24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA ATOA NENO MBUNGE MONDULI KUJIUZULU

Na ANDREW MSECHU, DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema hakuna jipya katika hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema) na kwamba ni kawaida kwa wanasiasa duniani kuhama vyama na kubadilishana vijiti.

Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kupitia CCM kwa miaka 25 tangu mwaka 1990 hadi 2015 kisha kuhamia Chadema na nafasi yake kuchukuliwa na Kalanga, alisema jana kuwa hatua hiyo imewapa heshima watu wa Monduli kwenye harakati za mabadiliko, hivyo kuwataka wasife moyo.

“Nimesikia taarifa za kujiuzulu kwa mbunge wangu wa Monduli, Julius Kalanga. Kwa sababu zozote zile atakazokuwa amezitoa, hiyo ni haki yake kikatiba.

“Najua wana Monduli wote nikiwemo mimi uamuzi huo umetuhuzunisha na kutuumiza, lakini nawaomba msife moyo hata dakika moja zaidi, kitendo hicho kizidi kutupa nguvu, ari, hamasa na mori zaidi kuendeleza mapambano ya kuitafuta demokrasia na mabadiliko ya kweli,” alisema katika taarifa yake.

Lowassa ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne na mgombea wa urais kupitia Chadema/Ukawa mwaka 2015, kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu Chadema.

KUJIUZULU KWA KALANGA

Akieleza sababu za kujiuzulu kwake juzi usiku, Kalanga alisema ameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona hapati ushirikiano kwa Serikali katika kuleta maendeleo jimboni.

Alisema ameamua kupoteza ubunge kwa masilahi mapana ya wananchi wa Monduli ili apatikane mbunge ambaye sasa atashirikiana na Serikali kutatua migogoro ya ardhi na matatizo mengine.

Kalanga ambaye kabla kuwa mbunge aliwahi kuwa diwani kupitia CCM, alieleza kuwa aliingia katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 akiwa na uhakika kwamba watashinda na kuwa sehemu ya Serikali.

“Na actually, sichekeshi lakini niwe mkweli, mimi sikujipanga kuwa mpinzani. Niligombea nikitarajia tutachukua nchi, lakini kwa bahati mbaya hatukufanikiwa, kwa hiyo mimi sioni sababu ya kuendelea kuwa sehemu ya upinzani wakati tayari ilani ipo na Serikali ipo, nikaona niungane nao kutekeleza majuku yetu,” alisema.

Alisema sababu nyingine ni kuona siasa za malumbano, uhasama na chuki zilizosababisha wananchi kukosa huduma na haki zao, hivyo ataendelea kuiomba jamii yao ya kimasai ambayo imebaki nyuma kimaendeleo kuungana na Serikali kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili.

Kalanga alisema katika historia ya Monduli, amebaini wabunge wote kuanzia hayati Edward Sokoine hadi Lowassa wamefanya mambo ya msingi yanayoacha alama katika jimbo hilo, lakini wamefanya hivyo wakiwa ndani ya Serikali na yeye kwa kuwa amekuwa mbunge wa kwanza akiwa nje ya Serikali, hawezi kufanya mambo ya msingi kama walivyofanya wao.

“Sasa ili na mimi nikumbukwe kama wao, ni wazi kwamba siwezi kuwa nje ya Serikali, kwa sababu siwezi kutimiza majukumu yangu, kwa hiyo nimepwaya,” alisema.

Alifafanua kwamba amepata ubunge akiwa nje ya serikali kwa hiyo ameshindwa kufanya kazi zake za kibunge ipasavyo, hatua iliyomsukuma kuamua kuachia nafasi hiyo.

Alieleza kwamba ubunge siyo suala la kumsumbua kwa kuwa amewahi kuishi kama mwananchi wa kawaida wa Monduli akiwa mkulima na mfugaji, hivyo anaweza kuendelea kufanya kazi hiyo akiamini kwamba hawezi kuendelea kuwa mbunge huku akiona anakuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi.

“Unapokuwa mbunge unakuwa na majukumu maeneo matatu, kwanza kwa masilahi ya wananchi, taifa lako na masilahi ya chama chako, lakini tunakutana na matatizo katika eneo la chama, kwamba unawezaje kusaidia wananchi wakati mnakuwa na jukumu la kisiasa mnalosimamia nyie kama chama wakati Serikali inatekeleza majukumu yake mengine,” alisema.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles