Mwandishi Wetu    Â
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema anaomba asigombanishwe na Rais John Magufuli kwamba ana mpango naye wa kuhamisha wapinzani kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), madai ambayo ameyakanusha.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Mto wa Mbu, mjini Arusha, Lowassa amesema kuna watu wanaongea uzushi huo ambapo amewataka wamuache Rais Magufuli afanye kazi zake vizuri kwani anamheshimu kwa mujibu wa Katiba.
Kauli hiyo ya Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imekuja wakati vuguvugu la kuhama vyama kwa wabunge, madiwani na viongozi wa upinzani, wiki chache baada ya Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema), kujivua uanachama wa chama hicho na siku moja baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli na Diwani wa Monduli Mjini, Isack Joseph, kujiuzulu nafasi hiyo na kujiunga na CCM.
“Nimesimama kujibu hoja ya baadhi ya magazeti kwamba niko mbioni kuwatoa wabunge upinzani kuwapeleka CCM, nina mpango na Rais Magufuli, nasema ni waongo wakubwa, mimi sina mpango wowote na wala sina ugomvi naye, acheni kufitini watu, acheni umbea.
“Sina mpango wowote wa namna hiyo. Maendeleo haya ya Monduli tumeyapata kwa umoja wetu na kufanya mambo
yanayokubalika, lazima tujivunie, tupo mahala pazuri,” amesema Lowassa.
Aidha, Lowassa amewataka watu wanaohama watumie sababu nyingine ila yeye na viongozi wa wenzake wako imara katika safari ya mabadiliko na kuongeza kuwa acha wengine waende tu.
“Ni ndugu zangu hao tumetoka mbali lazima tuwaheshimu, fitina za nini? Hatuna mpango wowote. Waache umbea. Namheshimu kwa mujibu wa katiba,” amesema Lowassa na kuongeza;
“Kuna mashindano ya kuhama vyama nchi nzima. Wanaohama nawatakia heri. Aliyekuwa Mbunge wa Monduli amesema hadharani nimemtanguliza Ikulu, huu ni uongo kwani mimi sina miguu yangu, anadanganya, ni uongo mtupu,” amesema Lowassa.