kuwa mkuu wa nchi.
“Naomba watu wajiandikishe, hakikisheni watoto wenu, wajomba na hata washikaji zetu wanajiandikisha katika Daftari la Wapigakura na nitarudi tena kwenu kuomba kura,” alisema.
Huku akishangiliwa na mamia ya wakazi wa Dodoma, Lowassa aliwaambia amekwenda kuomba wadhamini na si kuomba kura, kwani amebanwa na sheria na utaratibu wa chama chao.
Alisema ameguswa na mapokezi waliyompa na kuwashukuru wadhamini wake kwa kumwamini na kusisitiza kuwa atarudi tena kuomba kura.
“Leo siombi kura, naweka akiba ya maneno hata wakihesabu nina kampeni potelea mbali, lakini nilipokuwa waziri mkuu nilianza kuijenga Ikulu mnayoiona mpaka leo haijakamilika, nitakuja kuikamilisha, maana yake nini, nahamia Ikulu Dodoma,” alisema mbunge huyo wa Monduli huku akishangiliwa na mamia ya wananchi hao.

Dk. Bilal atamba kuwaunganisha Watanzania
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amesema iwapo CCM itampa ridhaa ya kupigiwa kura na kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, atawaunganisha Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao.
Dk. Bilal alisema hayo jana mjini hapa katika Makao Makuu ya CCM mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kugombea nafasi ya urais.
Aliwasili katika viwanja vya Makao Mkuu saa 7:05 mchana na kukabidhiwa fomu na Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. Mohammed Seif Khatib.
Dk. Bilal alisema Watanzania wote ni ndugu, hivyo akipewa ridhaa kazi atakayofanya ni kuvunja udini, ukabila, rangi ikiwa ndio njia pekee ya kukuza uchumi na kujenga taifa lililo imara.
Aliwaambia wanahabari na wana CCM waliojitokeza kumsindikiza kwamba nia ya kujitokeza kutaka ridhaa ya chama chake ni kutumia haki yake ya kidemokrasia akiwa kama mwanachama yeyote na Mtanzania mwenye uwezo wa kulisaidia taifa kupiga hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo.
Lakini pia alisema sababu ya pili ilikuwa ni kukipa uimara zaidi chama chao akiamini kwa kufanya hivyo atakuwa amekitendea haki.

VIPAUMBELE
Dk. Bilal alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zinazoendelea kupiga hatua kwa kasi kwenye nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii, hivyo iwapo atapata imani ya CCM na Watanzania ataendeleza pale walipomalizia wenzake bila kupoteza mwelekeo.
“Muungano wetu siyo kama ulivyokuwa zamani, sasa unakabiliwa na changamoto nyingi na kwa hivyo ni jukumu langu kuhakikisha nashirikisha wadau kutatua changamoto na kuimarisha muungano,” alisema Dk. Bilal.
Kipaumbele kingine ni ushirikishwaji wananchi kiuchumi pamoja na kukuza sekta ya viwanda, ujasiriamali, teknolojia, sekta binafsi ambayo ni shirikishi, kilimo, ushirika, ugatuzi wa madaraka kwa wananchi katika ngazi za vijiji na vitongoji.

BALOZI KARUME: NITAUNDA SHERIA ZENYE USAWA
Kada mwingine aliyechukua fomu jana alikuwa ni Balozi Ali Karume ambaye aliwasili katika ukumbi wa Makao Makuu ya CCM ilipotimu saa 8:30 mchana na kwenda moja kwa moja Idara ya Oganaizesheni na kukabidhiwa fomu na Mkuu wa idara hiyo, Dk. Mohammed Seif Khatib.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kazi ya kuchukua fomu, Balozi Karume alisema iwapo atateuliwa na CCM kupeperusha bendera yake katika uchaguzi mkuu ujao, jambo atakalofanya ni kuunda sheria zitakazoleta haki na usawa kwa wananchi.
Aidha, alisema kipaumbele chake ni kujenga uchumi wa kisasa pamoja na huu uliopo kuufanya uwe bora zaidi na kuupeleka nchi nzima ikiwamo vijijini wapate kuutumia.

SIYANTEMI ASEMA ATAKUBALI MATOKEO
Naye Amos Siyantemi ambaye ni mtumishi wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, alisema iwapo atashindwa katika kinyang’anyiro hicho atakubali matokeo.
Alisema atashirikiana na mgombea yeyote atakayepitishwa na chama chake kubeba bendera ya chama katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, Siyantemi aliahidi iwapo atateuliwa atahakikisha Watanzania wanadumisha amani na umoja wa taifa ikiwa ni pamoja kupiga vita viashiria vyote vitakavyotaka kuligawa taifa.

SUMAYE ASEMA YEYE SI MCHAFU
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema yeye si mchafu na kama angekuwa hivyo asingeweza kuishi kwa amani.
“Nilizushiwa mambo mengi wakati ule nilipogombea urais 2005, lakini baadaye aliyenichafua ambaye ni Mchungaji Mtikila alikuja mwenyewe kuniomba msamaha akisema kuwa alipotoshwa na watu ambao wanataka madaraka.
“Mimi ni mtu wa kawaida kabisa, naishi maisha ya kawaida, watoto wangu wanafanya kazi ya kuajiriwa, majirani zangu na watu walionizunguka huwa wananitembelea, wanayajua maisha yangu, sina makuu kabisa, sasa kama ningekuwa mchafu ningeshajulikana siku nyingi,” alisema Sumaye huku akishangiliwa na wana CCM waliokuwapo katika ukumbi huo.
Pamoja na mambo mengine, Sumaye alisema kipaumbele chake cha kwanza endapo atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano ni kuimarisha uchumi wa Watanzania.
Alisema ikiwa uchumi una hali mbaya huku vijana wakiendelea kusoma itakuwa ni bure kwa sababu watajazana mitaani huku kukiwa hakuna ajira.
“Mtambo wa kumaliza kila kitu ni uchumi. Nikipewa ridhaa ya kuongoza taifa hili nitaubadilisha uchumi na nitapunguza pengo la masikini na matajiri ili kusiwe na matabaka,” alisema.

MAGUFULI
Naye Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alichukua fomu ya kuwania urais huku akigoma kuzungumza na waandishi wa habari akisema safari bado ni ndefu, aombewe na Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles