24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA: HUWEZI KUZUIA GURUDUMU LA DEMOKRASIA

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema gurudumu la demokrasia limekwisha kuanza nchini hivyo ni vigumu  kulizuia.

Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,  alirejea  Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam jana baada Juni 27 kuhojiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Alihojiwa  kwa takriban saa nne juu ya kauli alizozitoa kuhusu viongozi wa dini wa kundi la Uamsho na akatakiwa kurudi  jana saa 6.00 mchana.

Akizungumza ofisini kwake Mikocheni, Lowassa alisema baada ya kuitikia wito wa polisi jana, hakuna mengi aliyoambiwa zaidi ya kuelezwa kuwa  upelelezi wa suala hilo unaendelea hivyo arejee  ofisini hapo Julai 13.

Alipoulizwa analichukuliaje suala hilo la kutakiwa kwenda  polisi mara kwa mara  alisema: “Njoo kesho, njoo kesho kutwa ni sehemu ya kazi yao (polisi).

“Kuhusu maoni yangu nitawaambia baada ya kumaliza hili, isionekana naingilia.

“Lakini nieleze jambo moja, demokrasia ikishaanza kuizuia ni taabu sana.

“Unaweza ukapunguza spidi ya gurudumu la demokrasia lakini huwezi kuiondoa, demokrsia imeshaanza, inaendelea, ni vigumu kuizuia.

“La pili, nichukue nafasi hii kuwaomba wanachama wa chama chetu na wananchi na wanaotutakia mema wasiwe na  shaka kila kitu kipo chini ya utaratibu mzuri.

“Tuko sawasawa, tuko sahihi na tunatekeleza kama alivyosema (Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe). Tunatekeleza sera ya chama chetu, wasiogope wawe na amani, watulie,” alisema Lowassa.

Alivyoulizwa kama wakati anatoa kauli kuhusu viongozi hao wa Uamsho labda aliteleza, Lowassa alisema, “I stand by what I said” (naisimamia kauli yangu).

Alisema anaamini alichosema ni sahihi kama alivyoeleza Mbowe na kwamba suala la msingi ni kuachiwa kwa Masheikh wa Uamsho.

Lowassa alisema Chadema  kama chama hakisemi kama viongozi hao wa dini wana makosa ama hawana, ila wamekaa ndani kwa muda mrefu bila kesi zao kusikilizwa.

“Wamekaa vya kutosha, hilo ndilo la msingi tunaloomba… katika hotuba yangu nilisema na kwenye magazeti waliandika vizuri, wale walioko madarakani wana mamlaka.

“Mtu mwenye dhamana ya kuwatoa ni Rais. Nikawaeleza wajipange wakaongee na Rais wamwambie ‘mzee, wenzetu tunaomba waachiliwe’.

“Mwenye madaraka ya mwisho ni Rais, mkiendelea na mahakama miaka minne, nane siyo… kwa hiyo narudia, ni vema wakamuombe Rais awaachilie.

“Sintoshangaa akitekeleza (akawaachia) kwa sababu juzi ametekeleza moja ya uamuzi wetu wa kuunda tume ya kuchunguza madini, tulivyokuwa Kahama tulisema tutaunda tume.

“Waendelee na uchunguzi wao (juu ya kauli yake), lakini narudia, gurudumu la demokrasia likianza kulizuia ni  taabu sana.

“Narudia mwenye mamlaka ya mwisho kuombwa na kushawishiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisema Lowassa.

Mbowe

Awali, Mbowe alisema suala alilolisema Lowassa ni miongoni mwa  mambo ya kwenye ilani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) iliyonadiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Alisema  hata yeye alipofuturu  na baadhi ya waumini wa jimboni kwake Hai mkoani Kilimanjaro hivi karibuni, walimwambia suala la kuachiwa kwa masheikh hao  bado halijapigiwa kelele za kutosha.

Mbowe alisema masheikh hao walikamatwa wakati Said Mwema  akiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, akafuatiwa na  Ernest Mangu  sasa ni Simon Sirro, huku pia Ma- DCI wakiwa wamebadilishwa kadhaa bila upelelezi wa  suala hilo kukamilika.

Alisema ni vema sasa upelelezi uliokusanywa wakati viongozi hao wakiwa polisi, utumike kuwahukumu au kuwaachia kwa dhamana.

Awali akizungumza karibu na makao makuu ya polisi, Mbowe alisema katika mazingira yenye utawala bora, viongozi wana wajibu wa kuheshimiana.

“Lowassa ni kiongozi mwandamizi wa nchi hii na wala si jambazi, kama polisi waliona uchunguzi haujakamilika wangeweza kufanya mawasiliano na kumwambia asije leo (jana).

“Hatukatai wito wa polisi lakini mambo mengine yanayofanywa ni ya uonevu na ubabe, wanazuia viongozi kuingia ndani ,” alisema Mbowe.

Alisema yeye na wenzake walilazimika kuacha bunge na shughuli nyingine ili kumsindikiza Lowassa lakini wameshangazwa na jinsi suala hilo lilivyo.

Alisema alichozungumza Lowassa tangu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 na kwenye futari wiki iliyopita ni sahihi kwa sababu  masheikh hao wa Uamsho wamekuwa mahabusu kwa muda mrefu bila   suala lao kuamuriwa.

“Polisi na serikali wasitufunge mdomo, hoja ya masheikh kukaa mahabusu kwa miaka mingi si jambo geni na linalalamikiwa.

“Kama Watanzania hawataongea kuhusu viongozi wa dini nani ataongea…tutaendelea kusema kadiri iwezekanavyo  ili kila mmoja apewe haki kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa Chadema pia alilaani hatua ya Jeshi la Polisi kuwafukuza waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia tukio hilo.

“Polisi lazima waelewe kwamba wanapotengeneza tukio lolote ni habari na waandishi wa habari ni sehemu muhimu katika kupashana taarifa.

“Ninyi waandishi wa habari mnakuwa marafiki  mnapohitajika kuuelezea umma taarifa ambazo zinalijenga jeshi la polisi lakini wakati mwingine wao wanawakataa,” alisema.

KIBATALA

Wakili wa Chadema, Peter Kibatala, alisema taratibu za upelelezi hazijakamilika hivyo Lowassa atatakiwa kurudi tena polisi Julai 13 mwaka huu.

“Lowassa aliripoti ofisi ya DCI kama alivyoelekezwa lakini jana hakukuwa na mahojiano.

“Tutakaporudi tena ndio tutafahamishwa nini kitakachofuata, kama suala hili litaishia polisi ama kupelekwa mahakamani,” alisema Kibatala.

KUWASILI POLISI

Lowassa aliwasili katika Makao Makuu ya Polisi saa 5:53 asubuhi huku akiwa ameongozana na mkewe, Regina Lowassa na viongozi wengine wa Chadema.

Hata hivyo aliingia katika ofisi hizo akiwa na mkewe na Wakili Kibatala huku viongozi wengine wakitakiwa kusubiri nje.

Hali ya usalama ilikuwa ya kawaida tofauti na Jumanne wiki hii ambapo kiongozi huyo aliripoti kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo waandishi wa habari walipata wakati mgumu kwa kutakiwa kuondoka eneo hilo baada ya Lowassa kuwasili.

Ya Kibiti

Mbowe akitoa maoni yake juu ya mambo yanayoendelea kwenye Wilaya za Mkuranga na Kibiti, Mbowe alisema ni vyema wanasiasa wakaacha vyombo vya ulinzi na usalama vikafanya kazi yake na kumaliza tatizo hilo.

Alisema kila wanasia wanavyotoa matamko, watu wanaendele kuuwawa hivyo sasa ni vyema waacha vyombo vya ulinzi na usalama vikafanya kazi yake mpaka vitakapoimaliza.

Alivitaka pia vyombo hivyo kutumia mbinu ya kushirikisha wananchi ili kujua mzizi wa suala hilo.

Alisema yeye  kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, amepewa taarifa za baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), kukamatwa na kuteswa ili kusema chanzo cha mauaji hayo.

Alisema ingawa hana uhakaika na wanaokamata viongozi hao, ni vyema kukawa na mbinu ya kushirikisha viongozi wa dini, siasa na wananchi wote ili kumaliza suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles