23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Lowassa: JK ajihukumu mwenyewe

lowassa*Asema hana kinyongo naye, amvaa JPM

*Agusia mikakati ya kuingia Ikulu 2020

 

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Ukawa, Edward Lowassa, amemtaka Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ajihukumu mwenyewe kutokana na matendo aliyoyafanya dhidi yake.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano yaliyorushwa na kituo cha Luninga cha Azam kupitia kipindi cha Funguka kilichoongozwa na mtangazaji mkongwe, Tido Mhando, huku akisema hana kinyongo na Kikwete.

Lowassa alitoa kauli hiyo alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na rais huyo mstaafu wa awamu ya nne, ambapo wawili hao walikuwa maswahiba wakubwa, lakini walikuja kutofautiana wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM mwaka jana.

“Siwezi kumhukumu Kikwete (Jakaya) yeye mwenyewe  ila wengine wamuhukumu na yeye ajihukumu mwenyewe, sijamwona hivi karibuni lakini sina kinyongo naye,” alisema Lowassa ambaye kwa sasa ametimiza mwaka mmoja tangu alipojiunga na Chadema Agosti mwaka jana.

Kutokana na hatua hiyo Lowassa pamoja na watu waliokuwa wakimuunga mkono ndani ya CCM waliweza kufunguliwa mafaili ndani ya CCM sambamba na kufuatiliwa nyendo zao, ambapo wakati wa mchakato huo jina la mwanasiasa huyo lilikatwa na Kamati ya Maadili chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye alikua mwenyekiti wa CCM taifa.

AMANI NA HATI MILIKI

Pamoja na mambo mengine, Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema kila mtu ana wajibu wa kuheshimu amani ya nchi na kwamba hakuna mwenye hati miliki.

Kutokana na hilo, alimtaka Rais Dk. John Magufuli, kuwa na utamaduni wa kufanya mazungumzo na wanasiasa ili kufikia mwafaka wa mambo ya kisiasa nchini.

“Serikali inatakiwa kuwa na tabia ya kuzungumza na si kutumia ghadhabu, sisi wote ni Watanzania kwanini tunaogopa kuzungumza. Siku zote mazungumzo ndiyo njia bora ya kufikia maridhiano,”alisema.

ZUIO LA MIKUTANO

Akizungumzia kuhusu mikutano ya siasa kuzuiwa, Lowassa alieleza kushangazwa kwa kitendo cha Rais Magufuli kupiga marufuku hiyo huku yeye akizunguka kufanya mikutano ya hadhara.

Alisema kwa kuwa aligombea urais mwaka jana na akachaguliwa na Watanzania milioni sita hivyo ana haki ya kuzunguka mikoani kuwashukuru waliompigia kura.

Pia alishangazwa na barua ya Msajili wa Vyama Siasa, akisema imejaa ghadhabu na si uongozi.

“Yeye anakwenda Kahama (Rais Magufuli)…kuwashukuru wananchi anafanya mikutano ya hadhara kwa nini na mimi nisiende Mbeya na Iringa kushukuru. Nimeona barua ya msajili imejaa ghadhabu zaidi si uongozi,”alisema Lowassa.

OPERESHENI UKUTA

Akizungumzia kuhusu operesheni Ukuta iliyozinduliwa hivi karibuni na Chadema, Lowassa alisema ni sahihi huku akisisitiza yafanyike mazungumzo kabla ya kufikia Septemba Mosi, mwaka huu.

“Yafanyike mazungumzo ya kushughulika na mambo haya kabla ya kufika Septemba Mosi, haiwezekani chama cha siasa eti hakuna siasa mpaka mwaka 2020…hili lazima litazamwe.

“Ukitoa amri, amri, amri za kiimla tuzungumze kila mtu anaheshimu amani ya nchi hii, tuzungumze tutaelewana,”alisema.

Alisema mtu akitaka kuvuruga maendeleo huanza kuvuruga vyama vya siasa.

NINGEFANYA VIZURI ZAIDI YA JPM

Alipoulizwa tathmini yake kuhusu utawala wa Rais Dk. Magufuli, alisema anafanya vizuri lakini ingekuwa yeye asingeanza na madawati bali angeanza na masilahi ya walimu.

“Magufuli anafanya vizuri katika maeneo fulani lakini mimi ningefanya vizuri zaidi, kama nilivyosema kipaumbele changu ni elimu, elimu, elimu…nisingeanza na madawati, ningeanza na masilahi ya walimu.

“Madawati ni sehemu ndogo sana ya elimu, wangechukua kwa ujumla na si madawati tu. Sisi upinzani tungeanza kwa ujumla wake, Serikali inapaswa ishughulike na mambo makubwa, madawati ni kazi ya makatibu kata.

“Kuna maeneo kwa maoni yangu ni muhimu zaidi ajira, lipo tatizo la ajira hapa nchini. Ajira haitazamwi mama ntilie, bodaboda tunawakimbiza barabarani hawana ajira.

“Kuna jambo lingine asaidiwe Rais, Serikali inatakiwa iheshimu mihimili mitatu, mfano alikwenda mahakamani siku ya Law Day (Siku ya Sheria),  akawaambia mkimaliza kesi zangu haraka na mkawatia hatiani nitawapeni hela ya kujenga majengo yenu, nadhani hakuwa na maana hiyo lakini ilitafsiriwa kwamba anatoa hongo,”alisema Lowassa.

AJIVUNIA SHULE ZA KATA

Lowassa alisema anamshukuru Mungu kushika bendera ya kusimamia shule za kata wakati akiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya nne.

“Namshukuru Mungu kushika bendera ile, najivunia kwa kweli nafurahi shule moja iliyoongoza ni ya kata. Naamini leo (jana),  zile shule zingekuwa mikononi mwangu zingekuwa mbali zaidi na bora,” alisema.

WABUNGE UKAWA

Akizungumzia mwenendo wa Bunge, Lowassa alisema tatizo kubwa kwa ujumla wake ni kutokana na Spika wa Bunge, Job Ndugai,  kutokuwapo bungeni.

Alisema tatizo lingine ni la kisaikolojia kutokana na Naibu Spika, Dk.Tulia Ackson, kuwapo katika nafasi hiyo kwa njia ambayo wengine wanaona si sahihi.

“Tatizo katika ujumla wake ni kutokana na Ndugai kuwa na hali mbaya ya afya namfahamu ni mtu makini sana…angekuwapo yale mambo yasingefikiwa.

“Kuna tatizo la kisaikolojia Naibu Spika amekuwa katika nafasi ile kwa njia ambazo pengine wengine wanaona si sahihi anachukua maamuzi ambayo ni magumu kidogo naelewa wabunge wetu kuchukua hatua ile ni sahihi…wangefanya nini?

“Siku ambayo wamejiweka plasta midomoni, Marekani nao walikuwa wamekaa chini mpaka asubuhi kupinga hoja ya Serikali, hivyo ni njia ya ku-express (kufikisha),  kutoridhika kwao, walistahili kufanya hivyo  kwa sababu haki yao haikusikilizwa.

“Wangekubali kuzungumza…bajeti imepita bila upinzani, hii si salama kwa demokrasia …siasa ni kuzungumza, naona ndicho kinachokosekana,” alisema Lowassa.

KUHAMIA DODOMA

Alisema viongozi wa awamu zote walikuwa na dhamira ya kuhamia Dodoma lakini kutokana na matukio fulani fulani makubwa mambo yanabadilika.

“Ninawatakia heri lakini wasiende kwa kasi sana wasije wakavunjika miguu.. utekelezaji wa kuhamia Dodoma ufanyike kisayansi, wanaweza kuchukua fedha za miradi ya maendeleo ili kuhamia Dodoma,”alisema.

MWAFAKA  Z’BAR

Kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, Lowassa alimwomba Rais Dk. Magufuli,  kulitazama suala hilo kwa kuwa hawezi kulikwepa na kwamba mwaka 2020 ni mbali kusubiri mwafaka.

“Namwomba Rais alitamaze hili la Zanzibar ni sehemu ya nchi yetu, mambo yanayotokea kama ni kweli yanatia kichefuchefu, kuna sauti ya watu wengi tusipuuze.

“Rais alisema si suala lake lakini hawezi kukwepa, watu wanakamatwa wanafungwa, Amani Karume alifanya vizuri kuleta Serikali ya maridhiano,” alisema.

Mwanasiasa huyo alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kufanyika mazungumzo kwa sababu watu wakionewa kwa muda mrefu wanachukua maamuzi ya hamaki.

“Kwanini usizungumze nao badala yake unachukua uamuzi tu. Aliniambia Maalim Seif tupewe kibali uchaguzi usimamiwe na AU (Umoja wa Afrika)  tusiachie watu wanaumia, tuzungumze na tukisema tusubiri mwaka 2020 miaka hiyo ni mingi sana lazima tuzungumze  tukafikiri amani ni salama.

“Wakati ule hata mimi walitaka nitangaze matokeo na pengine hali ingekuwa tofauti kidogo, watu hawakuridhika…kwanini tusizungumze, kuchukua ubabe tu hapana bwana please ni maisha ya watu. Tumekatiwa misaada na MCC na miradi imesimamishwa,”alisema Lowassa.

KATIBA MPYA

Akizungumzia kuhusu Katiba Mpya, alisema hilo ni suala gumu na kwamba linahitaji fikra mpya, kuvumiliana.

“Serikali haijatoa muda wa mazungumzo ilichukuliwa ghadhabu mpaka leo hatuna Katiba, tuzungumze…Katiba ni suala gumu linahitaji muda mrefu wa kuelewana. Fikra mpya, kuvumiliana na research (utafiti) ,”alisema Lowassa.

UTEUZI

“Zamani ili upate ajira kama hizi ulikuwa vetted (utathiminiwe). Siku hizi inakuja kugundulika mteuliwa si raia siku anaapishwa. Tusiwe intimidated (tunatishwa) na elimu, kwamba huyu kasoma sana.

“Kuna watu wana PhD (Shahada ya Uzamivu),  lakini wanafanya kazi vizuri. Katika mkutano mmoja Mwalimu Nyerere (Julius) alipata kusema kwamba Profesa anashikilia kitu kimoja kidogo mambo mengi hayajui…sasa hii ya amesoma, amesoma si kigezo pekee kuna uadilifu na uzalendo,”alisema Lowassa

URAIS 2020

“Wataniona Ikulu 2020, sina mashaka tukiwa na Katiba nzuri njia ni nyeupe… si vizuri kueleza mikakati yangu. Ukifanyika uchaguzi wa haki na kweli huku tume ikiwa huru, sina wasiwasi,”alisema.

UCHAGUZI 2015

“Haukuwa sawa hata kidogo… tuache mambo haya uchaguzi umeshamalizika tutaumizana mioyo bure, nina imani na upinzani tuna nguvu sana,” Lowassa alisema hayo alipotakiwa kuzungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles