WAZIRI Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amepandisha joto la homa ya kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Joto hilo amelipandisha jana huku jina lake likitajwa zaidi wiki hii bungeni na baadhi ya mahasimu wake kisiasa na wabunge wengine waliotaka asafishwe kutokana na kutuhumiwa katika kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond.
Wakati jana watu walitarajia Lowassa angetoa kauli kuhusu mambo ya urais baada ya kutumwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kumwakilisha katika harambee mkoani Arusha, lakini hakufanya hivyo na badala yake alisema Mei 24, mwaka huu anatarajia kutoa neno katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid vilivyopo Mjini Arusha.
Akizungumza mjini hapa jana akiwa Viwanja vya Msikiti Mkuu wa Ijumaa Bondeni wakati alipoongoza harambee ya ujenzi wa shule ya sekondari, Kituo cha Kiislamu na Msikiti wa Patandi uliopo wilayani Arumeru mkoani hapa, aliwaomba wananchi ifikapo tarehe hiyo wajitokeze kwa wingi kumsindikiza uwanjani hapo.
“Mei 24, mwaka huu naomba mniunge mkono pale viwanja vya Sheikh Amri Abeid ambako nitakuja kusema neno.
“Leo nisimalize uhondo ila naomba siku hiyo mjitokeze kwa wingi, mkiulizwa semeni mnakuja kuniunga mkono katika safari yangu ya matumaini,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na maelfu ya watu waliohudhuria harambee hiyo.
Katika harambee hiyo, Lowassa aliwasili jijini hapa kwa ndege kupitia uwanja mdogo wa Arusha akitokea bungeni mjini Dodoma na kulakiwa na msafara mrefu wa magari na pikipiki.
Katika harambee hiyo aliyoongozana na Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, zaidi ya Sh milioni 240 zilichangwa huku yeye, Dk. Bilal na viongozi wengine walichangia Sh milioni 105 wakati malengo ya mradi husika yakiwa ni Sh milioni 200.
Akizungumza kwa niaba ya Dk. Bilal, Lowassa aliipongeza Kamati ya Amani mkoani hapa inayoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu kwa kuendeleza mshikamano wa dhati katika kusimamia amani na utulivu.
Alisema Arusha ni kitovu cha utalii wa nchi na ni jiji lenye mwingiliano wa wageni wengi wanaokwenda kwa ajili ya kutalii katika hifadhi mbalimbali hivyo ni muhimu utulivu na amani vikaendelea kulindwa kwa ushirikiano wa watu wote.
“Jiji la Arusha ni kioo cha utalii hapa nchini kwetu, wageni wamekuwa wakiwasili mamia kwa maelfu kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali hivyo kama kutakuwa na vurugu wageni watashindwa kuja Arusha.
“Niombe wakazi wa Jiji la Arusha kuilinda amani kwa gharama yoyote, mshikamane bila ya kujali dini, kabila wala rangi kwa kuwa misingi tuliyonayo ni kila mmoja anapaswa kumheshimu mwenzake kwa kila namna,” alisema Lowassa.
Akisisitiza suala la amani, aliiomba Kamati ya Amani inayoongozwa na Askofu Lebulu kutochoka katika kazi ya kuelimisha wananchi wa Jiji la Arusha na mkoa kwa ujumla wake kuhusu umuhimu wa mshikamano na kutunza amani iliyopo kwa dini na makabila yote.
“Niiombe kamati hii ya viongozi wa dini hapa mkoani Arusha isimamie amani na kumkemea atakayekuwa na nia au kutaka kuleta chokochoko za kuhatarisha amani na utulivu,” alisema Lowassa kwa niaba ya Dk. Bilal.
Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaaban Juma, alisema malengo ya harambee hiyo ilikuwa ni kukusanya Sh milioni 200 kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari itakayojengwa Patandi, Tengeru wilayani Arumeru mkoani hapa.
Alisema sekondari hiyo itakayokuwa chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), itapokea wanafunzi kutoka dini zote na itakuwa ndani ya kituo cha watoto yatima.
Lowassa ambaye ni miongoni mwa makada sita wa CCM waliofungiwa na chama hicho kutokana na kile kilichodaiwa kufanya kampeni mapema ya kutaka kuwania urais ndani ya chama hicho, alisema hivyo katika harambee hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya baadhi ya mahasimu wake kutaka naye asafishwe kutokana na kashfa ya Richmond iliyogharimu uwaziri wake mkuu kama Ikulu ilivyowasafisha viongozi wengine waliotuhumiwa katika kashfa ya uchotwaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow na Operesheni Tokomeza.
Mmoja wa hasimu wake ni Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, aliyeungana na baadhi ya wabunge wengine wa CCM kumsifia Lowassa kutokana na utendaji wake.
Akizungumza bungeni jana, Sendeka alimsifia Lowassa akisema ni kiongozi mchapakazi na kueleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne hayawezi kutajwa bila mchango wake.
Sendeka alitoa kauli hiyo wakati akichangia Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoiwasilisha bungeni mwanzoni mwa wiki hii akiomba Sh trilioni tano kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Uhasama wa Sendeka uliibuka mwaka 2008 wakati wa kujadili Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyowasilishwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe, kuhusu kashfa ya Richmond baada ya kuwa miongoni mwa wabunge waliomtaka Lowassa awajibike kisiasa.
“Nitakuwa mwizi wa fadhila, kwamba unapozungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne, usipolitaja jina la Lowassa utakuwa hujatenda haki.
“Hakuna asiyekubali labda awe mwizi wa fadhila, kwamba kazi aliyoifanya Lowassa kwa miaka miwili ni ya kiwango cha kupigiwa mfano na kwa maana hiyo na yeye ni sehemu ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne ambayo wengine hawataki kuyaona,” alisema Sendeka.
Naye Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli aliyekuwa hasimu wake, alisema wakati Serikali ikiwasafisha baadhi ya watendaji, haoni jitihada kama hizo za kumsafisha Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu kutokana na kashfa ya Richmond.
Akizungumza bungeni juzi wakati akichangia hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Pinda, Lembeli, alishangazwa na taarifa ya Ikulu iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na kuwasafisha baadhi ya viongozi kwa kusema hatua hiyo haitoi taswira ya usawa.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mary Chatanda, alikuwa ni hasimu wa Lowassa lakini kwa sasa inadaiwa anamuunga mkono.
Pia Serukamba akichangia bungeni juzi, alikosoa hatua ya ripoti ya Ikulu ya kuwasafisha baadhi ya watuhumiwa wa Escrow na kuwaacha wengine.
Serukamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, alishangazwa na taarifa hiyo na kusema ili kutenda haki ni vema Serikali ikawasafisha watuhumiwa wote akiwamo Lowassa.