29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA , KIKWETE WANAWASILIANA – RIDHIWANI

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


RAIS mstaafu Jakaya Kikwete, amekuwa akiwasiliana na kujuliana hali na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kwa kadiri muda unavyowaruhusu.

Hayo yameelezwa jana na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete wakati akihojiwa na mtangazaji wa Ayo Tv, Millard Ayo ikiwa ni siku moja baada ya picha zake kusambaa katika mitandao mbalimbali ya jamii zikimwonyesha akisalimiana na Lowassa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mahojiano hayo, pamoja na mambo mengine, Ridhiwani ambaye pia ni mtoto mkubwa wa kiume wa Kikwete, alisema picha iliyojengwa kwa baadhi ya wanajamii kuwa baba yake na Lowassa ni maadui, haina ukweli wowote bali ni marafiki na wamekuwa na mawasiliano ya simu na wakati mwingine ya ana kwa ana.

Ridhiwani alisema watu wanapaswa kutenganisha urafiki wa kazi na nje ya kazi.

Alisema nje ya kazi Kikwete na Lowassa ni marafiki, wanawasiliana na kusaidiana na kwamba urafiki wao ndio umewafanya watoto wa familia hizo mbili kuwa huru kwa wazazi wao.

“Hakuna ugomvi wowote baina ya watu hawa wawili, ujue watu wanashindwa kuelewa kwenye masuala ya kazi hakuna urafiki, mfano kwenye suala la kutafuta urais, si la Jakaya peke yake.

“Na kama ni hivyo watu walisema Membe (Bernard) ni rafiki wa JK. Sasa kama ni kweli angeshindwa kumpa urais kama ndivyo watu wanavyoamini? Mchakato ule wa urais uko huru na yeye kama mwenyekiti wa chama kazi yake ilikuwa kusimamia tu.

“Na sisi tuko huru kabisa na ingekuwa kuna ugomvi baina ya Lowassa na JK ningekwendaje pale kumsalimia? Si angenitukana au kunipiga kofi, kile ni kilelezo cha upendo baina yetu. Ukweli ni kwamba JK na Lowassa wanaongea na wanawasiliana kwa simu,” alisema Ridhiwani.

Alipoulizwa kuhusu alichoongea na Lowassa alipokwenda kumsalimia walipokutana wakati wa mchezo wa mpira baina ya Simba na Yanga, alisema aliitumia pia fursa hiyo kubadilishana naye mawazo kwa sababu alikuwa hajamwona muda mrefu.

“Tukiwa pale uwanjani, nilipomwona nikaenda kumsalimia shikamoo baba, akaitikia hujambo mwanangu na akaniuliza kama mzee hajambo, nikamwambia hajambo lakini yuko Ethiopia, akasema akirudi msalimie sana,” alisema Ridhiwani.

Aidha Ridhiwani alisema alipigiwa simu na baba yake kutokea Ethiopia kumweleza kuwa ameona picha yake kwenye mitandao ya kijamii akiwa anasalimiana na Lowassa na kumuuliza walipokutana, akamjibu wamekutana Uwanja wa Taifa wakati wa mechi ya Simba na Yanga.

 “Jana (juzi) jioni mzee alinipigia simu alikuwa yuko Ethiopia, akaniambia ameniona niko na bwana Edward (Lowassa), nikamwambia ndio nimeona naye, akaniuliza tumekutana wapi, nikamwambia tumekutana Uwanja wa Taifa, akasema na yeye alikuja kuangalia mpira nikamjibu ndiyo.

“Akasema hayo ndiyo mambo mnayotakiwa kufanya, msifikie sehemu mkaona siasa ni vita, siasa si vita. Ndiyo maana nilipoongea na mzee pale pale nikaenda kwenye ukurasa wangu wa instagram nikaweka ile picha, nikaandika pale kuwa naendelea kujifunza, hiyo ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya ile ‘post’ yangu juzi,” alisema Ridhiwani.

Akizungumzia kuhusu baba yake anapokuwa nyumbani, alisema kuna wakati anakasirika, lakini mara nyingi huwa haonyeshi hasira zake na kwamba ana tabia ya kuuacha muda uzungumze.

“Kwa mfano wakati wa uongozi wake, akiona nchi inachemka, utakuta anashambuliwa kwenye mitandao ya kijamii, lakini alikuwa anakaa kimya halafu baadaye anakwenda kuzungumza na kumaliza kabisa jambo hilo kwa sababu alijipa muda wa kutafakari katika sura zote.

“Kuna wakati nikiwa kama mtoto nikiangalia kwenye mitandao watu wanamtukana, kuna siku nilisoma ‘comment’ niliumizwa sana, nikamfuata mzee nikamwambia hivi mambo haya mpaka lini? Akaniangalia akasema mwanangu ungekuwa unajua nguvu aliyonayo rais usingeyasema haya. 

“Yeye alielewa nguvu aliyaonayo rais, hivyo akawatazama wale waliokuwa wanamdhihaki, wanamtukana halafu nafikiri akamwachia Mungu. Na ndio leo hao hao waliomtukana na kumdhihaki wanasema wanam-miss JK, na ndio rundo la hao waliomtukana na kumdhihaki. Mzee ni mtu mwenye huruma sana,” alisema Ridhiwani.

Akielezea kuhusu taarifa kwamba wana undugu na Membe, alisema taarifa hizo hazina ukweli.

Alipoulizwa kuhusu jinsi alivyoingia katika harakati za kisiasa, alisema alipokwenda kwa baba yake kumweleza nia yake hiyo, alimuuliza kama ana uhakika wa kushinda na kumshauri kuwa asiingie kwenye siasa kwa sababu ana watu wanaomuunga mkono bali angie akiwa na ajenda.

Akizungumzia kuhusu tatizo la maji jimboni kwake, Ridhiwani alisema awamu ya kwanza na ya pili ya mradi wa maji imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

“Lakini ukamilifu huu ili yaweze kupatikana maji yanatakiwa yapatikane matanki katika awamu ya tatu, sasa fedha imeshatolewa, kuna matatizo ambayo tunajaribu kufuatilia na tayari tumeshazungumza na Waziri wa Maji,” alisema.

Kutokana na hilo, alimtahadharisha Waziri wa Maji kwamba akiendelea kuwasumbua kwa kutotatua tatizo hilo na yeye atamsumbua bungeni.

“Kwa lugha nzito ni kwamba Waziri wa Maji akiendelea kutusumbua na sisi tunayo sehemu ya kumsumbulia maana leo ukinikatalia huku mimi nitaenda kukukamatia bungeni pale, sasa hatutaki tufike huko.

“Lakini la msingi wizara au Serikali lazima isimamie huu mradi na kama hakuna hela ni bora waseme kwamba hakuna hela hivyo tusubiri.

“Watu wa Chalinze wamesubiri maji tangu uhuru, sasa leo wameona miundombinu, maji hakuna, ile kiu kama ilikuwa namba mbili sasa itakuwa imefika namba sita, mfano zamani watu walikuwa wanakunywa maji kwenye marambo wanachimba halafu wanachota maji sasa kurudi tena huko tunahatarisha maisha.

“Lakini pamoja na changamoto hizi kabla ya mwaka 2020 inawezekana tatizo la maji likaisha kama Serikali itatekeleza mpango tuliopanga,” alisema Ridhiwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles