30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

LISSU, WASONGA NUSURA WAZICHAPE MAHAKAMANI

Na SARAH MOSES-DODOMA


HATIMA ya kesi ya kupingwa kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) inatarajiwa kujulikana leo, huku mgombea urais wa chama hicho, Tundu Lissu nusura azichape kavukavu mahakamani na Wakili Godfrey Wasonga.

Kesi hiyo ambayo jana iliibua mvutano mkali kisheria Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, baada ya mawakili walioomba kuingizwa katika kesi ya kupinga uchaguzi wa TLS kuita shauri hilo ni sawa na takataka ‘rubbish’ .

Baada ya Jaji Awadhi Mohamed kuahirisha shauri hilo, nje ya mahakama mawakili hao walitaka kuzichapa kavukavu hali iliyowafanya watu waliokuwapo kulazimika kuwaamua kwa kuwasihi.

Kabla ya kesi hiyo kuanza mahakamani hapo Lissu alikuwa akizungumzia kesi zilizopita ambazo waliwahi kukutana na Wasonga na kudai kuwa kila akikutana naye huwa anashinda kutokana na kuijua sheria na kumponda Wasonga kwamba hajui sheria.

 

Kutokana na kauli hiyo ya Lissu ilimfanya Wakili Wasonga kujibu mapigo kwa kumtaka mbunge huyo wa Singida Mashariki, kukumbuka alichomfanyia kwenye kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Wasonga hakuishia kwenye kurushiana maneno mahakamani hapo na badala yake alikuwa akimfuta Lissu ili waweze kuzichapa hali iliyowafanya mawakili waliokuwapo mahakamani hapo kuwasihi wasiendelee kulumbamba kwani ni jambo la aibu kwao.

“Umesahau nilichokufanyia Singida", alisema Wasonga huku akimfuata Lissu alipokuwa amesimama.

Kutokana na hali hiyo mawakili wenzao akiwemo Deus Nyabili,  alimsihi Wasonga na kumwambia aache kwa kuwa si vyema mawakili kulumbana nje ya mahakama.

Hata walipoingia ndani ya mahakama hiyo,  Lissu alisema shauri hilo la Wasonga ni sawa na takataka kwa sababu ombi alilowasilisha halina tija yeyote na amekosea kimaandishi kulingana na sheria inavyoelekeza.

Mvutano huo uliibuka baada ya Jaji Awadhi Mohamed, anayesikiliza shauri hilo kuwapa muda wa dakika 15 wa kwenda kujadili ombi la Wakili Wasonga la kutaka kuondoa shauri hilo ili aweze kuwasilisha jingine mahakamani hapo.

Hata hivyo Jaji Awadhi kabla ya kuendelea kusoma shauri hilo, aliomba muda wa kwenda kupitia barua iliyowasilishwa na Wakili Wasonga, kutokana na kwamba amekutana nayo mahakamani hapo.

“Naomba niwape muda wa kwenda kupitia ombi la Wakili Wasonga la kutaka kuondoa shauri hilo, nami pia nikalipitie kwa sababu nimekutana na barua mahakamani hapa na baadaye tutarejea kwa ajili ya kuendelea kusikiliza shauri hili,” alisema Jaji Awadhi.

Wakati wakiwa katika mapumziko hayo, Lissu alisema shauri hilo limekosewa kwa kuwa sheria inaelekeza anapowasilisha maombi alipaswa aoneshe kuwa anapinga wao kuingizwa katika kesi hiyo lakini yeye aliweka sheria ambayo inawaruhusu kujumuishwa kwenye kesi hiyo.

“Tunamshangaa huyu Wasonga kwanini analeta shauri la kuondoa wakati sheria anaijua hivyo anaidharau mahakama na kuleta usumbufu, kwanini alete ombi ambalo limekosewa,” alisema Lissu.

Alisema amesikia tetesi kuwa anatakiwa akamatwe ili uchaguzi wa TLS ufanyike akiwa rumande na kwamba haogopi hata akiwa rumande atashinda tu kwa kuwa hakuna sheria inayomzuia asigombee nafasi hiyo hata akiwa ndani.

Naye, Wakili Simba Ngwilima ambaye anawania nafasi ya Makamu wa Rais TLS alisema kitendo cha Wakili Wasonga cha kuondoa shauri ili alete jingine ni jambo ambalo halikubaliki kwa sababu watu tayari wanafanya kampeni lakini anashangaa ni kitu gani kinamfanya aweke pingamizi la uchaguzi wakati na yeye ni miongoni mwa wagombea.

Waliporejea mahakamani baada ya mapumziko, Jaji Awadhi aliwaita mawakili wa TLS, Mwanasheria wa Serikali na mawakili walioomba kuingizwa katika kesi hiyo kabla ya kuingia mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na shauri la kesi hiyo.

Ilipofika majira ya Saa 11.40 asubuhi mahakama ilirejea, Wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo alisema maombi yaliyoletwa hayana tija yeyote wala ombi la Lissu na wenzake nalo halina tija na kwamba kwa nini wasingeomba waingie TLS kwa kuwa wao ni wanachama.

Hata hivyo mahakama ililazimika kupumzika tena na kurejea mchana majira ya saa 8.15 ambapo Mwipopo alisema kutokana na hali hiyo Wasonga anatakiwa kutoa gharama za usumbufu kwa mawakili walioshiriki kwenye kesi hiyo.

Kwa upande wa TLS ambayo ilikuwa ikiwakilishwa na Wakili Elias Machibya, Mary Munisi na Deus Nyabili walimshangaa Wasonga kwa kutaka kuondoa shauri hilo kwani alipowasilisha maombi hakujua kwamba amekosea na kwamba kutokana na usumbufu wa kuwasilisha ombi na kutaka kuliondoa wao hawaoni tatizo lakini anapaswa kulipa gharama za usumbufu.

Wakili Machibya alisema maombi ya kisheria hayawezi kurejeshwa kwa sababu aliyewasilisha anaijua sheria na kwamba hatua hiyo ni kuidharau mahakama na kama amekosea alipaswa kuliondoa na si kuomba kurejesha na kwamba inawezekana anataka kuvuruga uchaguzi.

Kwa upande wake, Wakili Wasonga alisema yeye amewasilisha ombi la kuondoa shauri na kuwasilisha jingine hivyo anachosubiri ni uamuzi utolewe ili kama shauri likitolewa aweze kuwasilisha jingine na hata kata tamaa kwasababu anachosimamia ni cha msingi kwake na kwa jamii.

Nayo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam inatarajia kutoa uamuzi wa kuyasikiliza ama kuyatupa maombi hayo leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles