23 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Lowassa: Kura zangu milioni sita ziende kwa JPM

*Asema amerudi nyumbani, si kwa jirani

*Awapa neno Chadema, akemea kubaguana

ELIYA MBONEA-MONDULI

WAZIRI Mkuu wa zamani Edward Lowassa, amewaomba Watanzania na watu milioni sita waliompigia kura katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, sasa kuzielekeza kwa Rais Dk. John Magufuli katika kumuunga mkono.

Lowassa alisema hayo jana wilayani Monduli alipozungumza na viongozi na wanachama wa CCM ikiwa ni mara ya kwanza kuzungumza hadharani tangu Machi Mosi, mwaka huu alipotangaza kurudi katika chama hicho.

Mwanasiasa huyo alihama CCM mwaka 2015, baada ya jina lake kukatwa wakati wa mchakato wa kumsaka mgombea urais wa chama hicho na kuhamia Chadema na alipeperusha bendera Ukawa.

Akizungumza na wanachama hao katika viwanja vya CCM Wilaya ya Monduli, alisema katika uchaguzi huo alipata kura nyingi kidogo.

“Niligombea urais katika uchaguzi uliopita nilipata kura nyingi kidogo, si ndogo milioni sita. Lakini sasa nawaomba Watanzania wote ambao kwa upendo wao walinipa kura milioni sita wazielekeze kwa Rais Dk. Magufuli.

“Tumuunge mkono ili apate nguvu ya kuliongoza taifa letu aweze kuendelea na kazi zake, tushirikane tusaidiane,” alisema Lowassa.

Kuhusu Chadema, alisema: “kwa Chadema nawaambia asanteni sana viongozi na wanachama, asanteni nawashukuru sana, sina zaidi, msiniwekee maneno mdomoni, asanteni nawashukuru sana.”

Lowassa aliyepokelewa ofisini hapo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole, alisema: “Nimekuja kueleza kwanini nimerudi nyumbani, jibu lake ni rahisi tu, nimerudi nyumbani, nimerudi nyumbani basi sijarudi kwa jirani wala kwa mtu nimerudi nyumbani kwangu.

“Monduli mnafahamu historia yangu ndani ya chama tangu nikiwa mtoto mdogo sasa nimelelewa na chama hiki.

“Nawashukuru kwa kunikubali nawashukuru sana Rais Dk. Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Polepole kwa kunikubalia kurudi tena CCM,” alisema Lowassa.

Pia alitaja sababu nyingine iliyomfanya kurudi kuwa ni pamoja na kusukumwa na kazi nzuri inayofanywa na Magufuli na CCM.

“Mambo yanakwenda kwa kasi hii anaifanya Rais, nimekuja kuwaombeni tumuunge mkono ili kazi hii iendelee vizuri,” alisema Lowassa.

Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julisu Nyerere, Lowassa alisema na kuongeza: “Mwalimu aliwahi kutufundisha kwamba duniani hapa kuna aina mbili ya viongozi book keepers na vision leaders.

“Aina ya viongozi book keepers ni viongozi wanaoangalia hesabu zinakwendaje, IFM imesemaje ili wajiandae kuomba mikopo lakini vision leaders ni viongozi wanaotazama mbele miaka 50 ijayo.

“Napenda kuwaambieni Rais Magufuli ni kiongozi anayetazama mbele (Vision Leader), ndiyo maana nchi inakwenda kwa kasi sana inawezekana kukatokea makossa ya hapa na pale lakini nchi inakwenda kwa kasi inayopasa.

“Nidhamu ya wafanyakazi ipo katika hali ya juu sana tukienda hivi tukamsaidia nchi yetu itakwenda kwa kasi sana, kwa hiyo nimekuja kuwaambia mimi nimejiunga naye kushiriki katika mahitaji mapana ya nchi yetu.

“Sina shaka juu ya uongozi wake na tukimuunga mkono wote kwa pamoja tutafika mbali sana.”

AMANI

Akizungumza kuhusu amani, Lowassa, alisema ndiyo iliyosababisha CCM kushinda katika uchaguzi uliopita na Watanzania wamekuwa wakiithamini na imewapa sifa za kushinda kwenye chaguzi.

“Nimeanza kusikia maneno ya kibaguzi oo kama ni Muislamu usiende kwake, kama ni Chadema usiende kwake na kadhalika na kuambiana tubaguane hili ni jambo baya hata Monduli limetokea.

“Hata hapa Monduli limetokea kuna rafiki yangu aliambiwa ukienda kwa Lowassa watapeleka jina lako kwa mkuu wa wilaya, sasa yarab jina la mkuu wa wilaya linahusika vipi na kuja nyumbani kwangu.

“Kuanzisha vitu vya aina hii havitusaidii tupingane bila kubaguana, tuheshimiane Mkristo akitaka kwenda kwa Muislamu aende vile vile na Muislamu akitaka kwenda kwa Mkristo aendee.

“Tumekaa hapa miaka mingi tukianza kuleta chokochocho itatuharibia, ni imani yetu na chama chetu kwamba tutaishi kwa imani hiyo kwa faida ya Watanzania wengi,” alisema Lowassa.

MAENDELEO

Akizungumza kuhusu maendeleo, aliwaambia wananchi waliofurika kwenye viwanja hivyo kwamba Benki ya Dunia (WB) imeanzisha utaratibu wa kupima maendeleo kwa kuangalia uchumi wa nchi umekuwa kwa kiasi gani.

“Sasa kigezo pekee si takwimu tena, bali kigezo kinaangalia hali ya mtu masikini ametoka katika umasikini kwa hali gani, hali yake ya maisha ikoje, Benki ya Dunia wakagundua Rais wa Brazil alikuwa na mgogoro kwenye chama chake.

“Lakini katika hali ya kipekee Rais yule wa Brazil aliambia amevunja rekodi duniani kwa kuweza kuwaendeleza watu milioni 250 kwa kuwatoa katika umasikini na kuwapandisha kwenye maisha bora.

“Hivyo ndio vipimo vinavyotakiwa katika maendeleo ya nchi naamini Rais Magufuli anaweza kuvifuata na tukaenda vizuri,” alisema Lowassa.

Pia alimshukuru Polepole kwa kumpokea na huku akikumbushia alivyokuwa akishambuliwa katika vyombo vya habari.

“Namshukuru sana Polepole kwa kuwakilisha Makao Makuu, alinigonga kweli zamani alikuwa akinisema kweli kweli kwenye TV lakini kwa sasa ni ndugu moja tunaelewana kuijenga CCM.

POLEPOLE

Awali, Polepole alisema wakuu wa chama hicho walitumia saa nne kuzungumza na Lowassa.

“Lowassa alitueleza mambo mazito alitoa sababu za msingi, chama chetu kinaendeshwa kwa utu, sasa sisi ni nani tusimsamehe kwa sababu imeandikwa msamehe ndugu yako saba mara 70.

“Lowassa alikuwa mgombea wa vyama vyote vya upinzani sasa wewe nani uendelee kubakia huko,” alisema.

MAMIA WARUDI CCM

Katika mkutano huo, Polepole aliwalisha kiapo wanachama waliorudi CCM wakiongozwa na Lowassa.

Polepole alizungumzia kanuni za chama hicho aliwataka wanachama wengine wanaotaka kurudi kuandika barua ngazi ya tawi ili waweze kujadiliwa kama alivyofanya Lowassa.

“Kikao cha tawi kilijadili barua ya Lowassa na kikaridhia Lowassa kurudi CCM,” alisema Polepole.

Kati ya waliorejea CCM yumo pia aliyekuwa Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole.

UWANJA WA NDEGE ARUSHA

Mamia ya wanachama wa CCM walianza kufurika kwenye uwanja huo kwa ajili ya kumpokea na aliwasili saa 6:20 mchana akiwa ameongozana na mkewe Regina Lowassa, mtoto wake Robert Lowassa, marafiki Khamis Mgeja, Matson Chizii na Edward Porokwa.

Uwanjani hapo alipokelewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM Mkoa wa Arusha, Daniel Awakii, Goodluck Medeye, Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Arusha John Pallangyo.

MONDULI

Alipowasili ofisi za CCM wilayani humo Lowassa alipokelewa na Polepole, pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Lootay Sanare.

Wakitoa salamu zao, baadhi ya wabunge wa mkoa huo akiwamo Julius Kalanga (Monduli), alimkaribisha Lowassa nyumbani akisema amekuwa baba na mlezi wa watu.

Mbunge wa Simanjiro, James ole Milya, alisema: “Mimi ni kijana wako umenisaidia na fahamu uwezo wako na uzalendo wako.

“Mungu hakukosea mwaka 2015 wewe usiwe rais wa nchi hii, kwa sababu hakuna watu ambao ungeweza kuongoza nao nchi kule Chadema.

“Niliondoka mwaka 2012 na tuliorudi CCM hatukukosea, tulienda kujifunza na kujua udhaifu wao.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,800FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles