28.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 3, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu, Zitto kifungoni

mtz1

*Wapo Mdee, Lema, Bulaya na Heche

*Kamati ya Mkuchika yawatia hatiani

 

Na Khamis Mkotya, Dodoma

BUNGE limewasimamisha kuhudhuria vikao vyake wabunge sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), baada ya kukutwa na makosa ya kudharau kiti na kufanya fujo bungeni.

Uamuzi huo wa Bunge umekuja baada ya kuridhia mapendekezo ya adhabu yaliyotolewa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, iliyowahoji wabunge hao kutokana na kufanya vurugu katika mkutano wa pili wa Bunge wa Januari 27, 2016 kuhusu matangazo ya Bunge ‘Live’.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya wote kutoka Chadema, wamesimamishwa kutohudhuria vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge vilivyobaki kuanzia Mei 30, 2016 pamoja na vikao vyote vya mkutano wa nne wa Bunge la 11 (sawa na mwezi mmoja na siku 15).

“Hawa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika na pia walihusika kwa kiasi kikubwa kuchochea vurugu zilizotokea siku ya tarehe 27 Januari, 2016,” alisema.

Wengine waliosimamishwa ni Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Halima Mdee (Kawe) wote kutoka Chadema.

Wabunge hao pamoja na Zitto, wamesimamishwa kutohudhuria vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge vilivyosalia kwa mwezi mmoja kuanzia Mei 30, 2016 kwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyosababisha kuvurugika kwa shughuli za Bunge.

Mwingine aliyekumbana na rungu hilo ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), ambaye amesimamishwa kutohudhuria vikao kumi mfululizo vya mkutano wa tatu wa Bunge hili kuanzia Mei 30, mwaka huu, baada ya kupatikana na kosa moja.

Akiwasilisha taarifa bungeni jana jioni, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika, alisema wabunge hao wametiwa hatiani baada ya kuhojiwa na kamati yake kutokana na makosa yao waliyofanya.

“Ni matarajio yangu kuwa wabunge wataipokea na kwa kauli moja wataikubali hoja iliyo mbele yetu ya matokeo ya taarifa ya kamati hii ya uchunguzi wa vitendo vya baadhi ya wabunge waliohusika kufanya vurugu bungeni.

“Na kudharau mamlaka ya Spika tarehe 27, Januari, 2016 ili kuimarisha nidhamu ndani ya Bunge letu tukufu na kuhakikisha kuwa kanuni za majadiliano bungeni zinaheshimiwa na kuzingatiwa na wabunge wote.

“Sheria na kanuni hizo zimeweka masharti kuhusu utaratibu unaotakiwa kufuatwa katika majadiliano bungeni na kwamba katika majadiliano, wabunge wanapaswa kuheshimu na kutii mamlaka ya Spika.

“Siku ya Januari 27, 2016 baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani bungeni walifanya vurugu na kudharau mamlaka ya Spika,” alisema.

Mkuchika aliendelea kusema kuwa Spika alipeleka suala la baadhi ya wabunge hao waliofanya vurugu na kudharau mamlaka ya Spika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kutaja majina manne ya wabunge hao.

“Spika aliwasilisha majina mengine matatu siku ya Mchi 10, 2016 ili kamati iweze kufanya uchunguzi kuhusu ushiriki wao katika vurugu zilizotokea Januari 27, ambao ni Zitto, Heche na Mdee.

“Wabunge wafuatao wamevunja masharti ya kifungu cha 24 (c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika,” alisema.

Mkuchika aliwataja wabunge waliokutwa na makosa hayo kuwa ni Lissu, Mdee, Gekul na Bulaya.

Kwa upande wake Zitto ameonekana kuwa alivunja masharti ya kifungu cha 24 (c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika.

 

CHIMBUKO LA SHAURI

Akizungumzia chimbuko la shauri hilo, Mkuchika ambaye pia ni Mbunge wa Newala alisema: “Januari 27, 2016 katika mkutano wa pili wa Bunge, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitoa kauli kuhusu uamuzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kusitisha kurusha matangazo ya moja kwa moja ‘Live’ ya Bunge na badala yake alieleza kuwa vipindi hivyo vitaonyeshwa katika kipindi maalumu kinachoitwa ‘Leo katika Bunge’.

“Baada ya waziri kutoa kauli hiyo, Mh Zitto Kabwe (mb) alitoa hoja ya kuahirisha mjadala kupitia kanuni ya 69. Katika kujenga hoja yake Zitto alimtaka mwenyekiti kusitisha mjadala wa kujadili hotuba ya rais ya kulizindua Bunge ili kujadili kauli ya waziri kwa kuwa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya TBC ni kuwazuia wananchi kufuatilia hoja za wabunge na kuwanyima wananchi haki ya kupata taarifa,” alisema.

Baada ya hoja hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alitoa mwongozo wa kiti kuhusu hoja ya Zitto akisema. “Kwa maana hiyo sasa nachukua uamuzi kwamba kuahirisha mjadala ulio mbele yetu wa hotuba ya rais hautakuwa uendeshaji bora wa shughuli za Bunge (makofi). Naagiza meza tuendelee.”

“Baada ya mwongozo huo wa Mwenyekiti, baadhi ya wabunge waliendelea kusimama na kuomba mwongozo katika jambo ambalo lilikwishaamuliwa.

“Wabunge waliendelea kuwasha vipaza sauti na kuzungumza bila utaratibu, jambo lililopelekea mwenyekiti kuahirisha kikao cha asubuhi ili kutoa nafasi kwa Kamati ya Uongozi kushauri namna ya kushughulikia suala husika,” alisema Mkuchika.

 

KUPOKEWA KWA MAANDAMANO

Kwa upande wao, Chama cha ACT-Wazalendo kupitia kwa ofisa habari wake, Abdallah Khamis, kimeelezea kusikitishwa na kitendo cha ugandamizaji wa demokrasia  uliofanywa na wabunge wa CCM wa kuwasimamisha  ubunge wabunge wa upinzani, akiwemo kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Alisema chama hicho kinaandaa mapokezi makubwa jijini Dar es Salaam kuwapokea mashujaa hao wa wananchi na kwamba ikibidi watafanya mkutano wa pamoja kuelezea udhaifu wa bunge la kumi na moja kila linapoongozwa na Naibu Spika.

Ameongeza kuwa kwa namna moja uamuzi huo wa wabunge wa CCM kwa kutumia kiti cha Spika kuwafukuza wabunge wa upinzani waliojitoa kusimamia masilahi ya wananchi unapaswa kupingwa na kila mpenda demokrasia, na kwamba wabunge hao ni mashujaa kwa kuwa wamekataa kuwa sehemu ya wagonga mihuri wa kupitisha mambo maovu ya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles