24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

“Lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi”-Dk. Ndumbaro

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Jukwa la Wahariri Tanzania(TEF) na Wadau wa Habari nchini wamehimizwa kupambana kwa hali na mali kubadili sheria za habari nchini.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Dams Ndumbaro alipokutana na uongozi wa TEF na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) jijini Arusha ambapo amesema, kama kuna wakati mzuri wa kulisukuma suala la kubadili sheria za habari ni sasa.

“Rais tuliyenaye sasa, Mheshimiwa Samia (Suluhu Hassan) ameonesha moyo na nia kubwa ya kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini. Kwa sasa mazingira ni mazuri na yanaruhusu.

“Lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi, maana mkisubiri miaka 10 ijayo, huwezi kujua atakayekuja baada ya hapo atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari,” amesema Dk. Ndumbaro.

Aidha, Dk. Ndumbaro amekiri hoja ya TEF na wadau kuwa suala la Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) nchini kuwa na mamlaka ya kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, mtoa hukumu na msimamizi wa hukumu aliyoipitisha linafifisha misingi ya utawala bora na utawala wa sheria hivyo hili ni moja ya mambo yanayopaswa kubadilishwa.

“Hili la dispute settlement (utatuzi wa migogoro), linahitaji uwazi mkubwa. Kuna hatari kubwa katika kuweka madaraka yote kwenye chombo kimoja (Mkurugenzi wa Idara ya Habari/MAELEZO…) nafahamu sheria ililenga ku-balance conflicting interests (kuweka mlinganyo kwa masilahi yanayogongana), maana serikali zote duniani huwa zinawaza kudhibiti.

“Serikali yoyote duniani ina wivu sana na mamlaka yake. Kitendo cha kugawa sehemu ya mamlaka yake huwa hakipendwi, ila kutenganisha mamlaka ndiyo utawala bora,” amesema Dk. Ndumbaro.

Amesema nia ya kusimamia na kuhakikisha haki inatendeka, ndiyo maana kilianzishwa chombo kama Mahakama ambayo ina jukumu la kusikiliza kila upande wenye malalamiko na kuamua nani anastahili haki ipi, hivyo akasema mamlaka ya kufungia chombo vya habari hayapaswi kuwekwa kwenye mikono ya mtu mmoja.

“Ni vyema likawapo Baraza la Usuluhishi. Fair Competition (ushindani wa haki) hazitegemei mtu mmoja. Kunakuwapo na jopo linalofanya uamuzi. Tuunde vyombo na tuhakikishe sheria hizi tunatengeneza mfumo utakaodumu miaka mingi,” amesema na kurejea mfano wa Serikali ya Marekani iliyotoka kulifungia gazeti la Washington Post miaka ya 1970 kwa kuchapisha nyaraka zilizoonyesha kuwa Serikali ya Marekani haikufuata utaratibu katika kuingia vitani na Vietnam, ila Mahakama ilipopitia ushahidi wa pande zote mbili, ililiruhusu gazeti hilo liendelee kuchapisha taarifa hizo.

Amesema, imethibitika kuwa baadhi ya nchi duniani hutumia mwavuli wa kudai kuwa wanazuia baadhi ya taarifa kwa sababu za usalama wa taifa, lakini taarifa nyingi huwa zinazuiwa kukinga maovu ya watu binafsi yasifahamike suala lisilohusiana na usalama wa taifa, akasisitiza:

“Ni kweli masuala yanayohusu usalama wa taifa lazima yalindwe, lakini si kulinda maovu ya watu binafsi yakafichwa kwenye mwavuli wa usalama wa taifa… tunapaswa kutunga sheria zetu zenye viwango na zitakazodumu kwa muda mrefu. Wakati ni huu,” amesema Dk. Ndumbalo.


- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles