Lowassa: Jeshi la Polisi linatumika vibaya

Edward Lowassa,
Edward Lowassa,
Edward Lowassa,

Na ELIUD NGONDO, MBEYA

WAZIRI Mkuu wa zamani aliyegombea urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Edward Lowassa, amesema Jeshi la Polisi linatumika vibaya.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Mbarali mkoani Mbeya, alipokuwa akihutubia wananchi nje ya Ukumbi wa Lutheran uliokuwa ufanyike mkutano wake wa ndani baada ya polisi kuufunga.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwataka wananchi kuwa watulivu na wasifanye fujo baada ya zuio hilo la polisi.

“Wananchi endeleeni kuwa watulivu, polisi wamezuia mkutano halali, msifanye fujo yoyote na pokeeni maelekezo kwa viongozi kwani nitarudi tena siku nyingine, pole sana kwa adha mliyoipata.

“Niseme Jeshi la Polisi linatumika vibaya, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kuivunja demokrasia ya vyama vingi na sheria na 5 ya mwaka 1992 ya uanzishwaji wa vyama vingi,” alisema Lowassa.

HALI ILIVYOKUWA

Mkutano huo ulizuiwa na polisi ambao walifunga ukumbi kwa ufunguo jana saa 5:40 asubuhi na kuwazuia kuingia ndani mamia ya wananchi na wanachama wa Chadema Wilaya ya Mbarali waliofika kumsikiliza Lowassa.

Alipowasili katika eneo la tukio, Lowassa alijikuta akikwama kufanya mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika hapo baada ya kukuta askari polisi wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbarali (OCD), L. Muhaji ambaye aliufunga ukumbi huo kwa kufuli.

Hatua hiyo ilimfanya Lowassa kubaki ndani ya gari lake, huku viongozi wa Chadema wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa), Frank Mwaisumbe pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Hashim Issa wakimfuata OCD juu ya hatua yake ya kufunga ukumbi huo.

Katika majadiliano hayo, OCD Muhaji aliwajibu viongozi hao kwamba amepokea maagizo kutoka ngazi za juu ya kuzuia mkutano huo kwa sababu walishapewa maelekezo katika vikao vyao, na hakuna haja kwa viongozi wa kitaifa kufanya mikutano wilayani humo.

Baada ya kusubiri kwa zaidi ya dakika 10, Lowassa alilazimika kushuka ndani ya gari na kwenda walipo viongozi hao na OCD.

Alipomuuliza OCD huyo kuhusu hatua yake ya kufunga ukumbi huo, majibu yake yalikuwa kama aliyowapa viongozi wa kanda.

“Ndugu yangu (OCD) inakuwaje hali hii? IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu) alisema haitakiwi polisi kuingilia shughuli za mikutano ya ndani, sasa wapigie wakubwa wako wakupe ‘confirmation’ (wakuthibitishie) ili uachie funguo za ukumbi,” alisema Lowassa wakati akizungumza na OCD.

Pamoja na hali hiyo, OCD huyo alipopiga simu kwa viongozi wake wa juu, haikupokewa hali iliyomlazimu Lowassa kumpigia simu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ili kupata maelezo ya suala hilo, lakini pia haikupokewa.

MTANZANIA lilipomtafuta Makalla kwa njia ya simu ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, simu yake haikupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu pia haukujibiwa.

AZUIWA KWENDA RUKWA

Awali jana asubuhi, Lowassa alijikuta akikwama kwenda katika mikoa ya Rukwa na Katavi baada ya polisi kuuzuia msafara wake kwa hofu kwamba unaweza kuingilia ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anayetembelea mikoa hiyo.

Lowassa alianzia ziara yake mkoani Mbeya tangu Agosti 21. Juzi alifanya vikao vya ndani katika majimbo yanayoshikiliwa na wabunge wa chama chake mkoani Songwe, na jana asubuhi alitarajiwa kwenda Katavi na Rukwa.

Katika Mikoa ya Rukwa na Katavi, alitarajiwa kufanya mikutano ya ndani majimbo ya Nkasi Kaskazini, Kusini na Sumbawanga.

Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Kanda ya Nyasa), Frank Mwaisumbe, alisema kwamba polisi walimpigia simu Lowassa juzi saa 1.00 jioni akiwa Tunduma, wakimtaka aahirishe ziara yake Mkoa wa Rukwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Gorge Kyando, alipoulizwa kwa njia ya simu, alisema waliwashauri viongozi wa Chadema wapange siku nyingine ya ziara kwa sababu mkoa ulikuwa na ugeni mkubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here