Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
SIKU chache baada ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee (Kawe) na Esther Bulaya (Bunda) kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa mwaka mmoja, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, amesema watakwenda mahakamani.
Mdee na Bulaya walikumbana na kifungo hicho mwanzoni mwa wiki baada ya kukutwa na kosa la kudharau mamlaka ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kutokana na hukumu hiyo, Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema, ameliambia MTANZANIA jana kwamba ana mpango wa kukutana na wabunge hao kuandaa hoja ya kupeleka Mahakama Kuu.
Alisema kusudio la kupeleka Mahakama Kuu hoja ya utetezi wa wabunge hao, ni kupata tafsiri ya uamuzi aliouchukua Spika Ndugai na kwamba utaratibu huo hawatakubaliana nao kwa vyovyote vile.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema uamuzi aliouchukua Spika Ndugai wa kufungia wabunge hao kuhudhuria vikao kwa miezi kumi, ni makosa makubwa.
“Tunataka mahakama ituambie kwenye ‘judicial review’ je, Bunge linaweza kufuta ubunge wa mbunge wake, kama wanavyotafsiri hawa kina Ndugai? Je, Bunge linaweza likatoa adhabu hata nje ya adhabu iliyopo kwenye kanuni? Je, Bunge lina uwezo wa kumwadhibu mbunge bila kumpa fursa ya kujitetea kwenye kamati na Bunge lenyewe.
“Tutaomba Mahakama Kuu itupe tafsiri, kwa vyovyote vile utaratibu huu hatutakubaliana nao, tukienda hivi, hawa CCM wa bungeni kuna siku wataamua mbunge asiingie bungeni kwa miaka mitano halafu wanasema Bunge lina mamlaka lisiingiliwe, Bunge halina mamlaka hayo.
“Kuna kanuni za kutoa adhabu kwa mbunge yeyote anayefanya kosa. Adhabu ya kumfungia mbunge kwa miezi 10 haipo kwenye Kanuni za Bunge la Tanzania, lakini kumekuwa na tabia na utamaduni, sasa inapofika kwa wabunge wa upinzani wanapewa adhabu kubwa kubwa ambazo ziko nje kabisa za utaratibu wa kanuni zilizopo,” alisema.
Alisema sheria na kanuni za Bunge imesema adhabu ya mbunge ni kumfungia vikao 20 kwa maana ya siku na kwamba adhabu nyinginezo haiwezi ikawa kifungo cha siku 100 au miezi kumi.
Alisema tafsiri nyinginezo si kuzuia tena kuhudhuria vikao kwa siku 20, bali inaweza ikawa kumnyima mbunge huyo mshahara, kuzuia bima yake ya afya, kumfutia posho ya jimbo.
“Sasa Bunge la Ndugai wanaelekea kufikiria kwamba Bunge lina uwezo wa kumsimamisha mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kipindi chochote kile watakachoamua wao. Hiyo tafsiri ni ya makosa kabisa ya mamlaka ya kutoa adhabu ya Bunge." alisema.