27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Ole wao

mtz1NA MAREGESI PAUL, KAHAMA

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewaonya viongozi watakaowanyanyasa wamachinga, mama ntilie na waendesha bodaboda baada ya yeye kuingia madarakani.

Amesema pamoja na kwamba Serikali yake itamjali kila Mtanzania, makundi hayo matatu ni marafiki zake na anajua umuhimu wao katika kukuza uchumi wa taifa.

Kutokana na hali hiyo, amesema hatasita kumchukulia hatua kiongozi yeyote wa Serikali atakayeyanyanyasa makundi hayo kwa kuwa ni marafiki zake.

Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitoa onyo hilo mjini Kahama jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa stendi mpya uitwao Mbulu.

“Matumaini ni makubwa sana mwaka huu, naomba Mungu anisaidie kwa sababu nakubaliana na mgombea ubunge wenu, James Lembeli, kwamba Kahama unatakiwa kuwa mkoa.

“Nasikitika pia ile bandari kavu ya Isaka kutofanya kazi, lakini nikifanikiwa kuingia madarakani, nitalifanyia kazi hili.

“Nasikitika vilevile kusikia habari ya maji, kwamba kuna maeneo hapa Kahama hamna maji, nawaahidi nikiingia madarakani, nitalimaliza hili na maji mtapata.

“Lakini, ole wao watakaowanyanyasa mama ntilie, wamachinga na waendesha bodaboda. Watu hawa ni marafiki zangu na nitakapoingia madarakani, nitawaboreshea maisha yao ikiwa ni pamoja na kuwaanzishia benki yao.

“Nawaahidi pia kufuatilia suala la operesheni tokomeza ili walioathiriwa walipwe fidia na jambo hili nililisema pia wakati nikiwa Katavi na Rukwa,” alisema Lowassa.

Aidha Lowassa alisema pamoja na kwamba kuna watu wanadharau uamuzi wake wa kuomba urais, lakini amelazimika kuomba nafasi hiyo kwa sababu amechoshwa na umasikini walionao Watanzania.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania wawe makini siku ya kupiga kura ili wamchague yeye na wagombea wa Ukawa kwa sababu wanachukizwa na umasikini wa Watanzania.

“Nimekuja hapa Kahama kuwaomba kura kwa sababu kura zenu ni muhimu sana kwangu. Hamjui ni kwa kiasi gani mnavyogusa moyo wangu pindi ninapoona maelfu ya watu mnakuja kwenye mikutano yangu kama hivi na mnanishangilia.

“Nawaambieni mnanipa imani nami nawaahidi utumishi uliotukuka, nawaahidi kwa sababu imani huzaa imani.

“Nimegombea urais kwa sababu nimechoshwa na ulegelege wa Serikali, nimegombea urais kwa sababu nataka kuunda Serikali yenye spidi kali ambayo haijawahi kutokea na itakayowajali wakulima, wafugaji, wachimbaji wadogo wadogo na Watanzania wote kwa ujumla.

“Nawaambieni kabisa, kwamba nataka nchi yangu ipae kimaendeleo, biashara ndogondogo zote zitafanywa na wazawa, biashara kubwa kubwa wazawa watakuwa na asilimia 70 na wageni watakuwa na asilimia 30, na nataka pia kila aliyekuwa akila mlo mmoja, ale milo miwili, aliyekuwa na baiskeli moja, awe nazo tano na aliyekuwa na ng’ombe kumi awe na ng’ombe 20.

“Siku hiyo ya Oktoba 25 mwaka huu ni siku muhimu sana kwetu, fikirieni nani wa kupigia kura, fikirieni mara mbilimbili kwa sababu siku hiyo ndiyo siku ya kuwaondoa CCM madarakani,” alisema.

 

JAMES LEMBELI

Naye mgombea ubunge Jimbo la Kahama Mjini, James Lembeli (Chadema), alimwambia Lowassa kwamba atakapoingia madarakani, awasaidie wananchi wa Kahama kufufua bandari kavu ya Isaka na pia awasaidie kuufanya Mji wa Kahama uwe kituo cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Pia alimtaka mgombea urais huyo awasaidie kupata maji ya uhakika katika vijiji visivyokuwa na maji, awasaidie kupata mtambo wa kupoza umeme unaotoka katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi na pia awasaidie kuondoa kero wanazopata wachimbaji wadogo wadogo wilayani Kahama.

Pamoja na hayo, Lembeli alimtaka Lowassa awasaidie kujenga barabara inayotoka Kahama hadi Kakora ili iweze kupitika wakati wote.

 

TAMBWE HIZA

Kwa upande wake, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha proganda cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tambwe Hiza, alisema alilazimika kukihama chama hicho kwa kuwa hakiwajali wananchi.

Kwa mujibu wa Hiza, wananchi vijijini wanaishi maisha ya shida, na kwamba ili kuwakomboa katika hali hiyo, ni lazima Watanzania waamue kuiondoa CCM madarakani kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Pia, alisema Lowassa ndiye mtu sahihi wa kuiondoa CCM madarakani na kwamba Watanzania wasipompa kura za kuingia Ikulu, itakuwa vigumu kuiondoa CCM kwa miaka ijayo.

Awali baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kahama, walimkabidhi Lowassa mkuki kama ishara ya kumtakia ujasiri dhidi ya maadui zake na pia walimkabidhi ngao kwa ajili ya ulinzi wa familia yake.

Pamoja na kuhutubia mkutano huo, Lowassa alihutubia mikutano mingine ya kampeni katika majimbo ya Solwa, Kishapu na Shinyanga Mjini na leo atakuwa mkoani Simiyu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles