29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa avunja ‘ndoa’ ya Zitto, Dk. Slaa

EDWARD NGOYAYE LOWASSANA MWANDISHI WETU DAR ES SALAAM

MKAKATI wa chama cha ACT Wazalendo kumtumia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kutumia jukwaa lake ‘kumchafua’ mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, umegonga mwamba.

Kukwama kwa mkakati huo kunatokana na kuwapo msigano wa mawazo miongoni mwa viongozi wa ACT ambao waliona kumtumia Dk. Slaa kuiponda Chadema na hata Ukawa wataifanya jamii kuamini kwamba wao (ACT) wanaisaidia CCM katika kampeni zake.

Chanzo cha kuaminika ndani ya ACT kimelidokeza MTANZANIA kuwa mpango wa kumkaribisha Dk. Slaa kusimama katika jukwaa lake na kuwasema vibaya viongozi wa Ukawa hususan Lowassa, kungekishushia hadhi chama hicho na kuonekana kinafanya kazi ya CCM.

“Ni kweli mpango huo ulikuwapo lakini baadhi ya viongozi wa ACT wamepima uzito wa kumtumia Dk. Slaa katika kampeni zetu ‘kuwashughulikia’ Ukawa au Chadema kungetuondoa katika mstari wa upinzani na kuitwa ‘CCM B’ kwa sababu tayari jamii inamuona Dk. Slaa kama ni msaliti wa mabadiliko kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.

Hali hiyo inaungwa mkono na taarifa iliyotolewa na ACT Wazalendo Dar es Salaam jana kuhusu kuacha kumtumia Dk Slaa katika kampeni zake kama ilivyotarajiwa, kuwa ni baada ya kufanya tathmini ya kina na kugundua kuwa hali ya usalama kwa kiongozi huyo si nzuri.

Taarifa hiyo ya ACT imetolewa siku moja baada ya gazeti la MTANZANIA Jumapili kuripoti kuwapo mpango wa Dk. Slaa kusimama katika jukwaa la chama hicho kuzungumza kile anachodai kukijua kuhusu tuhuma mbalimbali za viongozi mbalimbali wa Chadema wakati wa kuwapokea baadhi ya waliokuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojiunga na upinzani.

Taarifa kutoka ACT zilisema Dk. Slaa angeungana na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto katika mkutano uliopangwa awali kufanyika mkoani Iringa katika Uwanja wa Mwembetogwa ambako Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chadema aliyetofautina na wenzake kabla ya kutangaza kujitenga nao, angeeleza mambo yaliyofichika kuhusu tuhuma za ufisadi wanazodaiwa kuhusika nazo baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ukawa unaundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Dk. Slaa alitarajiwa kuwatataja kwenye mkutano huo kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Tundu Lissu ambaye ni mwanasheria wa chama hicho, John Mnyika ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa
Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa. Ingawa ACT haikuweka wazi kuhusu mpango huo wa kumtosa Dk. Slaa, lakini taarifa yake ilitoa hoja kwamba usalama wa kiongozi huyo utakuwa mdogo kutokana na
vitisho mbalimbali anavyovipata na kwamba chama hicho hakina uwezo wa kumhakikishia ulinzi.

“Chama chetu kimekuwa na mawasiliano na Dk. Slaa, mwanasiasa nguli wa upinzani nchini kuhusu uwezekano wa yeye kushiriki katika kampeni za chama chetu kwa lengo la kuendeleza vita dhidi ya ufisadi nchini. “Hivyo kutokana na hali hiyo ya vitisho dhidi ya usalama wake, chama chetu kimejiridhisha kuwa hakina uwezo wa kumhakikishia Dk.Slaa usalama wake atakapokuwa jukwaani.

“Kutokana na sababu hizo, ACT kimefuta mikutano yote ya nguli huyo wa siasa nchini ambayo alikuwa aifanye kupitia jukwaa la chama chetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya ACT ilisema inamshukuru Dk. Slaa kwa imani aliyonayo juu ya chama hicho na uamuzi wake wa kuikabidhi rasmi mikoba yake ya vita dhidi ya ufisadi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Slaa aliamini kwamba chama hicho ndicho chama pekee chenye uhalali na uwezo wa kupambana na ufisadi baada ya chama chake cha zamani Chadema kuitelekeza vita hiyo.

“Dk. Slaa alikuwa ashiriki kwa ukamilifu katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea kupitia jukwaa la ACT Wazalendo kwakuanza kwenye mkutano wa hadhara mjini Iringa Jumatano Oktoba 7 mwaka huu.

“Baadaye angeendelea na mikutano mingine katika majimbo mbalimbali na kuhitimisha kampeni hizo katika Viwanja vya Mwembeyanga Dar es Salaam, ambao ndiyo uwanja ambako vita dhidi ya ufisadi ilitangazwa rasmi Septemba 15 mwaka 2007,” ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles