Lowassa, Mbowe mbaroni Dar

0D6A9962*Polisi wavunja kikao cha siri cha Kamati Kuu

Na Veoronica Romwald

DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa wamekamatwa na Jeshi la Polisi.
Viongozi hao walikamatwa jana jijini Dar es Salaam na askari polisi waliokuwa wamevaa kiraia, baada ya kuvamia katika kikao cha Kamati Kuu ya dharura ya chama hicho kilichokuwa kinafanyika katika Hoteli ya Giraffe Ocean View.

Kikao hicho kilichoanza saa 5 asubuhi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Lowassa na wabunge wa chama hicho ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu.

Dalili za kuvunjwa kwa kikao hicho zilianza kujitokeza mchana, ambapo ilipofika saa 8:30 hali ilibadilika ndani ya kikao hicho, baada ya kufika maofisa wa polisi waliokuwa wamevaa kiraia na kuingia moja kwa moja hadi ukumbini na kwenda meza kuu ambako alikuwa amekaa Mbowe pamoja Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu upande (Bara), John Mnyika pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu akiwamo Edward Lowassa pamoja na Profesa Mwesiga Baregu.

“Wakati kikao kikiwa kinaendelea waliingia polisi waliokuwa wamevaa kiraia, licha ya kuzuiwa na walinzi wa chama hawakuelewa na kusema kuwa wana ujumbe muhimu kwa viongozi wa chama.
“Pamoja na mabishano ya muda mrefu waliingia ndani ya ukumbi wakiwa kama askari wanane na kwenda moja kwa moja meza kuu alipokuwa ameketi Mbowe na kumtaka avunje kikao.
“Hata hivyo Mbowe aligoma na kusema kuwa wao wapo kisheria ndani ya ukumbi ndipo wale polisi wakasema kwa kuwa amekaidi agizo hilo sasa viongozi wote wanatakiwa kutii sheria na wao wenyewe waende Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati.

“…Kutokana na agizo hilo wajumbe wengi walibaki wamepigwa butwaa na kulazimika kuahirisha kikao na kuongoza pamoja na viongozi hao kwenda polisi,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu.

Chanzo hicho kililiambia MTANZANIA kuwa muda wote polisi wakiwa ndani ya ukumbi huo walikuwa wakihoji uhalali wa kikao hicho ikiwemo agizo lililotolewa na Jeshi la Polisi la kuzuiwa kwa mikutano ya ndani pamoja na ile ya hadhara.

Hata hivyo kadiri muda ulivyokuwa unakwenda polisi waliongeza nguvu katika eneo hilo ambapo gari kadhaa za polisi zilionekana zikirandaranda katika eneo hilo.
Namna walivyofikishwa Polisi

Ilipotimu saa 10:20 msafara kati ya maofisa wa Jeshi la Polisi na viongozi hao uliwasili katika eneo la Kituo Kikuu cha Polisi Kati (Central), ambapo viongozi hao walishuka ndani ya magari na kuingia moja kwa moja katika chumba maalumu kwa mahoajiano.

Wakati wakiendelea na mahoajiano hayo baadhi ya wabunge na wanachama walianza kuwasili ili kujua hatima ya viongozi wao ambao walikuwa chini ya mikono ya polisi.

Hata hivyo walizuiwa kuingia ndani na kutakiwa kusimama mbali kabisa na mlango wa kuingilia kituoni hapo hali iliyowalazimu kwenda kukaa jirani eneo la stesheni.

Akizungumzia hatua ya kukamatwa kwa viongozi hao, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema wameshangazwa na hatua hiyo aliyoiita ya uonevu.
“Tulikaa Kamati Kuu kujadili mustakabali wa chama tulipo sasa na tufanye nini kusonga mbele lakini kabla hatujafika mwafaka askari walituvamia na kuwataka viongozi wetu kuvunja kikao,” alisema Msingwa.

Ilipofika saa 10:40 jioni wanasheria wa chama hicho wakiongozwa na Tundu Lissu waliwasili kituoni hapo ambapo nao walijikuta wakizuiwa kuingia ndani ya chumba cha mahojiano.
“Leo maajabu, haijawahi kutokea, chumba changu kimejaa wageni, “ alisema Lissu akifananisha chumba hicho ambacho naye amehoajiwa mara kadhaa na maofisa wa polisi wa kituo hicho.

Alisema hatua ya kukamatwa kwa viongozi wa Chadema si jambo la kushangaza kwani pamoja na hali hiyo bado hawajakata tamaa na wataendelea na harakati za kudai demokrasia ya kweli nchini.
“Viongozi wanakamatwa kwa sababu za kipuuzi zinazotolewa na Serikali, Magufuli kabla hata hajamaliza mwaka mmoja wa uongozi wake amepoteza kila sifa aliyokuwa aliyoanza kujipatia katika maeneo mengine.

“Kwa kuanzisha vita ya kuua demokrasia na atakumbukwa kwa kushindwa kuirejesha nchi katika mfumo wa chama kimoja hatua ya kutolewa kwa amri ya kuzuia vikao vya chama na maandamano ni haramu, wanasema tumekaidi lakini si kweli vikao na maandamano ni halali kwa mujibu wa sheria na tumeambiwa tuheshimu,” alisema Lissu

Alisema katika kikao hicho kulikuwa na wajumbe 178.
Wakati kina Lowassa wakihojiwa mwanamke mmoja mwenye umri wa makamu alizua tafrani katika geti la kuingilia kituoni hapo.

Hata hivyo haikufahamika bibi huyo alikuwa akihitaji kuonana na nani na ingawa maofisa wa jeshi hilo walimzuia kuingia, lakini alipita chini ya uzio wa geti hilo na kuingia ndani.
Muda kidogo mmoja wa maofisa wa jeshi hilo alimtoa nje ambapo aliondoka katika eneo hilo. Wakati viongozi hao wakiendelea kuhojiwa waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia wala kusogea katika eneo hilo la polisi.

Kauli ya Sirro

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, ili kujua sababua ya kushikiliwa kwa viongozi hao, alisema kwamba wamewakamta viongozi hao ili kujua sababu za wao kufanya mkutano hali ya kuwa imezuiwa.
Alisema mikutano hiyo imekuwa ikitumika kuchochea wananchi na kuwahamasisha kuvunja sheria za nchi kwa kufanya mapambano na Jeshi la polisi

“Ni kweli tunawashikilia viongozi kadhaa wa Chadema akiwemo Lowassa na Mbowe na kubwa tunataka kujua kikao chao wamefanya kwa sababu gani hali ya kuwa vimepigwa marufuku lakini wao wameendelea kufanya.

“Lakini pia tunataka kujua kwanini wanahamasisha maandamano wakati yatapelekea uvunjivu wa amani. Suala la kutolewa kwa dhamana siwezi kulisema kwa sasa maana bado tunaendelea na mahojiano nao,” alisema Kamanda Sirro alipozungumza na gazeti hili jana saa moja usiku.
Hata hivyo taarifa zilizopatikana jana usiku wakati MTANZANIA likienda mtamboni zilieleza kuwa, viongozi hao wa Chadema waliachiwa kwa dhamana.

Marufuku ya Polisi

Wiki iliyopita Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Nsato Msanzya (CP), alitangaza jeshi hilo, kupiga marufuku mikutano ya ndani yenye viashiria vya uchochezi na hata ikifanyika kwenye majukwaa watamshusha muhusika na kumfikisha kwenye mkono wa sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here