Na Khamis Mkotya, Dodoma
HATIMAYE makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliofungiwa kujihusisha na shughuli zozote zenye mwelekeo wa kufanya kampeni za kuwania kuteuliwa kuwania urais kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa wapo huru.
Makada hao wameondolewa kifungo hicho baada ya Kamati Kuu ya CCM (CC), kuridhia pendekezo la kamati ndogo ya maadili iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula, la kuwaondoa kifungoni.
Kamati Kuu ya CCM ilianza vikao vyake jana katika jengo la makao makuu ya chama hicho, maarufu kwa jina la ‘White House’, kwa kujadili ajenda mbalimbali zilizowasilishwa na Sekretarieti, ikiwamo Kamati ya Maadili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni katika ukumbi wa jengo hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Nape Nnaye, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya makada hao kumaliza adhabu yao.
Makada waliokuwa kifungoni ni Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wengine ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Nape alisema, wakati wa kujadili ajenda hiyo, Kamati ya Usalama na Maadili chini ya Mangula iliwasilisha pendekezo la kuachiwa kwa makada hao na kukubaliwa na wajumbe wa Kamati Kuu.
Nape alisema baada ya adhabu hiyo kumalizika, hakuna sharti lolote walilopewa, isipokuwa kusoma vizuri kanuni za chama ili kuepuka kurudia makosa ya kukiuka taratibu.
Kauli hiyo ya Nape inafuta uvumi ulioanza kusambaa mapema jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ukielezea kuwa kuondolewa kwa adhabu hiyo kuliambatana na barua za karipio kali.
Hata hivyo, Nape alisema wanachama watakaoendelea kukiuka taratibu, taarifa zao zitatumika katika mchujo wa majina ya kutafuta mgombea wa CCM wakati wa uteuzi.
“Kamati Kuu imepokea na kukubali pendekezo la Kamati ya Usalama na Maadili la kumalizika kwa kipindi cha adhabu kwa wanachama hao, kwa hiyo adhabu hiyo kwa sasa imemalizika na wanachama hao wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao katika chama.
“Hata hivyo, Kamati Kuu inawataka wanachama hao na wale wengine wenye nia ya kugombea kupitia CCM kuzisoma, kuziheshimu na kuzizingatia kanuni za maadili ya CCM na kanuni nyingine zinazoongoza mchakato ndani ya chama, ili wasije kukumbwa na adhabu kutokana na kuzivunja kanuni hizo.
“Hawa waliopewa adhabu na wengine watakaoanza au walioanza kampeni mapema na hivyo kukiuka miiko na maadili ya chama, taarifa za kukiuka kwao zitatumiwa wakati wa kuchuja majina kwa nafasi walizoziomba.
“Taarifa hizo zitatumika kuwapima na kuamua iwapo wana sifa za kutosha na wanafaa au hawafai kuteuliwa kuwania nafasi watakazoomba,” alisema Nape.
Kuondolewa kwa kifungo hicho kilichokuwa kikiwakabili baadhi ya makada wenye nguvu ya ushawishi wa kisiasa ndani ya CCM kunaashiria kuwa katika siku za karibuni mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho atateuliwa.
Dalili za kupatikana kwa mgombea huyo katika siku za karibuni zinapata nguvu hivi sasa kulingana na mwenendo wa kisiasa ndani ya CCM, ambapo makada wake wengi na wafuatiliaji wa siasa za chama hicho wamekuwa wakieleza kuwa mgombea wa chama hicho atatoka miongoni mwa waliokuwa kifungoni.
Mbali na kutangaza kufunguliwa kwa wanasiasa hao, Nape alieleza pia kuwa akidi ya wajumbe wa kikao kilichofikia uamuzi huo ilitimia kwa kuwataja wajumbe waliohudhuria kuwa 29 kati ya 32. Alisema wajumbe wawili hawakuhudhuria kutokana na dharura.
Kukamilika kwa kikao cha Kamati Kuu kunatoa fursa ya kuanza kwa vikao vya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), ambavyo vitafanyika kwa siku mbili kuanzia leo na kesho mjini hapa.
Wakati huo huo, jana Kamati Kuu ilitarajiwa kupokea na kujadili majina ya vijana wasomi wa CCM wanaowania nafasi za uongozi katika Shirikisho la Taifa la Wasomi wa Vyuo vya Elimu ya Juu.
Shirikisho la vyuo
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Katibu Mkuu Mtendaji wa Shirikisho hilo linalojulikana kama Tanzania Higher Learning Students Federation, Christopher Ngubiagai (MNEC), alithibitisha taarifa hizo.
Ngubiagai alisema, jumla ya majina 147 ya wasomi wenye shahada ya juu, shahada na shahada ya uzamili yalitarajiwa kuwasilishwa katika kikao hicho cha jana.
Alisema majina hayo yatachujwa ili kupata watakaokuwa na sifa za kugombea nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu, wajumbe watatu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), katibu wa siasa na uenezi na katibu wa uhamasishaji.
Ngubiagai alisema, Mei 25 mwaka huu utafanyika mkutano mkuu wa kwanza wa shirikisho hilo, utakaozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete kabla ya uchaguzi kufanyika Mei 26, mwaka huu.