24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA APIGWA KALENDA POLISI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameripoti tena Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam jana, kutokana na madai ya kutoa kauli za uchochezi.

Lowassa aliwasili polisi jana saa 3:05 asubuhi akiwa ameongozana na wakili wake Peter Kibatala, ambapo walikaa kwa muda mfupi na kutoka saa 3:35 asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuripoti, Kibatala alisema hakuna mahojiano yaliyofanyika na kwamba mteja wake ameelekezwa kurudi tena polisi Alhamisi ijayo.

“Lowassa ameripoti leo (jana) kama alivyolekezwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na ameambiwa arudi tena Alhamisi ijayo ambapo tutapata maelekezo zaidi,” alisema Kibatala.

Kwa mara ya kwanza Lowassa aliripoti Juni 27 mwaka huu kwa amri ya jeshi hilo ambapo alihojiwa kwa saa nne kisha kuachiwa kwa dhamana.

Aidha, Juni 29 aliripoti kwa mara ya pili na kuelezwa kuwa upelelezi bado unaendelea na kutakiwa kurudi tena jana.

Lowassa anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi wakati wa futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara mwezi uliopita.

Kwa mara ya kwanza kuripoti polisi, Lowassa alihojiwa kuhusiana na matamshi aliyoyatoa wakati wa futari hiyo na kuchukuliwa maelezo yake ya onyo.

Katika futari hiyo Lowassa alinukuliwa akisema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru kwa zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (Jumiki) bila kesi yao kusikilizwa.

Hali ya usalama jana ilikuwa ya kawaida kabla na baada ya Lowassa kuwasili katika Makao Makuu ya Polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles