23 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Lowassa, Maalim Seif watikisa

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAKATI mwaka 2019 ukielekea ukingoni matukio kadhaa ya kisiasa yaliyojitokeza kuanzia Januari Mosi yanabaki kama kumbukumbu kutokana na mvuto, upekee na yenye kuvuta hisia.

Katika uchambuzi huu inaangazia matukio mbalimbali ya kisiasa yaliyotokea mwaka huu.

LOWASSA AREJEA CCM

Machi Mosi mwaka huu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alitangaza kurudi rasmi CCM baada ya kuwa nje ya chama hicho karibu miaka minne tangu alipokihama na kujiunga na Chadema.

Lowassa alihama CCM baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kupitisha mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015, katika Uchaguzi Mkuu uliomweka madarakani Dk. John Magufuli.

NASARI, LISSU KUVULIWA UBUNGE

Machi 14 mwaka huu, Spika Ndugai alitangaza kuwa jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Joshua Nassari, kupoteza sifa ya kuwa mbunge.

Nassari alivuliwa ubunge akiwa kwenye harakati za kutekeleza majukumu ya kibunge kwani alikuwa na Kamati alikuwa katika ziara ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyokuwa Chuo cha Mweka mkoani Kilimanjaro.

Aidha Juni mwaka huu, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, naye alivuliwa ubunge kwa madai ya kutohudhuria vikao vya bunge bila taarifa na kutowasilisha taarifa rasmi kuhusu mali na madeni.

Uchaguzi wa marudio uliitishwa Julai na mgombea wa CCM, Miraji Mtaturu, alitangazwa mshindi kutokana na kuwa mgombea pekee aliyerejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kati ya wagombea 13 waliojitokeza.

MAALIM SEIF AJIUNGA NA ACT 

Machi 18 mwaka huu, Mwanasiasa mwenye ushawishi katika siasa za upinzani visiwani Zanzibar na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikihama chama hicho na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe.

Hatua ya Maalim Seif kuachana na CUF ilitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliompa ushindi Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kutokana na mgogoro wa kiuongozi baina ya viongozi hao uliodumu tangu mwaka 2016.

Baada ya Profesa Lipumba kurejea CUF ambako alijitoa wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 akipinga uamuzi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa kuwa mgombea wao.

SAKATA LA CAG, NDUGAI

Aprili ilishuhudiwa mgogoro wa kiutendaji kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mstaafu, Profesa Musa Assad, baada ya kiongozi huyo wa Bunge kumtuhumu CAG kukidharau chombo hicho kwa kukiita kuwa ni dhaifu.

Spika Ndugai alimtaka CAG ajiuzulu hali iliyoibua hisia tofauti miongoni mwa wadau na taharuki katika mitandao ya kijamii huku likionekana kuchukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi. 

Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilimwita CAG bungeni na kumhoji kuhusu kauli hiyo kisha ikapitisha azimio la kutofanya naye kazi baada ya kumtia hatiani kwa madai kuwa kauli yake ililenga kulidhalilisha Bunge. 

Pia Spika Ndugai alijikuta katika mgogoro na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele, akisema sababu ni utovu wa nidhamu wa kiongozi huyo na kugonganisha mihimili huku alitangaza kusitisha kwa muda uwakilishi wa Masele. 

Ndugai alimtuhumu Masele kuwa amekuwa akipeleka maneno ya uongo kwenye ngazi ya juu ya Serikali na kwamba Bunge lilikuwa likimuita arejee nchini kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge lakini alikaidi. 

Baadaye Ndugai alimwandikia barua Rais wa PAP, Roger Dang, kumweleza juu ya kusitisha kwa muda uwakilishi wa Masele katika Bunge hilo ili arudi kujibu madai yanayomkabili. 

WARAKA WA KINANA, MAKAMBA

Julai 14 Makatibu Wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, walimwandikia barua Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Pius Msekwa, wakilalamika kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Makamba na Kinana kupitia waraka wao huo walieleza kuwa walizingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122 na kwamba waliwasilisha maombi yao wakiwasihi wazee wa chama watumie busara zao katika kushughulikia jambo hilo ambalo walidai linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.

Katika waraka wa wastaafu hao uliosambaa kwenye mitandano ya kijamii, Kinana na Makamba walieleza kuwa baada ya kufanya tafakari walipata majibu mtu huyo anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.

Katika kipindi hicho hicho kwa nyakati tofauti sauti zinazodaiwa kuwa ni za Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, Nape Nnauye (Mtama), Makamba na Kinana zilisambaa katika mitandao wakizungumzia kuandaa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwa makatibu hao wastaafu.

Kisha ikafuata sauti inayodaiwa kuwa ni mawasiliano ya Nape na Mbunge wa Sengerema, Wiliam Ngeleja na baadaye ikafuata ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

January, Ngeleja na Nape kwa nyakati tofatuti walimwomba radhi Rais Magufuli kutokana na vitendo hivyo.

Tayari kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichoketi Desemba 13, jijini Mwanza, kiliwasamehe na kuwaonya wabunge watatu, January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama) ambao walihusishwa katika sakata hilo kutokana na uamuzi wao wa kumwomba msamaha Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Aidha halmashauri kuu iliagiza Kinana, Makamba na Membe waitwe na kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho kuhusu sakata la sauti zao kusambaa katika mitandao wakizungumzia mpasuko ndani ya chama hicho.

Pia watahojiwa kuhusu waraka wao waliouwasilisha katika Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM wakidai uongozi wa chama umeshindwa kuwalinda dhidi ya mtu ambaye amekuwa akiwadhalilisha huku akilindwa na watu wenye mamlaka na kinga kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,800FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles