29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa afunguka waliomtabiria kifo

 Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

 Na Waandishi Wetu-MBINGA/DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewashukuru wananchi kwa kumpigia kura kwa wingi licha ya baadhi kumsema vibaya kwa kumwita mgonjwa na kwamba angekufa.

Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa kauli hiyo mjini Mbinga mkoani Ruvuma ambako chama hicho kipo katika ziara ya kufanya mikutano ya ndani.

Akizungumza ndani ya vikao hivyo, Lowassa pasipo kutaja jina la mtu yeyote alisema: “Mwacheni Mungu aitwe Mungu, kwa sababu wote hata walionisema mabaya baadhi yao wameshatangulia mbele ya haki.”

Alisema kitendo cha wananchi kumpigia kura kwa wingi pamoja na kwamba alikuwa akizungumziwa vibaya juu ya afya yake, ni wazi kuwa walikubali kubeba lawama juu yake.

“Bila ujasiri na umoja wa dhati, hawa jamaa wataendelea kutupiku… lakini niwashukuru vile vile kwa kukubali kubeba lawama juu yangu, wapo waliosema huyu ni mgonjwa atakufa, bado mlinipigia kura nyingi ila Mungu ndiye hupanga yote,” alisema.

Pamoja na hayo, Lowassa aliwataka wanachama wa Chadema kuendelea kuwa na ujasiri na kudumisha umoja kwa kuendelea kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka 2020.

Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa kuzungumza juu ya watu ambao walihoji kuhusu mwenendo wa afya yake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Baadhi ya wanasiasa, hususani wale waliokuwa wakimpinga, walijaribu kuionyesha na hata kuiaminisha jamii kwamba mwanasiasa huyo ni mgonjwa na hafai kuongoza nchi.

Wapo ambao walidiriki kusema kwamba Ikulu si hospitali na wala hakuna gari la kubebea wagonjwa.

Miongoni mwa wapinzani wake ni baadhi ya wanasiasa wakubwa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwamo viongozi waliosikika katika majukwaa ya kampeni  mwaka jana wakiwashawishi wananchi kutomchagua Lowassa kwakuwa hata akipata urais hatotawala muda mrefu atakufa.

Wapo waliokwenda mbali na kusikika wakimwambia Lowassa Ikulu si wodi ya wagonjwa, hivyo hafai kupatiwa nafasi ya urais kulingana na afya aliyonayo.

Mikutano ambayo Lowassa ameitumia kuzungumzia suala hilo, inafanyika nchi nzima pamoja na kuwahusisha wajumbe wa ngazi mbalimbali za chama.

Uwepo wa Lowassa katika mikutano hiyo imesababisha watu wengi kukusanyika wakitaka kumuona.

Hata Lowassa anapokuwa anaondoka katika eneo hilo kuelekea mahali kupumzika, wananchi wamekuwa wakiunga msafara kwa kumfuata nyuma.

Mikutano hiyo inatajwa kuwa sehemu ya operesheni ya siku 40 inayofanyika nchi nzima iliyopewa jina la ‘Amsha Amsha’.

Mwanzoni mwa wiki hii, gazeti hili liliandika taarifa kuhusu operesheni hiyo likimnukuu mmoja wa mofisa wa ngazi za juu wa chama hicho, akisema viongozi wa Kamati Kuu na wabunge wote wa Chadema watakutana mkoani Morogoro kupanga mikakati.

Katika kikao hicho ambacho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, viongozi waligawana maeneo ya kufanya kazi kikanda ili kuweza kufanikisha mikutano hiyo ambayo imelenga kujijenga kwa kuwafikia wananchi wa kada ya chini nchi nzima.

Hatua hii imekuja baada ya miezi kadhaa tangu chama hicho kutangaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima – Operesheni Ukuta, ambayo ilisababisha Jeshi la Polisi kuipiga marufuku.

Operesheni hiyo iliyotarajiwa kufanyika Septemba mosi, mwaka huu, ambayo pamoja na mambo mengine ililenga kuishtaki Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kwa wananchi kutokana na aina ya uongozi wake, iliibua mvutano mkali kati ya Chadema na Jeshi la Polisi.

Jeshi hilo lilitoa onyo kali kwa mtu yeyote ambaye angeandamana, huku kwa mara ya kwanza Watanzania wakishuhudia askari kila mkoa wakifanya mazoezi makali mitaani.

Baada ya mvutano huo, na kile alichokiita mwenyewe kuwa wito wa viongozi wa dini, Mbowe alitangaza kuahirisha operesheni hiyo hadi Oktoba mosi, mwaka huu, kutoa nafasi kwa Rais Magufuli kufanya mazungumzo na viongozi wa dini kwa upatanisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles