LISSU: JK ANAPONAJE KWENYE HILI?

0
660
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema)

 

Na RAMADHAN HASSAN – Dodoma

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), jana aliibuka bungeni na kusema Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, hawezi  kupona kwenye sakata la mchanga wa madini wakati yeye ndiye mtu wa kwanza kusaini mikataba mikubwa ya madini nchini ambayo inapigiwa kelele leo.

Akichangia jana jioni kwenye bajeti Kuu ya Serikali, Lissu alisema kamati ya pili iliyomkabidhi Rais Dk. John Magufuli ripoti yake juzi, imewagusa baadhi ya mawaziri, wanasheria na makamishna wa madini huku ikimwacha Kikwete.

“Mtu wa kwanza kusaini mikataba na leseni za madini  tarehe 5 mwezi Agosti mwaka 1994 ni Meja Jakaya Mrisho Kikwete, leseni ya Bulyanhulu  hii inayopigiwa kelele leo, ilisainiwa na Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini.

“Hakuwa na kinga ya urais wakati ule kama aliyonayo leo. Kuhusiana na masuala aliyoyafanya wakati hajawa Rais na alisaini leseni, sio ya Bulyanhulu peke yake, ya Nzega na Geita, hizo leseni zina saini ya Kikwete, anaponaje?

“Kwa mapendekezo haya anaponaje? Kama mnataka kweli kushughulikia watu wanaoshiriki mambo haya, mbona mnachagua chagua?

“Hizi leseni na hizi sheria tatizo kubwa ni sheria za Tanzania tangu mwaka 1999, wenye kujua tumesema tatizo kubwa ni sheria za Tanzania, sisi ni wanachama wa mkataba wa kimataifa wa kulinda wawekezaji, sisi tumesaini mikataba na nchi moja moja zenye wawekezaji Tanzania, nchi 26 mikataba ya kulinda wawekezaji hawa.

“Mheshimiwa Spika kama kuna mchango ambao utakumbuka ni kupiga marufuku hii habari ya Certificate of Agency, kwenye utungaji sheria imetuletea matatizo makubwa na ‘mabomu’, sheria za gesi asilia na mafuta mlizotufukuza hapa na mkazipitisha ni ‘mabomu’ matupu.

“Katika taarifa hii ya jana, wamependekeza watu fulani fulani washughulikiwe; mawaziri, makamishna, Mwanasheria Mkuu bwana Chenge, Ngeleja, naombeni niwaambie kitu ili muwe na maarifa,” alisema Lissu.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=3aUsY3f2w7A[/embedyt]

Alisema yeye siyo  mtaalamu wa maandiko matakatifu, lakini kuna sehemu katika maandiko hayo inayosema kuwa watu wa Mungu wanaangamia kwa kukosa maarifa.

“Asubuhi umesema kwamba haya masuala ya madini yanahitaji semina, hilo ni jambo muhimu sana Mheshimiwa Spika kwa sababu hoja hiyo inahitaji maarifa sana na haiwezi kujadiliwa kwa hizi dakika tano tano au kumi kumi.

“Nataka nijikite katika masuala ya madini kwa sababu ambazo zipo wazi kabisa, Kamati ya Rais ya Profesa Osoro na Kamati ya Profesa Mruma iliyopita, si ripoti za kwanza kuzungumzia na kuchunguza matatizo katika sekta ya madini katika nchi hii na Rais Magufuli si wa kwanza.

“Mwaka 2002 Rais Mkapa  aliunda kamati iliyoongozwa na Mboma ambayo inaitwa Kamati ya Mboma, iliundwa kuchunguza matatizo katika sekta ya madini, hasa hasa madini ya vito vya thamani.

“Mwaka 2004 Waziri Mkuu Frederick Sumaye, Serikali ya Mkapa iliunda Kamati ya Dk. Jonas Kipokola kuchunguza matatizo ya sekta ya madini, taarifa yake ni ya Agosti 2004, mwaka uliofuata 2005 Rais Mkapa na Serikali yake waliunda Kamati ya Bukuku, alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, kuchunguza matatizo ya sekta ya madini.

“Mwaka 2006 miezi michache baada ya Rais Kikwete kutawazwa kuwa rais, akaunda Kamati ya Law Masha, bahati nzuri nimekuja na taarifa yake  hii hapa.

“Kamati ya Law Masha iliundwa kuchunguza sheria za madini, kodi na fedha na mikataba ya madini na kila kitu cha madini, taarifa hii hapa.

“Mwaka 2008 baada ya mgogoro wa Buzwagi hapa bungeni, Rais Kikwete aliunda Kamati ya Jaji Mark Bomani hii hapa, Kamati ya Bomani taarifa yake ni ya Aprili 2008.

“Kamati ya Osoro na Mruma ni kamati ya sita kuundwa kushughulikia masuala ya madini, sasa nimekuja na muhtasari wa Kamati ya Profesa Oroso.

“Naweza nikawaambia waheshimiwa wabunge hadidu za rejea za Kamati ya Mruma na Osoro ni zile zile zilizokuwa hadibu za rejea za Kipokola, Bukuku za Law Masha na za Kamati ya Bomani, matokeo yake, ‘Finding na Recommendation’ zipo hapa kwa kiasi kikubwa na Finding na Recommentantion zilizokuwa kwa Bukuku Kipokola Masha na Bomani hazijawahi kutekelezwa.

“Watu ambao wameuza madini ya nchi hii walipitisha sheria kwenye Bunge hili hili na ndio maana inashindikana,” alisema Lissu.

Akihitimisha Bunge jana jioni, Spika Ndugai, alisema amepokea ushauri wa Lissu kuhusu kutokubali kupitisha sheria kwa hati ya dharura na kusema endapo Serikali italeta sheria kwa dharura juu ya sheria za madini ama gesi, Bunge halitazipitisha kwa kuwa nchi imeibiwa vya kutosha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here