29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA, MBOWE, BULAYA WALALAMIKIA NJAA

LOWASA MBOWE

SHOMARI BINDA-BUNDA

Na MWANDISHI WETU-KAGERA

SIKU mbili baada ya Rais Dk. John Magufuli kukanusha taarifa za kuwako kwa tishio la njaa nchini akisema anayejua hilo ni yeye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema hali ya chakula hivi sasa ni mbaya.

Mbali na Lowassa, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya na wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare, wamesema hali ya njaa katika maeneo yao ni mbaya.

Kauli za wanasiasa hao wa upinzani zimekuja wakati juzi Rais Magufuli akiwa katika ziara yake mkoani Simiyu alikaririwa akisema: “Anayejua kuna njaa ni Rais wala si gazeti fulani, mimi ndiye nimepewa dhamana ya kuongoza Watanzania wote.”

Zaidi alikwenda mbali na kusema wafanyabiashara wanatumia magazeti kusema kuna njaa ili wasamehewe kodi ya mahindi yao waliyoyatoa Brazil kuja kuyauza hapa nchini.

Wakati Rais Magufuli akisema hayo, jana gazeti moja (Si Mtanzania) lilimkariri mmoja wa wateule wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba, akisema zaidi ya mifugo 3,000 imekufa wilayani kwake kwa kukosa malisho na maji kutokana na ukame.

Akizungumza katika mkutano mkuu maalumu wa Chadema Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera uliofanyika katika eneo la Bunazi, Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, alimtaka Rais Magufuli kutozipuuza hoja zinazotolewa kuhusiana na masuala mbalimbali ya nchi.

Kuhusiana na hali ya ukame nchini, Lowassa amesema hali ya chakula nchini hivi sasa ni mbaya sana.

“Tunamwomba Rais atafakari kwa uungwana hoja za watu wengine. Tunamheshimu ni rais lakini tunamwomba atafakari hoja hizi watu wasiendelee kuumia sana,” alisema Lowassa.

“Eneo moja ambalo hakika rais anatakiwa kusikia hoja za watu wengine ni suala la njaa. Nimeshuhudia mwenyewe pale Longido na maeneo mengine…hali ya mvua ni mbaya, hali ya chakula ni mbaya, watu wako hoi bin taaban halafu wanaambiwa hakuna kuwapelekea chakula!!” alishangaa Lowassa.

Akizungumzia juu ya madhila na wahanga wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Lowassa alielezea kushangazwa kwake na hatua ya rais kuamua kutopeleka misaada kwa wahanga hao akisema hata Mungu anashangaa.

“Mimi nakaa nasema mfano kama ni mama yako pale kijijini, halafu amekumbwa na janga hili, anaambiwa ajisaidie mwenyewe si atakushangaa, hata Mungu atashangaa,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare, amesema hali ya chakula katika Mkoa wa Kagera ni mbaya.

Kama ilivyo kwa Lwakatare kwa upande wake Bulaya alimwambia Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kuwa amekuwa akipokea ujumbe kutoka kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali wakilia matatizo ya njaa.

Katika hilo, Bulaya alimwomba Mbowe kulisemea jambo hilo kwenye ngazi ya Taifa.

Bulaya aliyasema hayo jana kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa chama hicho kilichofanyika wilayani Bunda.

Alisema licha ya ukame uliopo lakini  tembo wamechangia tatizo la njaa kutokana na kuharibu mazao mashambani.

“Mwenyekiti, hapa wananchi wana njaa na nimekuwa nikitumiwa ujumbe na wananchi wa jimbo langu wakilalamika kukosa chakula kutoka maeneo mbalimbali,” alisema Bulaya.

Katika ufunguzi wa kikao hicho, Mbowe alisema Taifa lina msiba wa njaa na amekuwa akipokea taarifa kutoka kwa wabunge wengi na ni vyema Serikali ikalifanyia kazi.

Alisema Watanzania waliwachagua viongozi si kwa kuwafanya watumwa bali kuendeleza nchi kwa misingi ya utu.

Mbowe alisema Watanzania wanalia njaa si kwamba ni wavivu bali ni hali ya ukame iliyopo na kwamba tatizo hilo halitaendeshwa kwa kauli za kukatisha tamaa kama zinavyotolewa na viongozi.

“Hili tatizo lipo na pale unapokuwa unawazuia binadamu kusema ipo siku mawe yatazungumza na ukweli utabainika kile ambacho Watanzania walikuwa wanakizungumzia kipo. Hifadhi ya chakula hapa nchini ilianzishwa ili kusaidia wakati wa majanga ya njaa, sasa leo kuna tatizo na wananchi wanasema lakini maneno yao yanakuwa yanapuuzwa, si jambo la kiungwana,” alisema Mbowe.

Akizungumzia hali ya kisiasa hapa nchini, Mbowe alisema yanayotokea sasa ya kuwafunga na kuwaweka mahabusu viongozi wa upinzani wakiwemo wabunge si suluhisho la kuendelea kupambana katika kuwazungumzia wananchi.

Alisema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, anasota mahabusu zaidi ya miezi miwili kwa kosa ambalo linastahili dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles