22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa atikisa ngome ya Zitto

OTH_6079NA MAREGESI PAUL, KIGOMA

MAFURIKO ya mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, jana yalihamia katika Mji wa Kigoma ambako Zitto Kabwe anagombea ubunge kupitia Chama cha ACT- Wazalendo.

Kama ilivyokuwa katika maeneo mengine alikopita mgombea huyo, umati mkubwa ulijitokeza katika mkutano wake wa kampeni za urais uliofanyika katika uwanja wa mikutano wa Mwanga ambao umewashangaza hata wakazi wa eneo hilo waliosema ni aghalabu uwanja huo kujaa.

Akizungumza katika mkutano huo, Lowassa aliwataka Watanzania waliopewa uraia na Serikali, wakatae kuonewa kwa kuwa hakuna kiongozi mwenye haki ya kuwaonea.

Alisema kwa kuwa Watanzania hao wanahesabika kuwa ni Watanzania halisi, wana wajibu wa kuwachagua viongozi wanaowataka kwa kuwa wana sifa za uraia.

 

“Tumepata taarifa kuna watu wanapitapita huko na kuwatisha Watanzania waliopewa uraia kwamba wasipowachagua wagombea wa CCM watawafutia uraia.

“Tumemtuma Masha (Lawrance Masha, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi), alifuatilie suala hili kwa undani.

“Lakini kataeni kuonewa, kataeni kubaguliwa, mtu akiwaletea upuuzi, kataeni kwa sababu hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuwachagulia mtu wa kumpigia kura.

“Serikali haiwezi kumnyang’anya mtu uraia wake, nawaambia msikubali kuonewa, hata mtu akikuita Mkongo, akikuita Mrundi au vinginevyo, usimjali ili mradi tu wewe ni Mtanzania,” alisema Lowassa.

Akizungumzia sekta ya maji, Lowassa aliwataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma wamchague yeye na wagombea wanaotoka katika vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili aweze kuwaletea maji ya uhakika.

Kwa mujibu wa Lowassa, kusambaza maji katika Mkoa wa Kigoma kutoka Ziwa Tanganyika ni kazi rahisi kwa kuwa wakati akiwa madarakani, aliweza kupeleka maji ya Ziwa Viktoria kutoka Mwanza hadi Shinyanga.

“Nipeni kura nyingi za kutoka moyoni ili hata wakiiba bado niendelee kupata kura za ushindi kwa sababu naambiwa hawa wenzetu ni hodari wa kuiba kura.

“Nimesikia hapa Kigoma mna tatizo la maji, sasa kama niliweza kutoa maji katika Ziwa Victoria na kuyapeleka hadi  Shinyanga, mnafikiri haya maji ya Ziwa Tanganyika yaliyoko hapa mlangoni nitashindwa kuyasambaza kwenu?

“Nipeni kura muone, nikiingia madarakani tu nitawasambazia maji na hamtakuwa tena na shida ya maji kama mliyonayo sasa,” alisema Lowassa.

 

SEKTA YA NYUMBA

Akizungumzia sekta ya nyumba, alisema haridhishwi na nyumba za nyasi wanazoishi baadhi ya Watanzania. Kutokana na hali hiyo, alisema kama atafanikiwa kuingia madarakani, itatungwa sera maalumu ya kutokomeza nyumba hizo nchini.

Alisema atalazimika kufanya hivyo ili Tanzania ifanane na nchi nyingine duniani zenye nyumba bora.

RELI NA BANDARI

Kuhusu maeneo hayo, alisema Serikali yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kunakuwa na reli imara tena inayochangia kukuza uchumi wa Taifa.

Alisema atakapoingia madarakani reli isiyo imara iliyoanza kujengwa na Serikali itafumuliwa ili ijengwe imara.

Kuhusu Bandari ya Kigoma ambayo alisema haiendeshwi kibiashara, Serikali yake itaibadilisha na kuiendesha kibiashara.

Pamoja na hayo, mgombea urais huyo alizungumzia uvuvi na kilimo cha mawese ambapo alisema atakapoingia madarakani, ataimarisha sekta hizo mbili kwa kuwa anajua umuhimu wake kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine nchini.

MASHA

Awali akihutubia mkutano huo, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrance Masha, aliungana na Lowassa katika suala la kuwatisha wakimbizi waliopewa uraia wa Tanzania na kusema wakimbizi hao hawana sababu ya kuogopa vitisho.

Pia, alisema tabia ya vyombo vya dola ikiwamo Idara ya Uhamiaji kuwatisha wakimbizi hao, haiwezi kukubalika kwa kuwa Watanzania hao wana haki ya kuwachagua viongozi wanaowataka na kuwakataa wagombea wa CCM.

“Nyie watu wa uhamiaji huu siyo wakati wa kuwatisha wananchi kwa kisingizio kwamba mtawanyang’anya uraia wa Tanzania kama hawatawachagua wagombea wa CCM.

“Watanzania wote wana haki ya kuwapigia kura wagombea wanaowataka, msiwatishe hata kidogo kwa sababu wakati wa uchaguzi siyo wakati wa kutishana.

“Majeshi yote yafanye kazi kwa kufuata sheria kwani Serikali ya Ukawa itakapoingia madarakani, itawajali watumishi wote ikiwa ni pamoja na kuwalipa malimbikizo yote wanayodai,” alisema Masha.

 

KAFULILA

Kwa upande wake, mgombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema Lowassa ndiye rais anayefaa kuiongoza Tanzania kwa kuwa ana uwezo wa kutosha.

Alisema kwamba, kashfa ya Richmond ambayo amekuwa akihusishwa nayo, haina msingi wowote kwa kuwa ameshasema inamhusu Rais Jakaya Kikwete.

“Lowassa ameshasema Richmond ni ya Kikwete lakini nawaambia pia kwamba Kigoma ni ngome ya upinzani na CCM imeshakataliwa misikitini na kanisani.

“Serikali ya Kikwete imebaki kuwa Serikali ya porojo ila Serikali ya Lowassa ndiyo itakayoweza kutatua kero zote ikiwamo ya maji kwa kuwa ataleta maji Kigoma kutoka Mto Malagarasi.

“Nawaambia upinzani wa uhakika dhidi ya CCM uko Ukawa na hakuna chama kinachoweza kuiondoa CCM madarakani bila kupitia Ukawa.

“Ukiwa mpinzani nje ya Ukawa wewe ni mradi wa CCM, hapa Kigoma tukitaka chama cha upinzani tuanzishe chama cha michikichi na siyo chama cha upinzani.

“Kwa hiyo mchagueni Lowassa, wachagueni wagombea wa Ukawa kwa sababu hawa ndiyo wapinzani wa kweli,” alisema Kafulila.

Pamoja na hayo, leo Lowassa na viongozi wa Ukawa, watahutubia mikutano mbalimbali katika Mkoa wa Tabora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles