26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA AUNGANA NA MAASKOFU KUOMBA MVUA

Na Mwandishi Wetu -BUKOBA


 

lowassaWAZIRI Mkuu  wa zamani,  Edward Lowassa, ameungana na maaskofu wa Kanisa Katoliki kutaka yafanyike maombi ya kuliepusha Taifa na baa la njaa.

Hiyo ni baada ya kuwapo   ukame wa muda mrefu nchini uliosababisha mazao mengi kukauka.

Lowassa ametoa kauli hiyo  siku moja baada ya maaskofu wa kanisa hilo kupitia Mwenyekiti wa Baraza lao, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa,  kutaka iongezwe kasi ya  maombi kwa kuwa baadhi ya maeneo nchini tayari yana uhaba wa chakula.

Alikuwa akitoa salamu zake katika Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Mjini Bukoba  ambako alikuwa miongoni mwa waumini kanisa hilo waliohudhuria misa ya kwanza.

Lowassa alisema si jambo la siri tena kuwa Taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la njaa.

Aliwashauri viongozi wa dini kwamba maombi ya kuliepusha taifa na baa la njaa  na ukame viwe  miongoni mwa vipaumbele vyao na kuwataka waumni wa madhehebu yote kuungana na viongozi wao kuliombea taifa.

“Nawaomba viongozi wa dini ikiwezekana msimamishe hata mambo mengine na kutoa kipaumbele cha kuliombea taifa letu.

“Wote mnajua hali ya chakula siyo nzuri katika maeneo mengi ya nchi,   sisi hatutachoka kuwasaidia wananchi,’’ alisema Lowassa.

Pamoja na kuwapo matamko mbalimbali ya viongozi wa Serikali yanayokatisha tamaa wananchi, Lowassa alisema   wao hawataacha kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali.

Aliwataka viongozi wa dini kufanya hivyo pia.

Lowassa alikuwa ni mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Alisema yuko Bukoba   kuwapa pole kwa ukame pamoja na  janga la tetemeko ingawa alifika mkoani humo mwaka jana na kuwasilisha mchango wa mifuko 400  ya saruji kwenye kamati ya maafa ya mkoa.

Katika misa hiyo, Lowassa alifuatana  na viongozi mbalimbali akiwamo Mbunge wa Bukoba Mjini,  Wilfred Lwakatare (Chadema).

Baadaye walishiriki vikao vya ndani katika Wilaya ya Bukoba kwa kukutana na viongozi kuanzia ngazi ya matawi.

Pia Lowassa alishiriki kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Kimwani kupitia Chadema,  Leonard Nchimani.

Kata hiyo inafanya uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, Sylvester Muliga (CUF) kuuawa kwa mapanga nyumbani kwake mwaka jana na watu wasiofahamika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles